Header Ads Widget

Responsive Advertisement

MAKALA | Adhabu Mbaya Kuwahi Kutolewa na Mahakama Kwa Mtoto Mdogo George Stinney (14) , Inasikitisha Sana.

Image result for george stinney
Ni rahisi sana kusikia kwamba mtu amenyongwa au anasubiri adhabu ya kunyongwa. Lakini ni hisia ya tofauti kabisa kushuhudia uhai wa mtu ukiwa unatolewa hata kama ni kwa mujibu wa sheria. Ukikanyaga tu hata mguu wako ndani ya chumba cha kunyonga, kuna hisia ya tofauti sana ambayo inaweza kukufanya hata ukabwe na majinamizi usingizini maisha yako yote yaliyobaki.
.
.
Kuna namna nyingi za watu 'kunyongwa' ulimwenguni katika karne hii kama vile kitanzi, 'Firing Squad', Lethal Injection au Gas Chamber… lakini katika hizi zote hakuna adhabu ya kuogofya zaidi kuzidi adhabu ya kifo kwa kiti cha umeme (Electric Chair).
.
.
Ilikuwa inapata kama majira ya saa moja na nusu jioni hivi katika gereza la CCI (Central Correctional Institution) lililopo jimboni Columbia nchini Marekani ambapo moja ya kijana mdogo zaidi katika historia ya dunia kuhukumiwa adhabu ya kifo. Kijana huyu George Stinney alikuwa amebakiza dakika kadhaa tu za uhai wa maisha yake.
.
.
Katika utekelezaji wa adhabu ya kifo sidhani kama kuna muda wa kuogofya kuzidi dakika zile za mwisho kabla ya adhabu yenyewe kutekelezwa. Naamini maumivu ya uhai kumtoka mtu anayenyongwa hayafikii maumivu anayoyapata dakika chache akisubiria tukio lenyewe. Mfungwa kama anapaswa kutolewa uhai kwa umeme mkali, akikanyaga tu ndani ya 'chamber' yenyewe ya kutekeleza adhabu, mbele yake kabisa ataona dirisha kubwa sana la kioo ambalo kwa muda huo litakuwa limezibwa kwa pazia ya kitambaa. Upande wa pili wa dirisha hili wanakuwa wameketi watu kadhaa muhimu kushuhudia utekelezwaji wa adhabu hii. Ndugu wa karibu wa mnyongwaji, ndugu wa karibu wa 'victim', wawakilishi wa vyombo vya ulinzi waliohusika na kesi na mara kadhaa pia kunakuwa na mwandishi wa habari.
.
.
Kwenye upande mmoja wa ukuta kunakuwa na Mkuu wa gereza pamoja na maafisa kadhaa wa magereza. Pembeni yao lazima kunakuwa na simu ya mezani na mmoja wao anakuwa ameishikilia sikioni mwake muda wote. Lengo ni kuhakikisha kwamba kama kuna Rais (kwa nchi nyingi) au Gavana (kwa Marekani na nchi chache nyingine) anaweza kubadili mawazo yake dakika za mwisho na kuamuri adhabu hiyo isitekelezwe.

Katikati ya kijichumba hiki ndipo 'kifo' kilipo. Kuna kiti cha mbao cha ukubwa wa wastani lakini chenye muonekano tofauti kabisa. Kina mikanda, kama mikanda ya kujifunga kwenye ndege au basi… lakini mikanda hii iko usawa wa kifua, kiunoni na pia iko kwenye eneo la kuwekea mikono na miguu. Lakini pia miguuni kuna vipande vya metali ambavyo anayepaswa kutolewa uhai ugusishwa ili kusaidia kutiririka kwa umeme. Juu kabisa sehemu ya kuwekea kichwa kuna kidubwasha kama kofia yenye umbo la bilauri ambayo imeunganishwa na mkondo wa umeme wenye Volti 2,400. Ni umeme huu ndio ambao utatiririka kwenye mwili wa mfungwa na kumuondolea uhai ndani ya chini ya theluthi ya dakika.
.
.
Hiki ndicho chumba ambacho kijana George Stinney aliingizwa siku hii ya June 16, 1944 majira ya saa moja jioni. Alikuwa amevekwa nguo zake za kifungwa za rangi ya buluu zenye mistari myeupe. Kichwani amenyolewa kipara kama ilivyo desturi ya siku ya kukalia kiti hiki kwamba sharti anyolewe kipara ili kuhakikisha mkondo wa umeme kutoka kwenye ile kofia kama kibakuli unatiririka vyema kichwani mwake na kwenda kwenye mwili mzima.
.
.
Kuna muda woga ukizidi hata machozi yanakuwa hayatoki. Stinnley alikuwa anatetemeka kwa woga huku amekumbatia Biblia ambayo alikuwa ameingia nayo humu kutoka selo alikokuwa analala.
.
.
Maafisa wawili wa magereza wakamshika mikono na kumuongoza mpaka kwenye kiti na kumkalisha na kuanza kumfunga mikanda. Mikanda ilikuwa inashindwa kushikilia mwili wake sawa sawa kutokana na udogo wake. Hii ilikuwa ni mara ya kwanza katika historia kwa mtu wa umri wake kuhukumiwa kifo kwa kiti cha umeme. Kwa sababu hakukuwahi kuwa na mfungwa mwingine wa umri au umbo lake ambaye aliwahi kukaa kwenye kiti hicho, kiti kiliundwa ili kuweza kukaa wafungwa watu wazima. Kwa lugha nyingine kiti kilikuwa 'kinampwaya'. Hii iliwalazimu maafisa magereza waache kumfunga mikanda mwilini kwa njia rasmi kama unafunga mkanda kiunoni na badala yake wamfunge kienyeji kama vile wanafunga kuni alimradi tu asifurukute hapo kitini.Pia kutokana na kutoenea vizuri kwenye kiti kwa maana ya kimo chake kuwa chini mno… ilibidi watumie ile biblia aliyokuja nayo kumuwekea chini ya makalio aikalie ili awe juu juu kidogo.
.
.
Baada ya hapo kama ilivyo ada likachukuliwa sponji lililolowa maji na kukamuliwa kichwani. Kisha likaloweshwa tena maji na kuwekwa kichwani bila kukamuliwa. Kisha akavalishwa dubwasha lile kama kofia au bilauri ambalo limeunganishwa na mkondo wa umeme wa Volti 2,400 (ikiwa bado haijawashwa kuruhusu umeme kupita).
.
.
George Stinney, kijana wa miaka 14 alikuwa tayari kwa ajili ya kuondolewa uhai wake kama adhabu yake ambavyo ilikuwa imeelekeza. Upande mmoja wa chumba moja ya afisa gereza bado alikuwa na simu sikioni kusikia kama kuna lolote kutoka kwa Gavana. Kama ndani ya dakika mbili zijazo hakutakuwa na pingamizi lolote kutoka kwa Gavana, maana yake ni kwamba Mkuu wa Gereza anapaswa kutoa amri ya switch ya umeme ibonyezwe kuruhusu Volti 2,400 za umeme kutiririka kwenye mwili wa Mtoto George Stinney.
.
.
Lile pazia mbele ya hiki kijichumba likafunguliwa. Kuliuwa na kioo kikubwa kutenganisha chumba hiki na chumba kingine. Upande wa pili kulikuwa na kama watu thelathini hivi waliohudhuria kushuhudia utekelezani wa adhabu hii.
.
.
"Do you have anything to say?" Mkuu wa Gereza alimuuliza George.
.
.
Mtoto George. Woga ambao alikuwa usoni mwake ulitosha kabisa kukufanya ujue ni namna gani alikuwa anaogopa kile ambacho kiko mbele yake. Uhai wake kutolewa ndani ya dakika chache zijazo. Uso wake wote ulikuwa umejawa na machozi kutokana na kilio cha kwikwi ambacho amekuwa analia tangu alipoamka asububi ya leo.
.
.
George akainua uso wake kuwatazama wale mashuhuda wa upande wa pili. Kati ya wale watu theleathini ni watu wachache sana ambao aliwatambua. Lakini aliyemtambua zaidi alikuwa ni Johnson. Mtoto wa kizungu wa umri wake. Wanaokaa mtaa mmoja. Johnson ni kaka wa mabinti wawili ambao inadaiwa kuwa George amewaua.
.
.
"I am sorry Johnson… but I din't kill those girls.!"
.
.
Ndio maneno pekee ambayo George alifanikiwa kuyatamka katikati ya kwikwi yake ya kilio.Sijui kama Johnson alikuwa anaujua uhalisia na ukweli wa yaliyo nyuma ya pazia. Lakini na yeye machozi yalimbubujika kuona mtoto wa umri wake katika hali ile na akielekea kutolewa uhai mbele yake.
.
.
Lakini suala moja la kujiuliza ni namna gani ambavyo George amefikia kwenye hatua hii? Na binadamu wa namna gani wenye akili timamu ambao wanaweza kuthubutu kutoa uhai wa mtoto wa miaka 14?
Hii inatupeleka mpaka siku 85 zilizopita kabla ya siku ya leo.
.
.
Katika jimbo la South Carolina kuna mji mdogo unaoitwa Alcolu. Mji huu ulikuwa na pande mbili ambazo zilikuwa zinatenganishwa na reli iliyopita katikati. Upande mmoja waliishi watu weusi na upande mwingine waliishi watu weupe. Pia kulikuwa na shule na makanisa kwa ajili ya weupe na weusi.
.
.
Siku ya March 22, mwaka huo 1944 watoto wawili wa kizungu, Betty mwenye miaka 11 na Mary mwenye miaka 8 walikuwa wanaendesha baiskeli zao kama ilivyo ada ya michezo ya watoto. Baiskeli hii walikuwa wanaendesha upande wa mitaa ambayo wanakaa watu weusi. Kwenye mitaa hii ya weusi George Stinney mwenye miaka 14 alikuwa anaishi na baba yake, mama yake na kaka yake mkubwa mmoja na wadogo zake wawili.
.
.
Watoto wale wa kizungu inasemekana kuwa walipita mbele ya nyumba ya akina George (ambaye alikuwa amekaa nje na mama yake) na kuuliza ni wapi ambapo wanaweza kuchuma maua waende wakachezee. Mama yake George akawaelekeza na wale watoto wakaondoka zao.
.
.
Watoto hawa hawakurejea tena kwao. Ilipofika usiku familia ya wale watoto wa kizungu waliwataarifu watu wengine kuwa watoto wao hawajarejea nyumbani. Kwa hiyo wanaume wengi watu wazima (akiwemo baba yake George) wakajitolea kuanza msako wa watoto hao wawili wa kizungu kujua wamepotelea wapi.
.
.
Siku ya tarehe 23, March miili ya watoto wale wawili wa Kizungu, Betty na Mary iliokotwa porini ikiwa imetupwa ndani ya shimo lenye tope.
.
.
Kesho yake siku ya Tarehe 24 March magazeti yakatoka na vichwa vya habari kwamba polisi wanamshikilia 'mwanaume' mweusi anayeitwa George Stainney kwa maujia ya watoto wale wa kizungu.
.
.
Baba yake George akafukuzwa kazi kiwandani alikokuwa anafanya kazi. Wakafukuzwa kwenye nyumba waliyokuwa wanaishi (ilikuwa nyumba ya kampuni).George akahojiwa na Polisi bila uwepo wa wazazi wake wala mwanasheria. Na Polisi wakatoa taarifa kwamba George "amekiri" kufanya tukio hilo.
.
.
George akapandishwa kizimbani. Alipewa wakili wa utetezi ambaye alichaguliwa na serikali. Upande wa walalamikaji wakawasilisha "ushahidi" wao. Ambao hakukuwa na ushahidi wowote ule zaidi ya wao kusema kuwa George "amekiri" kutenda kosa. Wakili wa George ajabu ni kwamba hakuuliza swali lolote wala kufanya 'cross-examination' kama ilivyo ada ya wakili wa utetezi uendeshwaji wa kesi. Ushahidi wa Polisi ulikuwa na makandokando mengi mno. Kwani ulikuwa unajipinga wenyewe kwa wenyewe. Kwa mfano shahidi mmoja alisema kuwa George alishambuliwa na yule binti mkubwa wa kizungu na yeye (George) akachukua chuma cha reli na kuwapiga nacho kama kujitetea mpaka kuwaua.
Shahidi mwingine alieleza George aliwafuata nyuma nyuma kwa siri binti wale wakiwa wanatafuta maua mpaka walipofika sehemu isiyokuwa na watu na kuwavamia na kuwaua.
.
.
Lakini wakili wa utetezi hakusema chochote alikaa kimya kipindi chote cha kesi. Upande wa mashtaka ulitumia masaa mawili kuwasilisha kesi yao. Tofauti na ilivyozoeleka kwamba keshi za mauaji zinaweza kuchukua miaka au aghalabu miezi kadhaa mpaka kuisha, lakini masaa haya mawili ambayo yalitumika kuwasilisha keshi ndiyo ulikuwa muda ambao kesi ilidumu. Sio mwaka au mwezi au wiki. Bali kesi ilichukua masaa mawili tu. Kisha baraza na wazee (Jury) ambalo lote lilikuwa na watu weupe tupu lilikaa chemba kwa dakika 10 tu na kisha kurudi na uamuzi wa pamoja kwamba wamemkuta George na hatia na hivyo kupelekea mahakama kumuhukumu George adhabu ya kifo. Mahakama pia ikafunga uwezekano wa George kukata rufaa.
.
.
Twende mbele kidogo… miaka 70 baadae (Mwaka 2014)
.
.
Kesi hii tangu miaka ile ya ya 1940s ilizua utata mkubwa na utengano wa kijamii. Wengi waliamini kwamba kuna mtu halisi ambaye alifanya yale mauaji na lawama alikuwa anabebeshwa George kutokana na rangi yake ya ngozi.
Hata namna kesi ambavyo iliendeshwa ilikuwa inaakisi kabisa kwamba George alikuwa anakandamizwa kutokana na kuwa mtu mweusi.Kwa hiyo kuanzia miaka ya 2004, familia ya George, wanaharakati na taasisi za kitaaluma walianzisha vuguvugu la kutaka kesi ya George kusikilizwa upya. Hatimaye mahakama kuu ya Marekani ikaifungua tena kesi upya na ikaanza kuunguruma.
.
.
December mwaka 2014 mahakama kuu ilifuta adhabu ya kifo ambayo ilitolewa kwa George na kusema kwamba kwanza kabisa, kuna dalili ya George kuwa alilazimishwa kukiri kosa na Polisi baada ya kupigwa. Pili George hakupatiwa 'fair trial'. Pia hakupewa fursa ya kujitetea kwa ufasaha kama haki yake ya kikatiba. Lakini pia kesi haikuendeshwa kwa mujibu wa maadili na weledi wa kimahakama. Lakini pia mahakama kuu ililaani namna ambavyo mtoto wa miaka 14 kesi yake kuendeshwa namna ile na kutoa adhabu ya kifo kwa mtoto mdogo kienyeji vile.
.
.
Kwa hiyo George alifutiwa adhabu ya kifo na Mahakama Kuu. Lakini hii ni miaka 70 baada ya kisanga kile mwaka 1944. Je ni nini ambacho kilimpata George siku ile kwenye Electric Chair??
.
.
George 'alinyongwa' kwa kiti cha umeme siku ile ya June 16, 1944. Kwa taratibu za mfungwa kuuawa kwa electric chair, ni process ambayo inatakiwa ifanyike chini hata ya thelethi ya dakika. Lakini kunyongwa kwa George kulikuwa ni kwa kikatili mno au kama wazungu wasemavyo, gruesome! Ilichukua takribani dakika nne nzima.
Baada ya switch kuwashwa na mkondo wa umeme wa volti 24000 kuanza kutiririka kwenye mwili wake na kuanza kupaparika kukata roho, kofia ile ya umeme kama bilauri kichwani ilimvuka George na hivyo kulazimu iwekwe upya tena bila kuzima umeme.
.
.
Jambo la kusikitisha zaidi, mfungwa akiwa anauwawa kwa mfano kwa kitanzi au firing squad au kiti cha umeme huwa anaveshwa 'mask' kama kitambaa hivi ili kuficha uso wake. Lakini baada ya ile kofia ya umeme kumvuka George, uso wake ulibaki hadharani kuonyesha namna ambavyo macho yalikuwa yamemtoa karibia kudondoka huku uso ukiwa umejaa machozi na kamasi.
.
.
Ilikuwa ni moja tukio la kinyama zaidi katika mfumo wa unyongaji wa magereza nchini Marekani hasa ukizingatia aliyefanyiwa hivi ni mtoto wa miaka 14 tu.

Credits | Written and Compiled by Habib Anga - The Bold | RoryaFinest.com

Post a Comment

0 Comments