Header Ads Widget

Responsive Advertisement

Riwaya Ya Kijasusi | Kikosi cha Kisasi Sehem ya 2


Image result for african spies
SURA YA PILI
DAR ES SALAAM
Mjini Dar es salaam, kama ilivyo katika miji mingine yoyote Ulimwenguni, kulikuwa kumejaa pilikapilika siku hii ya jumamosi usiku. Saa tano hizi za usiku pilikapilika zilikuwa bado nyingi sana. Watu wengi waliokuwa wameanza starehe za Jumamosi mapema mchana walikuwa wanarejea nyumbani kupumzika, wakati wengine waliokuwa wameanza starehe jioni, walikuwa wamo katikati ya sherehe na wakati ule ule walikuwa na kundi jingine ambalo ndipo lilikuwa linaanza pilikapilika za sherehe saa tano hizi.
Katika msululu wa magari yaliyokuwa kwenye barabara ya Morogoro yakitokea mjini kuelekea sehemu ya Ubungo, mlikuwa na gari moja aina ya 'Colt Gallat Coupe' nambari TZ 300130 ambayo ndani yake mlikuwa na kijana mmoja nadhifu sana na msichana mmoja mrembo sana, ambao walikuwa katikati ya ubishi.
"Mimi nakwambia twende Mlimani Park," alisema yule kijana.
"Nieleze kwa nini tusiende Safari Resort?" Aliuliza yule msichana.
"Bendi mpya ipo pale ya Zaire."
Yaani wewe unafuata upya wa bendi au bendi yenyewe ilivyo."
"Basi Lolita mpenzi, tutakwenda Safari Resort," alijibu yule kijana huku akiongeza mwendo wa gari.
"Lakini usije ukawa umeudhika, ee Willy mpenzi."
"La hasha, ningekuwa sikuridhika ningekuambia, bila kusita." Kusema kweli magari mengi yalikuwa yakielekea kwenye klabu moja maarufu sana iitwayo Resort iliyoko sehemu ya Kimara. Kwa hivi baada ya watu hawa kukubaliana kwenda kustarehe usiku huu huko Safari Resort walielekea moja kwa moja mpaka kwenye klabu hiyo. Walipoingia ndani ya klabu hii walikuta watu tayari walikuwa wamejaa. Muziki ulikuwa ndipo umepamba moto.
"Loo Willy rekodi hiyo mimi naipenda," alisema Lolita mara tu walipoingia ndani,
"Twende tukacheze alijibu Willy. Bila hata kutafuta mahala pa kukaa kwanza waliingia kwenye uwanja wa kucheza na kuanza kulisakata rumba.
Baada ya rekodi hii kwisha, walitoka na kuanza kutafuta mahala pa kukaa.
"Willy karibu huku," Meneja wa klabu alimkaribisha. Meneja wa klabu hii alikuwa amemwona Willy wakati akiingia, na kwa sababu alikuwa akimheshimu sana, alimtafutia mahala pa kukaa ili asipate taabu kutafuta.
"Asante sana Rajabu, hujambo lakini?"
"Mimi sijambo, je wewe?"
"Alhamdulillahi Mungu anasaidia".
"Oh, samahani bibie tabia yangu inataka kuwa mbaya kwa kutokusabahi kwanza, hujambo?"
Rajabu alimsalimia Lolita huku akiwakalisha kwenye meza aliyokuwa amewatayarishia.
"Sijambo mimi" alijibu Lolita huku akiketi.
"Ngoja niwajulishe, huyu ni Lolita rafiki yangu," alimjulisha Lolita kwa Rajabu, "Na huyu ni rafiki yangu vile vile ndiye Meneja wa hapa," alimjulisha Rajabu kwa Lolita.
"Nafurahi kukuona," Rajabu alimwambia Lolita.
"Na mimi pia nafurahi kukuona" alijibu Lolita.
Kisha Rajabu aliwaagizia vinywaji, "Sijui bibie utapendelea kunywa nini?".
"Nafikiri itanifaa safari".
"Na wewe Willy?".
"Na mimi hiyo hiyo itanifaa kwa kuanzia."
Vinywaji viliagizwa na Rajab akaondoka.
"Willy," Lolita aliita kwa mshangao, Willy akajua kwanini?.
"Mara nyingi huwa nafika hapa kiasi cha kwamba huyu meneja amenizoea."
"Ndiyo sababu ulikuwa hutaki kuja huku au sivyo?"
"Nilitaka libadilisha mazingira kidogo."
"Mahala pazuri sana miye huwa napasikia tu sijawahi kufika, rekodi za bendi hii huwa nazisikia tu ndani ya redio, ama kweli anapiga sana."
"Ni mahala pazuri sana."
Vibywaji vilifika na kuanza kunywa huku wakiwa mara kwa mara wakiondoka kwenda kulisakata rumba.
Kiasi cha saa saba hivi usiku, wakati Willy na Lolita wakilisakata rumba uwanjani Willy alimuona Rajabu akielekea mezani kwao ambayo ilikuwa tupu. Alitazama kule na huku akionyesha dalili kuwa alikuwa akiwafuata.
"Nadhani Rajabu anatufuata," Willy alimwambia Lolita.
"Umemwona wapi?" aliuliza Lolita huku akiendelea kucheza.
"Yuko pale mezani kwetu."
"Ina maana wewe unacheza na huku ukiangalia mezani petu!"
"Inabidi nifanye hivyo Lolly mpenzi, maana hakuna mtu anayelinda meza yetu, anaweza kutokea mhuni au mlevi akanywa pombe yetu au akamwaga. Vile vile anaweza akatokea mtu anayechukia wewe au mimi akatuwekea sumu ndani ya pombe yetu,"
"Usiseme hivyo Willy, mimi sina mtu anayenichukia kiasi hicho. Lo ondoa wazo kama hilo."
"Huwezi kujua, dunia ya siku hizi imejaa fitina tupu. Hebu twende tukamwone huenda anatuhitaji naona kama ana wasiwasi hivi!"
Kwa shingo upande Lolita alikubali kuondoka maana muziki waliokuwa wakiucheza ulikuwa muziki taratibu uliokuwa ukiliwaza mioyo ya wachezaji na wasikilizaji wote hawa waliokuwa katika mapenzi.
"Kuna simu yako ofisini kwangu", Rajabu alimwambia Willy kwa shauku walipomkaribia.
"Asante" Willy alijibu kisha akamgeukia Lolita ambaye alikuwa akimwangalia kwa mshangao akamwambia, "Mpenzi, ningoje nikasikilize simu mara moja."
"Nani anakupigia simu saa saba hizi za usiku?" Aliuliza Lolita.
"Nitamjuaje kabla sijaisikia simu yenyewe?" Alijibu Willy.
"Amejuaje kama uko hapa? Je kama tungeebda Mlimani Park?".
"Nitajuaje kuwa amejua niko hapa kabla sijasema naye Loly mpenzi?"
"Haya baba nenda", alijibu Lolita kwa sauti ya kutoridhika.
"Wasichana watu wa ajabu sana, kwa mawazo yake anafikiri simu hii inatoka kwa msichana mwingine", alilalama Willy huku wakielekea ofisini kwa Rajabu.
Msichana akikupenda sana basi ujuwe amejawa na wivu juu yako, lakini hata hivyo Willy kama msichana hakuonei wivu ujuwe hakupendi. Hii inaonyesha waziwazi kuwa msichana huyu anakupenda sana", alisema Rajabu huku wakiingia ndani ya ofisi.
Bila kumjibu Rajabu, Willy aliiendea simu na kuinua.
"Helo, nani mwenzangu?" aliuliza.
"Unastarehe tu mwenzetu, leo una chuma kipya nini?" alijibiwa.
"Aah Maselina uko wapi?"
"Nipo nyumbani kwangu, nimejaribu Mlimani Park sikupata ikabidi nijaribu hapo, vipi muziki hapo."
"Muziki safi tu, natumai hukunipigia saa hizi kuniuliza muziki hapa ukoje." alijibu Willy kwa sauti nzito.
"Usiwe mkali baba, kwa taarifa yako kama ulikuwa na mipango ya starehe na hicho chuma ulichonacho basi sahau. Nimepata simu muda mfupi uliopita toka kwa Chifu, kwa hiyo njoo hapa kwangu haraka iwezekanavyo nina salamu zako maalumu," alijibu kwa sauti ya utani.
Lakini kwa sababu Willy alikuwa akimwelewa sana Maselina, uso wake ulionyesha kuwa ulikuwa umezingatia vizuri sana ujumbe huu.
"Asante sana, nakuja," halafu akamgeukia Rajabu, Sisi sasa tutaondoka"
"Vipi kuna matatizo nyumbani mbona haraka hivi baada ya kupata hiyo simu?"
"Hapana, hakuna matatizo yoyote ila kumefika wageni nyumbani, nilikuwa nimeacha ujumbe kuwa wakifika wakati wowote nielezwe."
"Aisii, basi karibu tena wiki ijayo, mlete huyu mrembo tena maana hajastarehe vizuri leo."
"Bila shaka nitamleta".
"Oke Willy niagie na mrembo huyo."
"Asante, nitakuagia. Kwa heri."
"Kwa heri asante", waliagana kwa kupeana mikono.
Alipokuwa akirudi kwenye meza yake, mawazo yake tayari yalikuwa kazini yakifikiri salamu zake kutoka kwa Chifu zitakuwa salamu za namna gani.
Alipofika mezani pake alimkuta Lolita anazozana na kijana mmoja aliyekuwa anataka kwenda kucheza naye kwa nguvu.
"Vipi ndugu mbona unakuja kufanya fujo hapa?" alimuuliza huyo kijana.
"Siyo fujo ila tu na mimi nataka kupata fursa ya kucheza na mrembo huyu itakuwaje tukuachie wewe ufaidi vyote peke yako?" Yule kijana alijibu kwa dharau. Willy alimwangalia akagundua kuwa tayari alikuwa ameishalewa vibaya sana.
"Twende zetu Loly, achana naye huyu kisha lewa."
"Afadhali umekuja mapema alitaka kunivuta kwa nguvu", alijibu Lolita huku akisimama.
"Haya kaka nenda kafaidi peke yako. Lakini nakupa onyo usije na mrembo kiasi hiki siku nyingine lazima nitakufanyia fujo," alisema yule kijana.
"Sawa mshindi ni wewe," alijibu Willy kwa dharau huku wakiondoka akiwa amemkumbatia Lolita kiunoni.
Macho ya watu wengi yaliwaangaza huku wakidiliki kusema.
"Lo, kweli vijana hao wanapendeza kwa uwili wao", kusema kweli vijana hao walikuwa wanapendeza sana. Kuchaguana walikuwa wamechaguana. Willy alikuwa mwenye sura ya kupendeza sana. Mavazi yalikuwa yakimkaa kama vile alizaliwa nayo kwa hivyo yalimfanya azidi kupendeza kiasi ambacho kila mtu aliyemuona alikiri kuwa alikuwa kijana nadhifu sana. Kwa jinsi hii haikuwa vigumu kwa Willy kuwa na uhusiano mzuri na wasichana wengi. Kwa upande wa mapato Willy alijulikana kuwa kijana mwenye kipato cha juu. Watu wengi hawakuelewa hasa alikuwa akifanya kazi gani, ila tu walijuwa alikuwa anashughulikia biasahara akiwa kama wakala wa makampuni ya nchi za nje katika Tanzania. Kwa hivi kusafirisafiri nchi za nje ambapo huyu kijana alikuwa akifanya mara kwa mara kuliweza kueleweka vilevile. Lakini ukweli wenyewe ni kwamba kijana nadhifu huyu hakuwa mfanyabiashara ila alikuwa mpelelezi maarufu katika Afrika jina lake kamili akiitwa Willy Gamba, ila watu wengi walijua jina lake la kwanza, kwa hiyo kila mtu alimwita kwa jina la Willy.
Msichana aliyekuwa amefuatana naye usiku huu alikuwa msichana rafiki kati ya rafiki zake wasichana wachache aliokuwa nao mjini Dar es Salaam. Msichana huyu alikuwa akifanya kazi na shirika la Reli Tanzania kama mwandishi muhtasi.
Kati ya wasichana wazuri mjini Dar es Salaam huyu msichana alikuwa mmoja wao, kwani alikuwa mrembo hasa. Alikuwa na umbo zuri kiasi cha kwamba kila apitapo watu humwangalia. Toka chini hadi juu alitosheleza kuitwa mrembo kwa kila hali. Kwa hiyo vijana hawa walipoonana hawakuwa na budi kupendana, kwani kwa uwili wao walipendeza sana kwani walionekana kama mapacha.
"Simu ilikuwa inatoka wapi?" aliuliza Lolita.
"Ilikuwa ni simu ya kikazi."
"Mteja wangu mmoja wa Lusaka amefika kuniona. Alipofika amepiga simu kwa mwandishi muhtasi wangu ambaye alianza kunitafuta mpaka amenipata. Kwa hivi inanibidi nikamuone sasa," Willy alidanganya.
"Kwanini usingoje kesho, yanini kumfuata usiku huu," Lolita aliendelea kudadisi,
"Unajua tena shughuli za kikazi, wateja wangu ni wafanyabiashara kama unionavyo mimi, kwa hiyo anaweza kuwa anasafiri kesho asubuhi huenda ndiyo maana ananihitaji haraka hivi," alizidi kudanganya.
"Lo, mwandishi wako lazima awe na kazi sana, kuamshwa usiku hivi na kuanza kukutafuta! Je kama na yeye angekuwa ameenda kustarehe huyo mteja wako angekupataje?" Lolita aliuliza.
"Kama mimi niko nje lazima mwandishi wangu yuko nyumbani na kama yeye yuko nje mimi niko nyumbani, hii ni sheria yetu ya kazi maana kazi yetu tunaweza kuhitajiwa na wateja wetu saa yoyote ofisini au nyumbani."
Walielezana yote haya huku wakielekea mjini wakirudi kutoka Kimara, "Sasa Loly mimi nitakupeleka mpaka nyumabani kwangu, halafu mimi nitakwenda nikaonane na huyu mgeni, mara moja nitakukuta."
"Lakini usikawie, eh Willy mpenzi."
"USiwe na wasiwasi, nitarudi mara tu nimalizapo mazungumzo." Kwa sababu saa hizi za usiku magari huwa hakuna, iliwachukuwa muda mchache kufika nyumabani kwa Willy, sehemu ya Upanga. Walipofika nyumbani, Willy alifungua nyumba wakaingia ndani.
"Mpenzi nenda kapumzike mimi nitarudi sasa hivi."
"Willy mpenzi, usikawie." Alilalamika Lolita huku Willy akimvuta na kumpa busu motomoto walikaa hivi kwa dakika mbili hivi ndipo akamwachia.
"Kalale Loly, nakuja sasa hivi," Willy alisema na kuondoka aliingia ndani ya gari lake akawasha moto kuelekea sehemu ya Mikumi ambako ndiko Maselina alikuwa akiishi. Wakati akielekea kwa Maselina, Willy alimfikiria sana Maselina. Alimfikiria kuwa msichana shupavu sana katika kazi yake. Maselina alikuwa mwandishi wa siri wa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Tanzania ambaye kiofisi alijulikana kama Chifu. Alikuwa na umri upatao miaka ishirini na sita (26) na alikuwa ameisha fanyakazi katika idara hii kwa muda wa miaka sita. Kwa ajili ya ushupavu wa kazi yake baada ya kuwa na idara hiyo kwa muda wa miaka mitatu aliweza kuchaguliwa kuwa mwandishi wa siri wa Chifu. Bado alikuwa hajaolewa na ilikuwa vigumu kujuwa ni kwa sababu gani kwani kama ni kwa uzuri alikuwa mzuri wa kutosha na kama ni kwa tabia alikuwa na tabia nzuri sana. Wafanyakazi wenziwe walifikiri kuwa huenda kazi aliyokuwa akiifanya ilimfanya asiweze kuolewa kwani kazi kama ile kwa mwanamke aliyeolewa ingekuwa ngumu kuitekeleza, Hata Willy alikubaliana na mawazo haya. Kila Maselina alipokuwa akiulizwa na marafiki zake juu ya suala hili la kuolewa alitabasamu tu na kusema, "Muda wangu wa kuolewa bado haujafikia", Willy na Maselina walikuwa wakielewana sana kikazi na kuelewana huku kulijenga urafiki wa aina yake kati yao. Watu wengi walifikiri kuwa walikuwa katika mapenzi lakini ukweli ni kuwa hata siku moja wazo hilo haliingia mawazoni mwao ingawaje siku zingine walikuwa wakienda kwenye starehe pamoja. Ili kuueleza urafiki kati ya Willy na Maselina nitaeleweka vizuri nikisema urafiki huu ulikuwa kama wa mtu na dada yake.
Ilikuwa saa nane za usiku wakati Willy aliposimamisha gari mbele ya nyumba ya Maselina. Taa ilikuwa ikiwaka sebuleni iliyoonyesha kuwa Maselina alikuwa macho akimsubiri Willy, "Karibu Willy, inakuchukua mwaka kutoka Kimara kufika hapa au ilibidi ukakifiche hicho chuma chako kabla ya kuja hapa!".
"Hauko mbali sana na ukweli," alijibu Willy huku akiingia ndani na Maselina alirudishia mlango.
Maselina alikwenda kufungua barafu akatoa chupa ya Konyagi na vpande vya barafu na ndimu akatenga bilauli mbili na kuweka Konyagi kwa ajili ya Willy na akatayarisha nyingine kwa ajili yake mwenyewe.
"Nimepata simu kutoka kwa Chifu, masaa machache yaliyopita," alieleza Maselina huku akiketi kitako, "Anakutaka ufike Lusaka kabla ya kesho mchana. Ameeleza kuwa kuna jambo muhimu sana kiasi cha kwamba unaweza ukahitajika kusafiri bila kurudi hapa Dar es Salaam. Kwa hivi ameamru kuwa ufanye safari yako kamili kamili kabisa. Hii Willy ina maana kuwa kuna safari nyingine kabambe inakungoja maana kufuatana na maelezo ya Chifu inabidi uende ukiwa na vyombo vyako vyote. Kuna ndege ya jeshi la Zambia ambayo ilifika hapa kuchukua mizigo yao, tayari mipango imeishafanywa uondoke nayo. Rubani wa ndege hiyo anazo habari kuwa atakuwa na abiria ambaye anahitajiwa kuhudhuria mkutano wa bodi ya wakurugenzi ya Tazara ambao unaendelea huko mjini Lusaka. Kwa hivyo utasafiri kama mfanyakazi wa Tazara hadi Lusaka ambapo utaonana na Chifu kwa maagizo zaidi. Ndege itaondoka saa nne asubuhi kwa hiyo nenda ukajitayarishe. Jina lako alilopewa rubani huyo ni Marko Mabawa, Meneja wa Shirika la Reli la Tazara. Nimempigia Wilson simu anakutayarishia hati ya kusafiria kwenda Lusaka kwa jina hilo ambayo ataileta moja kwa moja kwako asubuhi hii ya leo. Mambo mengine yamebaki juu yako kutekeleza. Je una swali kutokana maelezo hayo?" (Hapa Maselina alipumzika huku akimwangalia Willy kwa matumaini).
"La hasha", Willy alijibu, "Nafikiri nimekuelewa kwa ufasaha kabisa. Lililobaki ni dukuduku moyoni mwangu kuna nini huko Lusaka, maana hata jinsi Chifu alivyoitwa na kuondoka ilikuwa kiajabu ajabu. Hata hivyo nitapiga moyo konde nikayajuwe nitakapofika. Hii ina maana nimeitwa peke yangu?".
"Bila shaka, maana sikupata maelekezo ya mtu mwingine ila wewe tu", Maselina alijibu.
"Asante Maselina, mimi naondoka nikajitayarishe, kama kukwa na jambo lolote zaidi unaweza kunipata nyumbani kwangu kabla ya hiyo saa nne".
"Vizuri Willy, mimi ninakuombea safari njema uende salama Mungu awe nawe upate kurudi salama. Kama mara hii ni safari nyingine ya hatari ninakuomba ukajiangalie vizuri usije kupata madhala ya aina yoyote. Uwe ukikumbuka kuwa kila siku mimi nitakuwa pamoja nawe katika sala zangu, ukiwa na imani hiyo naamini utarudi salama maana Mungu anasema aombaye atapewa na vilevile husema anamsaidia anayejisaidia. Kwa hiyo kwa sababu tunaombea usalama wako ni matumaini yetu kuwa Mungu atakupa usalama kwa sababu wewe kila wakati unajisaidia vilevile Mungu atakusaidia.
"Asante kwa kunipa maneno ya kunipa moyo, ndiyo sababu Maselina sintaweza kukusahau hata kwa siku moja maisha mwangu kwa kufuatana na maneno ambayo huwa ukinipa kila ninapokuwa nikikaribiwa na safari kabambe", Willy alimaliza kinywaji chake akaagana na Maselina ambaye alimsindikiza hadi kwenye gari lake.
"Kwa heri Willy."
"Kwa heri Maselina," waliagana huku Willy akiondosha gari lake na kumpeperushia Maselina busu . Maselina alibaki pale nje ameshikwa na butwa na huku akisikia uchungu moyoni mwake kwa vile Willy alikuwa yumo mbioni kwenda katika safari zake za hatari.
Willy naye alishikwa na wasiwasi kuwa safari hii kwenda Lusaka ingezaa safari nyingine ya hatari.Lakini kwa vile Willy hatari ndiyo ilikuwa shughuli yake kidogo alikuwa akisikia roho ya furaha kujua kuwa alikuwa anakwenda kwenye safari nyingine ambayo ingeweza kuzaa hatari ila tu kilichokuwa kikimtia wasiwasi ni hatari za namna gani atakazo pambana nazo, maana safari hii ilikuwa ya kiajabu ajabu kufuatana na vile Chifu alivyo kuwa ameondoka na sasa alikuwa akimwita yeye Willy afike Lusaka upesi iwezekanavyo.
Willy aliwasili nyumbani kwake na kumkuta Lolita anagalagala tu kitandani bado hajalala.
"Mbona hulali Loly mpenzi?"
"Nitapataje usingizi bila ya wewe kuwa karibu nani? Nilikuwa ninakungoja kwa shauku sana.
Njoo basi unibembeleze nipate usingizi." Willy alikata shauri apate usingizi ingawaje wa muda mfupi kwa hivi alichojoa nguo zake tayari kwa kulala.
"Mgeni wako umempata", aliuliza Lolita huku akuwa amemkumbatia Willy.
"Nimeonana naye, na tumezungumza vya kutosha. Na katika mazungumzo yetu itanibidi asubuhi hii niende safari Lusaka." Lolita alishituka kidogo na kuanza kulalamika.
"Aah Willy usiende kesho, hata hatujafaidi "week-end" hii wewe unapanga safari! Ngoja utaenda jumatatu".
"Haitawezekana Loly, hata mimi ningependa nipumzike nawe "week-end" hii lakini inabidi niwe Lusaka kabla ya saa kumi mchana maana inabidi nionane na mteja wangu mmoja ambaye itambidi aondoke Lusaka Mjini Kuelekea Ulaya, kwa hiyo inanibidi nimuwahi kabla hajaondoka.
Usiwe na wasiwasi mimi nitarudi mara tu baada ya kuonana naye."
"Haya baba mimi siwezi kukulazimisha. Sogea basi unikumbatie vizuri." Willy alizima taa, akajisogeza na kumkumbatia Lolita vizuri.
Ilikuwa yapata saa kumi na mbili asubuhi Willy alipoamka na kuanza kujitayarisha. Lolita naye aliamka huku pombe bado zikiwa kichwani na usingizi ukiwa bado unamuelemea, lakini ilimbidi aamke kusudi aweze kumtengenezea Willy kifungua kinywa.
"Lala tu Loly mpenzi, mimi nitashughulika mwenyewe,"
Willy alimueleza alipomuona macho yake yakiwa mazito yamejaa usingizi.
"Hata ngoja nikutengenezee Chemsha kinywa, kama ni kulala nitalala wakati utakapoondoka.
"Hiari yako mama"
"Asante" alijibu Lolita huku akielekea jikoni. Willy alichukua mkoba wake maalumu wa kwa safari za namna hii na kuanza kuupakia. Alifungua sehemu ya uficho ya mkoba huu ambayo ikifungwa hakuna mtu anaweza kutambua kama kuna nafasi ya kutia vitu katika sehemu hiyo.
Alimchungulia Lolita na kumuona yupo jikoni akijishughulisha na kutengeneza chai. Aliendelea kufunguwa kabati lake, kisha akafunguwa saraka iliyokuwa ndani ya kabati na kutoa bastola tatu, fulana mbili zisizopenyezeka kwa risasi za bunduki, mabunda ya risasi na vitu vingine vingi vya kuweza kumsaidia wakati wa hatari kisha akaiweka ndani ya sehemu ya ufuko wa mkoba wake na kufunga.Baada ya kupakia vitu hivi aliingia kuweka vitu ambavyo mfanya biashara yeyote anategemea kuwa navyo safarini. Wakati akiwa katika pilikapilika hizi simu ililia na akaenda kuisikiliza.
"Hallo nyumbani kwa Gamba hapa,"
"Nani mwenzangu?"
"Wewe unataka kuzungumza na nani?"
"Naomba kuzungumza na ndugu Marko Mabawa"
"Subiri tafadhali," Willy alijibu huku kwa sauti nzito.
"Mimi ni rubani Josiah Banda wa Jeshi la anga la Zambia, Nadhani una habari zangu!"
"Aaa ndugu Banda habari za asubuhi?"
"Ni nzuri tu, je wewe,"
"Mimi salama. Habari zako nimepata na mimi niko katika pilika za kujitayarisha, nitakuwa uwanja wa ndege mnamo saa tatu hivi," alimweleza.
"Fanya mapema kidogo maanna tulikuwa tuondoke saa nne, lakini tumeamriwa sasa tuondoke saa tatu,"
"Sawa basi, "Willy alijibu, mimi nitakuwa hapo uwanjani kati ya saa mbili na saa mbili na nusu."
"Haya vizuri asante, tutaonana wakati huo."
"Asante kwaheri' alijibu Willy na kukata simu. Baada ya simu hii aliendelea na kutayarisha vitu vyake vya safari. Alipokuwa tayari, Lolita naye alikuwa ameandaa meza tayari kwa chemsha kinywa. Wote walikaa na kuanza kustafutahi.
"Nitaenda na gari mpaka uwanja wa ndege na nitamuachia kijana mmoja wa ofisini kwangu ambaye atakuletea. Unaweza kutumia gari mpaka hapo nitakaporudi," Willy alimweleza Lolita huku wakiendelea kula.
"Kama ni hivyo ngoja basi mimi nikusindikize hadi uwanja wa ndege na mimi nitarudi na gari,"
"Hapana, wewe pumzika tu maana hadi sasa bado hujalala."
"Wewe Mbona ndiye kabisa hujalala." Lolita alisema huku akimwangalia kwa macho ya kurembua.
"Mimi nimeisha zoea, usinitilie wasiwasi."
"Kama utakavyopenda Willy"
"Vile vile ningefurahi kama ungekuwa unakuja kuangalia nyumba mara moja moja hadi nitakaporudi."
"Ina maana utakaa sana."
"Hapana, lakini huwezi kujua mambo ya safari hii naweka kama tahadhari tu."
Kidogo walisikia gari linasimama nje. Willy alienda kufunguwa mlango akakuta ni Wilson.
"Karibu ndani," Willy alimkaribisha.
"Asante nimekuletea Pasi yako, mimi nakwenda," alijibu Wilson huku akiwa na wasiwasi kama kawaida yake kila aonanapo na Willy.
"Usiende, maana utanisindikiza hadi uwanja wa ndege. Gari lako acha hapa, utalichukuwa utakaporudisha gari langu." Waliingia ndani lakini Wilson alikataa kukaribia mezani huku akimkodolea macho Lolita ambaye alikuwa amevaa vazi la usiku.
Baada ya kustafutahi Willy na Lolita waliingia chumba cha kulala kwa mazungumzo mafupi.
"Oke Loly mpenzi, mimi ninakwenda tutaonana nitakaporudi."
Bila kumjibu Lolita alimng'ang'ania mabegani kwa kuanza kumpa busu kali sana lililochukuwa kama dakika tatu.
"Haya kwaheri Willy," Lolita aliaga taratibu huku mwili wake ukitetemeka.
"Asante, usiwe na wasiwasi mimi nitarudi upesi itakavyowezekana." Walitoka nje ya chumba.
"Twende zetu Wilson" Willy alisema huku amebeba mkoba wake ambao ulionekana mdogo sana, lakini huku ulikuwa umebeba mambo makubwa. Lolita aliwasindikiza mpaka kwenye gari, na walipoondoka alibaki machozi yakimtoka.
Willy alifika uwanja wa ndege kiasi cha saa mbili na dakika ishirini na kusimamisha gari lake kwenye lango la sehemu ya ndege za Jeshi la Tanzania.
"Wilson asante sana na sasa unaweza kurudi."
"Asante, safiri salama."
Kwenye lango alikuta mwanajeshi aliyekuwa kwenye zamu.
"Mimi ni Marko Mabawa ni abiria wa ndege ya Jeshi la Zambia," alijitambulisha.
"Ahaa wanakusubiri nenda kwenye ndege ile pale," askari alisema huku akionyesha kwa kidole ilipokuwa ndege ya Jeshi la Zambia. Alipofika alikuta Rubani Banda anamsubiri na baada ya kumaliza taratibu zote za safari za hapo kiwanjani waliingia ndani ya ndege tayari kwa kuruka kuelekea Lusaka, Zambia.
ITAENDELEA

Post a Comment

0 Comments