Moja kati ya sehemu ambazo zitatuchukua miaka mingi sana ili tuweze kufahamu kwa uhakika kabisa juu ya kile ambacho kinaendelea ndani yake basi ni eneo hili la RAF Mentwith Hill (Royal Air Force Mentwith Hill Station) ambalo liko maeneo ya Harrogate, North Yorkshire nchini Uingereza.
Eneo hili ni eneo la kijeshi na liko ndani ya nchi ya Uingereza, lakini ajabu ni kwamba eneo hili linamilikiwa na kuendeshwa na Wizara ya Ulinzi ya Marekani (DOD). Hata wafanyakazi kwenye eneo hili ni wamarekani kutoka idara za USAF na NSA. Makubaliano hasa kati ya nchi ya Uingereza na Marekani mpaka kufikia Marekani kukabidhiwa sehemu hii ya kijeshi bado ni siri kubwa.
Kituo hiki cha siri kubwa chenye kukaa kwenye ardhi yenye ukubwa wa kilomita 2 za mraba, kilifunguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1954 na British War Office (Wizara ya Ulinzi ya sasa ya Uingereza) na mwaka 1958. lakini kituo hiki kilitolewa kwa Marekani kupitia idara yao ya ASA ya kipindi hicho (US Army Security Agency) ambayo kwa sasa imeunganishwa kwenye idara ya Millitary Intteligence ambayo ni sehemu ya INSCOM (US Army Intelligence and Security Command). Lengo kuu la awali la kuanzishwa kwa kituo hiki lilikuwa ni kufuatilia mawasiliano ya mawimbi na kielektroniki nchini Urusi kipindi kile cha vita baridi.
Mwaka 1966 kituo hiki kilikabidhiwa kwa NSA (National Security Agency) kutoka kwa idara ya ASA ambao ndio awali walikabidhiwa na Uingereza.
Mara nyingi watu hujiuliza, kituo hiki kilianzishwa kwa lengo la kufuatilia mawasiliano ya kieletroniki nchini Urusi kipindi kile cha vita baridi… kwa nini kituo hiki bado kipo mpaka sasa? Je, kwa sasa kituo hiki kina kazi gani hasa?
Japokuwa shughuli zinazoendelea katika kituo hiki ni siri kubwa, lakini kumekuwa na taarifa za uhakika kwamba kituo hiki kinatumiwa na NSA kwa ajili ya kufuatilia mawasiliano ya watu wenye kutiliwa shaka ulimwenguni kote. Si hivyo tu kituo hiki pia kinatumiwa na NSA kunasa mawasiliano karibia yote ambayo wanaweza kuyapata… hata simu za raia wa kawaida tu.
Mfano mzuri ni skandali ambayo iliibuka mwanzoni mwa miaka ya 2000 ambapo iligundulika kwamba mwaka 1975 NSA kwa kushirikiana na shirika la mawasiliano la Uingereza waliunganisha mkongo wa mawasiliano katika mfumo wa mawasiliano ya simu za kimataifa zenye kupita nchini Uingereza katika kituo cha mawimbi cha Hunters Stones kwenda kwenye kituo cha kijasusi cha RAF Mentwith Hill na baadae mkongo huo kuboreshwa mwaka 1992 na kuwa wa fibre optics. Hii iliwawezesha NSA katika kituo cha RAF Mentwith Hill kuwa na uwezo wa kunasa na kurekodi zaidi ya simu 100,000 kwa pamoja na kwa wakati mmoja.
Lakini pia kituo hiki kinatumika kama Ground Station ya Satellite za kipepelezi za nchi ya Marekani.
Pia kumekuwa na taarifa za uhakika pia kuwa kituo hiki kinatumika kuratibu mashambullizi ya anga huko Mashariki ya Kati kwa kutumia “drones”. Mafungamano ya ECHELON na RAF Mentwith Hill Station
Kuna kitu kinaitwa ECHELON. ECHELON ni program maalumu ya kijasusi ambayo inaratibiwa na nchi zenye kujulikana kama “Five Eyes” kwenye jumuiya ya kimataifa kuhusu masuala ya ujasusi.
Ni kwamba katika miaka ya mwishoni mwa 1940s kulianza mafungamano ya kiintelijesia ambayo mwaka 1961 yalizaa makubaliano kati ya nchi za Marekani, Uingereza, Canada, Australia na New Zealand na makubaliano hayo kufanywa rasmi kiserikali mwaka 1971 ambapo walisaini mkataba unaoitwa UKUSA (UKUSA Security Agreement). Mkataba huu unatanabasiha maslahi ya pampja ya kiintelijensia kati ya nchi hizo na kufungua mlango wa kushirikishana taarifa za kijasusi ambazo zina maslahi yao nchi hizo zote tano kwa pamoja. Kama ulikuwa haufahamu basi hii ndio sababu ya nchi za Marekani na Uingereza na hata Cadana kuwa kama ndugu wa damu, kuwa na msimamo mmoja kwenye masuala karibia yote ya kimataifa na kushirikiana kupitiliza kufikia kiwango cha Uingereza kuonekana kama kibaraka wa Marekani. Pamoja na sababu nyingine lakini moja ya sababu kuu kabisa ni huu mkataba wa UKUSA na program ya ECHELON.
Sasa ECHELON ni “code name” ya program hii ya pamoja ya ‘surveillance’ ya kimataifa kukusanya na kuratibu na kuchambua intelijensia za mawimbi (SIGINT – Signal Intelligence) kati ya nchi hizi za ushirikiano wa “Five Eyes”.
Nadhani unaweza kuona tofauti ambayo mara nyingi ni rahisi kuchanganya. Miaka ya zamani ili kuweka tofauti hii bayana, mfumo wa ‘stone ghost’ ulikuwa unaitwa ‘Interlink-C’. Kwa kifupi basi, hiyo ndio RAF Mentwith Hill Station. Moja ya sehemu adhimu zaidi ulimwenguni. Moja ya sehemu ya siri zaidi ambpo mpaka sasa watu kwenye jumuiya za ujasusi duniani wanakuna mbongo kuweza kung’amua nini hasa ambacho kinaendelea ndani yake. Ni moja ya sehemu ambyo unaweza kuiona kwa mbali na majengo yake na mitambo yake yenye umbo la kuvutia mpaka watu kuibatiza jina mitambo hiyo kama ‘golf balls’ kutokana na umbo lake, lakini kamwe… abadani hata siku moja hatutaweza kukanyaga mguu ndani yake. Ni wachaguliwa wachache tu ndani ya NSA ambao ‘wanafaidi’ kuona upande wa pili wa ulimwengu… upande ambao unakupa nguvu ya kuweza kukulevya na muda mwingine kujihisi kama ulimwengu uko kiganjani.
Written & Compiled by Habib Anga | The Bold | roryafinets.com
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena