Wananchi wakiangalia nyumba iliyoteketea na kuangamiza familia nzima.
WATU
sita wa familia moja akiwamo Kapteni mstaafu wa Jeshi la Ulinzi la
Wananchi (JWTZ), wamekufa papo hapo baada ya kuteketezwa kwa moto jijini
Dar es Salaam. Janga hilo la moto limetokea
jana saa 10:30 alfajiri katika eneo la Kipunguni A, Ukonga Banana,
wilayani Ilala. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Mary Nzuki alisema jana
kuwa moto huo ulizuka ghafla katika nyumba inayomilikiwa na mstaafu
huyo wa Jeshi, David Mpira anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 55
na 60.
Alisema wengine waliokufa katika ajali hiyo ni mke wa
marehemu, Selina Yegela anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 50 na
55, ambaye pia ni mstaafu wa iliyokuwa Kampuni ya Kuhudumia Ndege
(DAHACO), sasa Swissport.
Aidha, moto huo pia umesababisha vifo
vya watoto wawili wanaokadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 20 na 30
ambao ni, Lucas Mpira na Samwel Yegela.
Kamanda Nzuki alisema
wajukuu wa marehemu nao wamekufa katika ajali hiyo, ambao ni Selina
Emmanuel (9) mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Minazi
Mirefu na Pauline Emmanuel (3), mwanafunzi wa chekechea katika Shule ya
Tumaini iliyopo Kitunda.
“Chanzo cha moto huo bado
hakijafahamika, tunaendelea na uchunguzi na tunashirikiana na Shirika la
Umeme (Tanesco) ili kubaini chanzo kilichosababisha moto huo,” alisema
Nzuki. Maiti wamehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na
uchunguzi bado unaendelea
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena