Header Ads Widget

Responsive Advertisement

FAHAMU ~ CESARE BORGIA Binadamu ambaye sura yake inatumika kama Kielelezo cha Sura ya Yesu na madhehebu ya Kikristo

 Image result for Cesare Borgia
Watu wengi sana wamejiuliza mara nyingi juu ya taswira ya Yesu Kristo wa Nazareth (4KK-30BK) kielelezo kikuu cha imani ya Ukristo kwa zaidi ya miaka elfu mbili sasa. Yesu Kristo hutajwa kama mwana wa Mungu na wafuasi wake kote ulimwenguni. Marejeo ya maisha ya Yesu Kristo yanabainishwa vema katika vitabu vinne vya injili vya Mathayo, Marko, Luka na Yohana katika Agano Jipya la Biblia Takatifu.
   Yesu mzungu
zimetapakaa kote ulimwenguni. Picha hizo zimekuwa zikizivuta kwa nguvu hisia za waumini ama wafuasi wake. Filamu ya Yesu Kristo nayo katika mkumbo huo, kama zilivyo picha zingine, zimeweka hisia katika mioyo ya wafuasi wake kama ni picha halisi za Yesu Kristo.
    Baadhi ya wadadisi na watafiti wamekuwa na maswali mengi kuliko majibu juu ya sura halisi ya Yesu Kristo. Lakini mwandishi Alexandre Dumas katika kitabu chake cha Volume One Of Celebrated Crime, anatanabaisha kwamba, picha nyingi zilizochorwa kuhusu Yesu Kristo wakati wa utawala wa Papa Alexander VI kati ya mwaka 1492 hadi 1503, zilibeba sura ya mtoto wa pili wa papa huyo, Cesare Borgia. Mwandishi huyo anasema kwamba, picha hizo ndizo zenye ushawishi mkubwa hadi leo hii, zikiwafanya wafuasi wake wengi kudhani ndiye Yesu Kristo.
    Maelezo mengine yanakiri kuwa, taswira ya Yesu Kristo ni kijana huyo Cesare Borgia kama ilivyochorwa katika kuta za kanisa na mchoraji Michaelangelo di Lodovice Bounarroti Simon (1475-1564). Mchoraji mwingine maarufu sana enzi hizo Altobello Melone, panapo mwaka 1520, kiasi cha miaka kumi na mitatu baada ya kifo cha Cesare Borgia, aliichora picha ya Yesu Kristo kwa kutumia taswira ya Cesare Borgia katika kazi yake The Walk To Emmaus. Pengine hali hii ilichochewa kwa kiasi kikubwa na nguvu kubwa ambayo Cesare Borgia na familia yake waliyokuwa nayo wakati huo kama ambavyo tutajaribu kutazama baadaye.
    Mwanamuziki Killah Priest (Walter Reed) wa kundi la muziki wa rap huko Marekani, panapo mwaka 1995 katika kibao chake alichokiita B.I.B.L.E (Basic Instructions Before Leaving Earth) ameimba;
    
    "I even learnt Caucasians were really the tribe of Edam,
    The white image of Christ, is really Cesare Borgia, and uhh,
    The second son of Pope Alexander, the Sixth of Rome,
    And once the picture was shown,
    That's how the devils tricked my dome…"
    
    Cesare Borgia alikuwa ni kijana mwenye sura nzuri yenye kuvutia mno. Ingawa maisha yake duniani yalidumu kwa takribani miaka thelathini tu, yale aliyoyafanya yalikuwa ni makubwa mno na kuacha athari kubwa katika maisha ya sasa hususani katika nyanja ya sayansi ya siasa.
    MJUE CESARE BORGIA
    Cesare Roderic Llancol de Borja ni mtoto wa pili wa Roderic Llancol de Borja (Rodrigo Borgia kwa Kitaliano) aliyekuwa papa wa kanisa Katoliki tokea mwaka 1492 hadi mwaka 1503 alipokumbwa na mauti kwa chanzo chenye utata hadi leo hii. Rodrigo Borgia ama Papa Alexander wa Sita, ni papa anayekumbukwa kama papa mwovu ama mafia kuliko mapapa wote waliowahi kuongoza Kanisa Katoliki.
    Papa Alexander VI alizaliwa huko Xativa, Valencia, Hispania panapo tarehe 1 Januari 1437, wazazi wake wakiwa Jofre Llancol y Escriva na Isabel de Borja. Roderic alitumia ubini wa mama yake, Borja kutokana na kupanda kwa mjomba wake, Alonso de Borja hadi kuwa papa mwaka 1455 na kuitwa Papa Calixtus III. Hivyo Roderic akapenda zaidi kutumia jina la mama yake kwani tayari lilikuwa likihusiana na mamlaka ya kanisa.
    Roderic de Borja alihitimu sheria huko Bologna. Baada ya mjomba wake kuwa papa, akapandishwa vyeo na kuwa askofu, kardinali na hatimaye Makamu wa Mkuu wa Kanisa (Vice-Chancellor). Cheo cha umakamu mkuu wa kanisa akadumu nacho chini ya mapapa watano, Calixtus III (mjomba wake), Pius II, Paul II na Innocent VIII. Hilo lilimfanya kupata uzoefu mkubwa katika masuala ya utwawala wa Kanisa Katoliki. Aliweza kujijengea ushawishi na utajiri mkubwa sana.
    Kufuatia kifo cha Papa Innocent VIII panapo mwaka 1492, makardinali waliokuwa na nafasi kubwa ya kuchaguliwa kuwa papa, walikuwa ni Borja mwenyewe, Ascanio Sforza na Giuliano della Rovere. John Burchard aliyehudumu kama mkuu wa itifaki katika nyumba ya papa chini ya mapapa kadhaa, aliandika katika shajara (diary) yake ya mwaka 1492 kwamba, kushinda kwa Roderic de Borja (wakati huo tayari akiwa amebadili jina na kuitwa Rodrigo Borgia, tafsiri ya Kitaliano ili kuondoa dhana ya kwamba yeye ni Mspaniola) kulitokana na kununua kura za makardinali. Hivyo Rodrigo Borgia ama Papa Alexander VI, anatajwa kama papa mpenda rushwa zaidi katika historia ya Kanisa Katoliki.
    Papa Alexander VI alikiri hadharani kuwa na watoto pamoja na mahawara. Alikuwa na watoto wengi, lakini watoto aliowafanya rasmi ni wale aliozaa na Vanozza dei Cattani ambao ni Giovanni (Juan), Cesare, Goffredo (Gioffre ama Jofre) na binti wa pekee Lucrezia (Crezia). Papa Alexander VI aliwapenda sana watoto wake hawa na aliyafanya maslahi ya kanisa kuwa maslahi ya watoto hawa. Alimwoza bintiye Lucrezia mara tatu tofauti kwa maslahi yake ya kisiasa, huku mume wa pili akiuawa ndani ya makazi ya papa.
    Cesare Borgia, mtoto wa pili wa Papa Alexander VI ama Rodrigo Borgia, anasemekana kuzaliwa kati ya mwaka 1475 na 1476, ingawa tarehe rasmi imewekwa kuwa 13 Septemba 1475 wakati huo Rodrigo akiwa kardinali na makamu mkuu wa kanisa. Mwandishi Stefano Infessura anaeleza kuwa, awali Cesare Borgia alikataliwa na Rodrigo Borgia. Rodrigo Borgia alidai Cesare ni mtoto wa mtu mwingine aliyewahi kutembea na Vanozza dei Cattani, Kardinali Giuliano della Rovere, aliyekuwa adui mkubwa wa Kardinali Rodrigo Borgia. Lakini baadaye ikathibitika kuwa ni mtoto halali wa Kardinali Borgia. Kwa macho yake ya kahawia na nywele nyeusi, Cesare Borgia anaelezwa kuwa mtoto mwenye sura nzuri mno ya kupendeza na umbo zuri na kubwa lenye kuvutia sana kama la baba yake.
    Cesare Borgia alianza kupanda vyeo vya kikanisa kama Askofu wa Pamplona akiwa na umri wa miaka 15. Akiwa amehitimu sheria huko Perugia na Pisa, na baba yake kupata upapa, Cesare Borgia akafanywa kuwa kardinali wa Valencia akiwa na umri wa miaka 18. Papa Alexander VI alipenda sana Cesare Borgia aje awe papa ili aendelee kuyalinda maslahi ya familia ya Borgia. Familia ambayo mwandishi Mmarekani mwenye asili ya Italia, Mario Puzo, katika riwaya yake ya mwisho na maarufu, The Family, anaitaja kama familia ovu kuliko zote zilizowahi kutokea Italia katika kipindi cha mvuvumko na mwamko-sanaa (renaissance).
    Cesare Borgia hakuvipenda vyeo vya kanisa. Alihitaji zaidi nafasi katika jeshi la papa. Alipenda aje aoe na kuwa na watoto halali na siyo haramu kama wao. Baba yake, badala yake akampa Giovanni kuwa Kepteni Jenerali wa majeshi ya papa, jambo ambalo halikumridhisha Cesare Borgia hata kidogo. Papa Alexander VI akaendelea kusisitiza nia yake ya kutaka maisha ya Cesare Borgia yawe kanisani.
    Lakini siku moja katika mwaka 1497, katika mazingira yenye utatanishi mkubwa sana, Giovanni aliuawa na maiti yake kuokotwa pembezoni mwa mto Tiber ikiwa imenyofolewa pua na baadhi ya sehemu. Watu wengi wakamtuhumu Cesare Borgia kuwa amemuua ndugu yake ili apate ukuu wa majeshi. Ingawa ukweli ni kwamba Giovanni (Juan) aliuawa na ndugu yake mwingine Goffredo (Jofre) kwa sababu za wivu wa mapenzi baada ya kubainika Giovanni kutembea na mke wa mdogo wake, Goffredo, Sancha ama Sancia wa Aragon. Sancha alikuwa akitembea na Giovanni na Cesare wakati huo huo.
    Hata hivyo, Cesare Borgia bado alikihitaji mno cheo hicho. Ili akipate, tarehe 17 Agosti 1498, Cesare Borgia alijiuzulu ukardinali na kuwa mtu wa kwanza katika historia kujiuzulu cheo hicho, cheo kilichootwa na viongozi wengi wa kanisa. Siku hiyo hiyo, Mfalme Louis XII wa Ufaransa akamtawza Cesare Borgia kuwa mtawala huru (Duke) wa Valentinois. Hii ndiyo asili ya jina la utani la Cesare Borgia, Valentino, kutokana na kuwahi kuwa kardinali wa Valencia na sasa mtawala huru wa jimbo.
    Cesare Borgia akamwoa Charlotte d'Albret (Lottie, ndivo alivyopenda kumwita) dada wa Mfalme John III wa Navarre. Akateuliwa kuwa balozi maalumu wa papa katika Ufaransa, nchi iliyokuwa na uhusiano mzuri na papa huyo. Pia akateuliwa na Papa Alexander VI kuwa Kepteni Jenerali wa majeshi ya papa akiwa na wajibu mkubwa wa kupanua na kuimarisha mamlaka ya papa wa Roma.
    Akiwa kijana mwenye nguvu, alikuwa na jeshi imara sana lililopata sapoti ya hali na mali kutoka kwa papa. Mwaka 1499 hadi 1500, Cesare Borgia aliweza kuudhibiti mji wa Romagna. Baadaye mwaka uliofuatia, Papa Alexander VI akamtawaza kuwa mtawala huru wa jimbo la Romagna. Kuitwaa Romagna yalikuwa ni mafanikio makubwa sana katika kuipa nguvu mamlaka ya papa kutokana na utajiri mkubwa jimbo hilo. Wananchi wa Romagna waliukaribisha utawala wa papa kwa mikono miwili. Jeshi la papa lilikuwa na nguvu sana huku likijivunia kutumia mapato ya kanisa Katoliki chini ya uungwaji mkono kwa asilimia zote na Papa Alexander VI.
    Kipindi kilichofuatia kilikuwa ni kipindi chenye mafanikio makubwa sana katika operesheni za kijeshi za Cesare Borgia. Panapo mwaka 1502, mpiganaji hodari Cesare Borgia, aliweza kuitwaa miji ya Piombino, Elba na Camerino. Pia kwa kufanikiwa kuidhibiti Urbino, aliweza kuupata utawala wa jimbo hilo huku mkakati wake mwingine ukiwa ni kudhibiti jimbo la Bologna. Lakini kutokana na ukatili wake, baadhi ya viongozi wakafanya njama dhidi yake. Cesare Borgia alijaliwa maarifa sana, akazimaizi njama hizo. Kwa kutumia vema akili aliyobarikiwa, akafanya nao muafaka. Mwandishi Paolo Giovio anasema kwamba, viongozi wale walipoingia kwenye mtego huo, waliishia kufungwa na kunyongwa hadharani siku ya mkesha wa mwaka mpya wa 1503. 
    Mwaka 1503, matukio makubwa mawili yalisababisha kuanguka kwa Cesare Borgia. Tukio la kwanza ni pale majeshi ya Hispania yalipoigeukia Ufaransa na kuiondoa kusini mwa Italia. Cesare Borgia alikubali kushindwa huko.
    Tukio la pili lililokuwa kubwa zaidi, ni kifo cha baba yake, Papa Alexander VI. Siku moja mwanzoni mwa mwezi Agosti 1503, wakiwa katika dhifa kwenye makazi ya papa, Cesare Borgia na Papa Alexander VI walikunywa sumu kwa bahati mbaya. Inadaiwa kuwa sumu hiyo ilikusudiwa kwa Kardinali Giuliano della Rovere, aliyekuwa adui mkubwa sana wa familia ya Borgia. Cesare aliweza kupona baada ya kuugua muda mrefu, huku Rodrigo Borgia, Papa Alexander VI akifariki dunia tarehe 18 Agosti 1503. Ingawa maelezo mengine hudai Papa Alexander VI alifariki kwa ugonjwa wa malaria, ukweli unabaki kuwa alifariki kwa sumu hasa kutokana na hali ya mwili wake baada ya kifo chake. Mwili huo ulibadilika rangi na kuwa mweusi. Kabla ya kukumbwa na mauti akiwa hoi kitandani, alifanikiwa kutubutu madhambi yake ili apate msamaha wa dhambi. Mwili wake ulizikwa Saint Peter's Basilica huko Vatican City, Italia.
    Baada ya kifo cha papa, kwa ushawishi mkubwa sana wa Cesare Borgia, Kardinali Francesco Todeschini Piccolomini akachaguliwa kuwa Papa Pius III tarehe 22 Septemba 1503. Kardinali huyu alikuwa muungaji mkono mzuri wa familia ya Borgia. Hata hivyo hakudumu sana kwani alifariki dunia siku chache baadaye hapo tarehe 18 Oktoba 1503.
    Makardinali walipokutana tena mwezi Oktoba ili kumchagua papa mpya, Kardinali Rovere akamwahidi Cesare Borgia kuwa angeyalinda maslahi ya familia ya Borgia na kuendelea kutoa pesa ili kufanikisha mikakati ya ya Cesare ya kijeshi, wakati huo akiwa anaikusudia Tuscany. Cesare Borgia akamwambia kuweka ahadi hiyo katika maandishi ili baadaye asije kumgeuka. Kardinali Rovere akafanya hivyo. Hivyo kwa ushawishi wa Cesare Borgia, Kardinali Rovere akachaguliwa kuwa Papa Julius II.
    Lakini mwezi Disemba mwaka huo huo, Papa Julius II akamgeuka Cesare Borgia na kuagiza akamatwe na mali zote za familia ya Borgia zikakamatwa. Cesare Borgia akakamatwa na kufungwa na Gian Paolo Baglioni karibu na Perugia. Akafanikiwa kukimbilia Naples ili kutafuta msaada kwa ndugu na marafiki. Lakini wote Papa Julius na Ferdinand wa Aragon waliuogopa sana uwepo wa jeshi la Borgia. Hivyo wakafanikiwa tena kumfunga Cesare Borgia, safari hii ikiwa huko Castle de La mota, Medina del Campo. Hata hivyo panapo mwaka 1506, Cesare Borgia akafanikiwa kutoroka na kwenda Navarre ambako mfalme wake Jean d'Albret alikuwa ni shemeji yake kwa mke wake Charlotte.
    Mfalme Louis XII wa Ufaransa akagoma kumrudishia Cesare maeneo yake ya utawala, na zaidi akataka hata kuitwaa Navarre kwa sapoti ya familia za kikabaila. Cesare Borgia akaingia vitani kumpigania shemeji yake Mfalme John III wa Navarre. Akafariki katika mapambano makali huko Viana hapo tarehe 12 Machi 1507.
    Cesare Borgia aliacha watoto takribani kumi na moja lakini rasmi wakiwa ni Girolamo Borgia aliyekuja kumwoa Isabella Contessa di Capri na Lucrezia Borgia ambaye baada ya kifo cha baba yake aliamua kwenda kuungana na shangazi yake Lucrezia Borgia huko Ferrara.
    Cesare Borgia alizikwa katika kaburi la maru maru pembeni ya madhabahu ya kanisa la Santa Maria kukiwa na maandishi, "Hapa amelala katika ardhi changa mtu aliyeogopwa na wote, aliyeishika amani na vita katika mkono wake."
    Mwaka 1537 Askofu wa Calahorra alilitembelea kanisa hilo na kushtushwa na kusikitishwa kwa mtu mwenye dhambi kama Cesare kuzikwa mahali patakatifu. Akaagiza kaburi hilo libomolewe na mabaki yake yahamishiwe nje ya kanisa ili yakanyagwe na watu na wanyama. Ikawa hivyo.
    Mabaki hayo yakakaa hapo nje hadi mwaka 1945, yalipochimbuliwa kwa bahati mbaya na watu waliokuwa wakifanya kazi katika eneo hilo. Wanasiasa kadha wa eneo hilo wakaliomba Kanisa Katoliki kupa maziko maalumu.
    Mwaka 2007, Fernando Sebastian Aguilar, Askofu Mkuu wa Pamplona akatoa kibali kwa mabaki hayo kurudishwa ndani ya kanisa. Hivyo mabaki hayo yakarudishwa kuzikwa sehemu ile takatifu hapo 11 Machi 2007 ikiwa ni siku moja kabla ya kuadhimisha miaka 500 ya kifo chake. Kanisa hilo likasema, "Chochote alichokifanya katika maisha, anastahili kusamehewa sasa."

Post a Comment

0 Comments