SURA YA KWANZA
LUSAKA
"Tafadhali sikilizeni, huyu ni rubani Mwanakatwe ninafurahi kuwafahamisheni kuwa tunakaribia uwanja wa ndege wa Lusaka ambapo ndipo patakuwa mwisho wa safari yetu, Ni matumaini yangu pamoja na wafanyakazi wenzangu kuwa mmefurahia safari yetu mliyosafiri na Shirika la ndege la Zambia, na tunawakaribisheni tena kusafiri nasi mpatapo safari. Sasa fungeni mikanda yenu tayari kwa kutua, asanteni,"Abiria wote ndani ya ndege hii walifunga mikanda yao tayari kwa kutua. Wale waliokuwa karibu na madirisha waliangalia chini kuiona Lusaka ilivyo kwa juu. Kweli ilitoa picha ya kupendeza sana. Wakati abiria wengine wakijishughulisha na mambo hayo kulikuwa na abiria wanne ambao mara kwa mara walikuwa wanaziangalia saa zao kana kwamba wanachelewa kitu fulani. Mara tu rubani alipotoa taarifa wawili wao waliangaliana. Ingawa abiria hawa walikuwa hawakupandia sehemu moja lakini wawili wao walikuwa wakifahamiana. Wawili walikuwa wamepandia Khartoum Sudan na wawili Dar es Salaam Tanzania. Wawili kati ya watu hawa wanne walikuwa Mawaziri wa Ulinzi kutokana katika nchi hizi mbili na walikuwa wakifahamiana vizuri sana. Ingawaje walikuwa bado hawajapata fursa ya kuzungumza lakini kila mmoja wao alihisi sababu ya kuwepo kwa mwenzake katika safari hii. Watu waliokuwa wameandamana na Mawaziri hawa ni Wakurugenzi wa Upelelezi wa nchi zao.
Abiria hawa ambao walitegemewa kusafiri katika daraja la kwanza, walikuwa wamesafiri katika daraja la kawaida na hakuna abiria wenziwe wala wafanyakazi wa ndani ya ndege waliowatambua kuwa ni akina nani kwani hata hati zao za kusafiria (passport) walizokuwa wakitumia zilikuwa za kawaida tu.
Ndege ilipokuwa imetua abiria walitelemka na kuelekea ofisi za uhamiaji na ushuru wa forodha. Hawa watu wanne walipita sehemu hizi bila matatizo, ingawaje mara kwa mara waliziangalia saa zao kwa wasiwasi kidogo kana kwamba wanazidi kuchelewa kitu. Waliweza kupita kwa urahisi zaidi kwa sababu hawakuwa na mizigo mingi ila mikoba tu ya kawaida.
Walipotokeza nje ya jengo la Uwanja wa ndege walipokelewa na madereva wa teksi waliokuwa tayari kupata abiria wa kupeleka mjini. Hawa watu wanne waliingia ndani ya teksi iliyokuwa karibu na mmoja kati yao akaamru.
"Mjini haraka sana".
"Mpita kuti amadala?" aliuliza dereva teksi katika lugha ya Kinyanja.
"Hatujui kilugha sisi," alijibu mmoja wa watu hawa.
"Nyinyi ni wageni?".
"Ndiyo".
"Nilikuwa na maana mjini niwapeleke sehemu gani?".
"Kwacha House".
Ajabu ni kwamba muda wote huo hawa watu walikuwa hawajasalimiana wala kusemeshana. Kutokana na ukimya na namna ya watu hawa walikuwa na haraka isiyo kifani, kwa hiyo dereva alivuta kasi ili kusudi aweze kuwaridhisha abiria wake. Sharti kama angejuwa ni watu gani aliowabeba asingekubali kwenda mwendo aliokuwa akienda. Maana hawa Mawaziri wawili wa Ulinzi walikuwa ni wanakamati wa kamati ndogo ya usalama ya Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika.
Hii kamati ndogo ya usalama ilikuwa na wanakamati kutoka nchi nane na mara hii wanakamati hawa walikuwa wameitwa kwenye mkutano wa dharura na wa siri mjini Lusaka, ambako Mwenyekiti wa kamati hii ndiko alikuwa anatoka. Habari walizokuwa wamepelekewa wanakamati hawa kwa njia ya simu zilikuwa zimewataka wanakamati hawa wafike Lusaka kwenye kikao hicho cha dharura ambacho kingefanyika Jumamosi saa kumi jioni wakiwa pamoja na Wakurugenzi wa upelelezi wa nchi zao kwa sababu ya tatizo la mawasiliano wanakamati hawa ndio walikuwa wa mwisho kufika mjini Lusaka. Wanakamati kutoka nchi nyingine walikuwa tayari wamewasili.
Wakati dereva wa teksi anaegesha gari, kwenye maegesho ya Kwacha House ilikuwa yapata saa kumi unusu mchana ambayo ilikuwa inamaana walikuwa wameisha chelewa muda wa nusu saa. Mmoja alimlipa dereva na wao nusu wakikimbia walielekea mlango wa mbele wa Kwacha House.
Kwa mara ya kwanza toka wakutane ndipo waziri wa ulinzi wa Tanzania aliwasalimu, "Habari zenu, poleni na safari tumechelewa lakini si sana, Sisi salama, natumaini watakuwa wanatungoja, hata hivyo sisi tumejitahidi sana kufika kama walivyopanga," Alijibu Waziri wa Ulinzi wa Sudan huku wakiwa wamefika meza ya mapokezi ya Kwacha House. Kabla hata hawajazungumza na msichana aliyekuwa amekaa kwenye hiyo meza alitokea kijana mmoja bila hata kuwauliza akawaambia "Wazee twendenui huku," Na wao bila kuuliza walimfuata, "Mmekuwa mnangojewa kwa hamu sana mkutano bado haujaanza," Huyu kijana aliwaeleza huku akipanda ngazi za ghorofa ya kwanza. Walimfuatana wakiwa bado na hiyo hali yao ya wasiwasi maana walikuwa hawajui mkutano huu ulioitwa kiajabu ulikuwa wa nini.
"Chumba hiki ndicho cha mkutano," aliwaeleza yule kijana huku akifungua na wao bila kusita wakaingia ndani. Ndani ya chumba hiki cha mkutano mlikuwa na meza kubwa ya mkutano ambayo tayari watu kumi na wawili walikuwa wamekaa huku wakiizunguka meza. Mtu mmoja ambaye alikuwa anafanya idadi ndani ya hiki chumba cha mkutano kuwa kumi na tatu alikuwa amesimama dirishani akiangalia chini barabarani. Kanakwamba alikuwa akihesabu magari yaliyokuwa yakipita hapo chini. Hata walipokuwa wakiingia hawa wanakamati wengine, bado aliendelea kuangalia, huko chini kanakwamba alikuwa hakusikia kishindo cha kuingia kwao.
Hawa wanakamati walioingia walikaa kwenye nafasi zao na kushiriki katika kilichokuwepo ndani ya chumba hiki, huku kila mtu akionekana kuwa mwenye mawazo mengi sana. Baada ya kupita kama dakika tano hivi, huyu mtu aliyekuwa amesimama kwenye dirisha aligeuka na kuangalia chumbani. Huyu alikuwa ndiye Mwenyekiti wa kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika. Alienda mpaka kwenye meza akavuta kiti akakaa, kisha akavunja kimya kilichokuwamo chumbani kwa kusema, "Ndugu Wanakamati, inabidi nitoe shukrani zangu kwenu nyote kwa kuweza kuitikia mwito wa kuhudhuria hiki kakao cha dharura cha kamati ya usalama ambacho kimeitishwa kinamna yake. Nilikuwa na wasiwasi mwingi kuwa huenda wanakamati wengine wangeshindwa kufika kwa muda uliopangwa. Hii inazidi kutudhihirishia kuwa Afrika ni moja na umoja wa Afrika unazidi kukomaa siku hadi siku" Alinyamaza kido kiasi cha kupitisha mate, halafu akaendelea "Vile vile ningependa kuwakaribisha Wakurugenzi wa Upelelezi ambao kwa kawaida si wanakamati wa kamati hii, kuwa mtakuwa na haki ya kupiga kura kama wanakamati wa kawaida. Nafikiri tumeelewana mpaka hapo."
"Tumeelewa," walijibu wanakamati kwa pamoja. Kila mtu alionyesha sura ya uchu wa kutaka kujua hasa ajenda ya mkutano huu. Huku akiwa amekunja uso aliendelea. "Ndugu wanakamati, nasikitika kuwaeleza kuwa hiki kikao chetu si cha kawaida na ndiyo sababu kimeitishwa kwa siri kwa maana haikutakiwa ijulikane kuwa kikao hiki kimeitishwa kutokana na jambo lenyewe ambalo limefanya kikao hiki kiwepo kutokana na jamno lenyewe ambalo limefanya kikao hiki kiwepo. Ni jinsi hii mhitasari wa maneno yatakayoamjadiliwa na kuamriwa katika mkutano huu hautachukuliwa.
Hii ina maana itabidi sisi wote tusikilize kwa makini na yote tutakayoyasikia tuyaweke moyoni mwetu, yawe siri yetu," Chumba cha mkutano kilikuwa kimya kabisa isipokuwa sauti ya Mwenyekiti peke yake. Alipokuwa amefikia hapa sura ya kila mtu ilionyesha mshangao wa jinsi mkutano ulivyokuwa ukiendeshwa huku wengine mioyo yao ikipiga haraka haraka kwa shauku ya kutaka kujua jambo lenyewe.
"Ndugu wanakamati." Mwenyekiti aliendelea kwa sauti ya huzuni. "Naamini mmesikia tukio lililotokea mjini Kinshasa Zaire juzi usiku na kutangazwa jana," aliwaangalia huku baadhi yao wakitingisha vichwa kuonyesha kuwa walikuwa na habari kisha akaendelea, "Tumepata habari kuwa aliyekuwa rais wa shirikisho la vyama vya wapigania uhuru Kusini mwa Afrika ndugu Edward Mongo ameuawa huko mjini Kinshasa Zaire baada ya gari alilokuwa akitembelea kutegwa bomu ndani ya mtambo wake na kuripuka. Yeye alikuwa ametokea Libreville Gabon ambako alikuwa akihudhuria mkutano wa umoja wa Matafa kuhusu kuzuia Ufaransa kuiuzia Afrika Kusini dhana za kivita na kuisaidia kutengeneza silaha za Nyuklia. Na alikuwa amepita mjini Kinshasa kwa mazungumzo na serikali ya Zaire kuhusu hali iliyoko Kusini mwa Afrika, Na kabla ya kufanya mazungumzo hayo, ndugu Mongo alikufa juzi usiku kwa mripuko wa bomu lililotegwa ndani ya injini ya gari aliyokuwa amepewa kutembelea. Jambo hili limesikitisha wakuu wa nchi huru za Afrika, kwa maana kifo cha ndugu Mongo kina maana ya pigo kubwa kwa ushirikiano wa vyama vya wapigania uhuru Kusini mwa Afrika! Hii inaonyesha waziwazi kuwa ni njama za makaburu na vibaraka wao kutaka kuvunja harakati za ukombozi zinazofanywa na wapigania uhuru Kusini mwa Afrika. Ni dhahiri kuwa kumuua ndugu Mongo wamejipalia mkaa, lakini kitendo kama hiki hatuwezi kukiruhusu kiendelee.
Kwa jinsi hii ndugu wanakamati, kikao hiki cha dharura kimeitishwa kusudi kitafute dawa ya kukomesha vitendo kama hivi na vile vile kutafuta jinsi gani tunaweza kuwapa fundisho hawa wanaohusika na kitendo kama hiki kuwa sasa Afrika iko macho na haitaki kuchezewa. Hili ndilo jukumu tumepewa na wakuu wa nchi huru za Afrika na hatuna budi kulitekeleza," alimaliza huku akiwatazama wajumbe kikamilifu.
"Ndugu Mwenyekiti, bado haijaeleweka sawasawa hasa kuhusu inatakiwa tufanye nini?. Kwa kweli jambo hili ni la kusikitisha sana na hata wakati natoka nyumbani niliacha baraza la mawaziri limekutana kuzungumzia tukio hili. Kwa hivi jambo tutakalozunguzia au kuamua hapa lina maana kuwa ndiyo utakuwa msimamo wa nchi huru za Afrika. Kwa jinsi hii, ndugu Mwenyekiti, tunaomba utueleze suala hili kinaganaga kusudi tuweze kulielewa sawasawa na pindi tutakapotoa maamzi yalingane na matakwa ya nchi huru za Afrika", alitoa rai mjumbe kutoka Kenya.
Wajumbe wengine walitingisha vichwa, kuonyesha kuwa na wao walihitaji ufafanuzi zaidi. Akijibu hoja hiyo, Mwenyekiti alisema, "Ndugu wanakamati, nadhani itabidi nifafanue jambo hili kwa kutoa historia fupi juu ya matukio ya namna hii na nini kimefanyika katika jitihada za kuyazuia.
"Miaka mitatu iliyopita kumetokea matukio ya mauaji kwa viongozi wa wapigania uhuru na tukio hili la juzi linakuwa la sita kwa muda wa miaka mitatu. Tukio la kwanza ambalo lilitokea mwaka juzi lilitokea mjini Dar es Salaam ambapo Mkuu wa ofisi wa Wapigania Uhuru iliyoko mjini hapo ndugu Leon Fadaka aliuawa kwa bomu baada ya kupokea kifurushi kilichokuwa kimetumwa kwake kwa njia ya posta na wakati alipokuwa akikifungua kililipuka kwani ndani yake kuliwa na bomu na alikufa pale pale. Uchunguzi ulifanyika ikabainika kuwa kifurushi hili kilikuwa kimetumwa kwake kwa njia ya posta kutoka mjini Kinshasa. Serikali ya Zaire ilijaribu kuchunguza jambo hili lakini bila ya mafanikio. Mwaka huo huo wa juzi baada ya miezi sita tangu kuuawa kwa ndugu Fadaka, kulitokea tukio lingine la namna hiyo hiyo hapa mjini Lusaka, baada ya Mkuu wa ofisi ya wapigania Uhuru ya hapa naye kupata barua kutoka mjini Paris Ufaransa na mara alipokuwa akifungua bahasha, kukatokea mripuko ambao ulimuua papo hapo.
Tukio hili lililaaniwa vikali kote Ulimwenguni lakini hakuna mtu wala kikundi cha watu kilichokamatwa bali lawama ziliwaangukia makaburu na vibaraka wao kuwa ndiyo tu wangeweza kuhusika na vitendo hivi. Matukio mengine matatu yametokea mwaka jana. Tukio la kwanza mwaka jana lilitokea mjini Lagos Nigeria, wakati ndugu Nelson Chikwanda ambaye alikuwa mwakilishi wa wapigania uhuru katika ofisi njema za Umoja wa nchi huru za Afrika iliyoko mjini hapo alipigwa risasi na mtu asiyejulikana. Uchunguzi mkali ulifanyika lakini hakuna lolote lililotambulika.
Miezi mitatu baada ya tukio hili huko Lagos, ofisi ya wapigania uhuru iliyoko mjini Nairobi ililipuliwa na wafanyakazi watatu akiwemo ndugu Nene ofisa wa juu katika ofisi hiyo aliuawa. Tukio la mwisho mwaka jana lilitokea tena mjini Kinshasa wakati Afisa wa juu katika Jeshi la wapigania uhuru Meja Komba Matengo alipokutwa ameawa ndani ya Hoteli Tiptop chumbani mwake. Yeye alikuwa amewasili mjini hapo kuhudhuria kikao cha kamati ya ukombozi ya nchi huru za Afrika kilichokuwa kikizunguzia kuunganishwa majeshi ya wapigania uhuru Kusini mwa Afrika. Na ndugu wanakamati tukio la mwisho kufikia sasa ni hili ambalo limetokea juzi. Naamini nyote mnakumbuka hatua ambazo zimechukuliwa kujaribu kuhakikisha usalama wa ndugu hawa wapigania uhuru. Mpaka sasa tumefaulu kutegua mabomu kadhaa yaliyokuwa yametumwa kwa wapigania uhuru kadhaa kwa njia ya barua ama vifurushi jambo hili tumeweza kufuzu kwa sababu barua zote au vifurushi vinavyotumwa kwa watu hawa vinafunguliwa kwanza na wataalam kutoka idara ya usalama ya kila nchi ambapo ofisi hizi zilizopo. Lakini jinsi ya kuzuia matukio mengine kama lilile lililotokea Lagos, Kinshasa, TipTop Hoteli na hili la juzi inakuwa vigumu sana kuyazuia.
Hata hivyo, hatuna budi kujihami, kwani hatuwezi kukaa tu huku ndugu zetu wakiuawa huku na kule ili kusudi harakati za ukombozi wa Kusini mwa Afrika ziweze kusimama. Kwa hivi, ndugu wanakamati, tuko hapa ili tujadiliane ni njia gani tuzitumie katika kujihami. nafikiri nimeeleweka vya kutosha," alimalizia Mwenyekiti.
Mkutano ulishikwa na ukimya wa kama dakika tano hivi huku kila mjumbe akizingatia mambo yote yaliyokuwa yameelezwa. Mjumbe wa Zambia ambaye kwa kawaida huwa ndiye Mwenyekiti wa kamati hii ndiye alikuwa wa kwanza kuvunja kimya hiki kwa kusema, "Ndugu Mwenyekiti na ndugu wanakamati wenzangu, kusema ukweli jukumu hili tulilopewa ni jukumu gumu sana. Ni gumu kwa sababu inabidi kikao hiki kiamue nini kitu gani kitendeke dhidi ya mauaji haya ambayo yanatokea kwa ndugu zetu wapigania uhuru. Ingawaje suala hili ni gumu lakini hatuna budi kulitatua maana tumeaminiwa na viongozi wa nchi zetu na ni matumaini yangu lolote tutakaloliamua hapa ndiyo utakuwa uamzi wa Afrika. Ndugu wanakamati, matukio haya kama yalivyoelezwa na ndugu Mwenyekiti, Utaona ya kwanza yanatokea katika nchi zetu zilizo huru. Ingekuwa habari nyingine kama matukio haya yangetokea kwenye uwanja wa mapambano kwani jambo kama hili lingeweza kueleweka. Lakini utaona kuwa tunapigwa vita nyumbani kwetu. Hii ina maana tumeshindwa kuwalinda hawa ndugu zetu? Suala sasa ni tufanye nini? Kwa upande wangu naonelea ya kwamba inabidi tutafute kiini cha matukio haya, kwani tukishapata kiini chake itakuwa rahisi kupata ufumbuzi. Mpaka sasa hivi tumefahamishwa kuwa matukio mawili yametokea mjini Kinshasa, moja Dar es Salaam, moja hapa Lusaka, moja Nairobi na moja Lagos. Tukio la mjini Dar es Salaam linasemekana limetokana na kifurushi kilichokuwa kimetumwa kwa njia ya posta kutoka mjini Kinshasa, Zaire. Uchunguzi huu unatuonyesha wazi wazi kuwa tukio la Dar es Salaam kilikuwa mjini Kinshasa, kwa hiyo hii inatupa idadi ya matukio matatu kati ya sita yakiwa yametokea mjini Kinshasa Zaire. Ndugu wanakamati, kutokana na hali hii, inaonekana waziwazi kuwa mjini Kinshasa kuna mambo na kama uchunguzi halisi ukifanywa mjini hapo huenda tukapata kiini hasa cha mauaji haya. Kwa hivi ni rai yangu kuwa utumwe ujumbe kutoka kwenye kamati hii ukaonane na wakuu wa serikali ya Zaire, uzungumzie juu ya jambo hili, ukiwa unaomba serikali ya Zaire ifanye upelelezi kabambe juu ya matukio hayo. Ni imani yangu kuwa kwa kufanya hivi tutapata ufumbuzi wa jambo hili. Sijui wanakamati wenzangu mnasemaje," alimaliza.
Mjumbe wa Sudan aliinua kichwa na kwamwangalia Mwenyekiti akionyesha sura ya kutaka kusema kitu. Mwenyekiti ambaye naye alikuwa akimwangalia alimtingishia kichwa kumuashiria aendelee. Hivyo alianza kwa kusema, "Ndugu Mwenyekiti na ndugu wajumbe, kusema kweli mzigo tuliopewa ni mzigo mzito lakini kama walivyokwisha sema walionitangulia hatuna budi kuubeba. Ningependa kuunga mkono maelezo ya ndugu mjumbe aliyemaliza kusema kabla yangu, maelezo ambayo nisingependa kuyarudia kwani naamini yameeleweka vizuri sana. Kweli mtu yeyote anaweza kuona mjini Kinshasa kuna matatizo na ingefaa zaidi uchunguzi ufanyike mjini hapo juu ya matukio haya. Ingawa makubaliano ya suala hili inabidi uchunguxi ufanyike lakini namna alivyotoa maoni ndugu mjumbe mimi nina maoni tofauti na yeye jinsi ambavyo uchunguzi huu ungefaa ufanyike. Ndugu wajumbe ni matumaini yangu kuwa mtakubaliana na mimi kila tukio la namna hii linalotokea katika nchi yoyote lazima upelelezi wa hali ya juu ufanyike kusudi yeyote anayehusika aweze kukamatwa na kutiwa hatiani. Hivi ndivyo nchi zote zilizopatwa na baraa la aina hii zimejitahidi kufanya, ingawaje bila mafanikio maalumu. Mwisho wa kila upelelezi umekuwa ni lawama tu kwa Afrika Kusini na vibaraka wake. Kwa jinsi hii ndugu wajumbe kutuma ujumbe ukazungumze na serikali ya Zaire ili kuongeza jitihada katika upelelezi wake kuhusu matukio haya, itakuwa sawa na kuiomba kufanya kitu ambacho imekwisha kifanya, kwani mimi naamini kwa dhati kuwa Zaire imekuwa ikifanya kila iwezavyo kusudi iweze kuwakamata hawa wauaji, ingawaje bila mafanikio. Kwa hivi naonelea kuwa Zaire inahitaji msaada katika upelelezi wake msaada ambao unabidi utoke nje ili kuimarisha nguvu za wapelelezi wa nchi hiyo.
Kwa hiyo nato oni kuwa kiundwe kikosi cha wapepezi kitakachotoka katika Nchi Huru za Kiafrika ambacho kitaenda Zaire kikasaidiane na wapelelezi wa Zaire ni bahati nzuri kuona kuwa katika mkutano huu, wakurugenzi wa upelelezi wa nchi huru nane za Kiafrika wako hapa na wanaweza kutusaidia kitaalam jinsi ya kuunda kikosi hiki," alimaliza huku akipigiwa makofi ya kumpongeza kwa maoni yake, vile vile ikionyesha wajumbe wengi waliafiki maoni yake. Kwa mara ya kwanza minong'ono ilisikika katika chumba hiki, Mwenyekiti aliikatisha minong'ono hii kwa kusema.
"Ndugu wajumbe mnanipa moyo kwa kuona kuwa jambo ambalo limekuwa nikilifikiria siku nyingi na kunisumbua rohoni siku nyingi leo limeweza kusemwa na nyinyi kabla hata mimi mwenyewe sijalisema. Nilikuwa nachelea kulisema awali nikiwa na mawazo kuwa huenda lingeweza kupingwa, lakini ni furaha iliyoje kuona jambo hili limeshangiliwa na wajumbe wote, ni kweli kabisa ya kuwa wakurugenzi wa upelelezi mmeitwa katika mkutano huu ili muweze kutusaidia kitaalam ni jinsi gani tunaweza kuunda "Kikosi cha Kisasi" kikosi kidogo na chenye kufaa. Kabla sijasema mengi naonelea niwaachie uwanja wataalam waweze kutushauri kabla hatujafikia uamzi kamili,"
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Nigeria ndiye alikuwa wa kwanza kusema, "Asante sana ndugu Mwenyekiti na ndugu wajumbe. Kikao hiki mimi ni mara yangu ya kwanza kuhudhuria na, nakihudhuria wakati hasa ambapo nahitajika kukihudhuria kikamilifu katika matatizo yanayoikabili Afrika kwa wakati huu. Ni wazo zuri sana kuunda "Kikosi cha Kisasi" ambacho kitasaidia katika kutafuta na kukipiga vita kikosi kingine cha maadui wa Afrika. Mawazo yaliyokwisha tolewa kuwa baada ya kikosi hiki kuundwa kiende Kinshasa kikasaidiane na idara ya usalama ni jambo la busara. Lakini kwa upande wangu kutokana na ujuzi wangu katika mambo ya upelelezi, mimi naonelea kuwa baada ya kuunda kikosi hiki si vizuri kikasaidiane na idara ya usalama ya Zaire bali kiende huko kikijitegemea na wala kisijulikane kabisa na mtu yeyote nchini Zaire kama kuna kikosi kama hiki. Nikisema hivi sina maana kuwa siiamini sserikali ya Zaire, bali ni kufuatana na hali yenyewe ya kazi ya kipelelezi ilivyo. Jinsi watu wachache Afrika watakavyoweza kufahamu kuwepo kwa kikosi hicho ndivyo kitakavyokuwa na nafasi nzuri ya kuweza kufanikiwa. Kwa maana inabidi ieleweke wazi kuwa adui tunayepigana nae ana nguvu na ujuzi wa hali ya juu na ndiyo sababu watu maarufu sita wameweza kuuawa bila kushika au kuawa mtu hata mmoja kwa upande wa wauaji. Kutokana na tukio lililotokea mjini Lagos nimejifunza mengi kwani upelelezi wa tukio lote ulifanyika chini yangu. Kwa hivyo nathubutu kusema kuwa hili ni kundi la wauaji wa hali ya juu sana na wana mipango ya hali ya juu sana. Kiupelelezi hata mimi nahisi mjini Kinshasa kuna mizizi ya matukio haya. Kwa kifupi basi ni maoni yangu kuwa kwanza lazima tuunde kikosi cha wapelelezi wa hali ya juu sana katika Afrika, pili kikosi hiki kiwe na watu wachache sana, tatu kitakapokwenda Zaire kiingie kisirisiri na kifanye kazi zake kwa siri kama kikundi cha maadui kinavyofanya kazi kisiri, na serikali ya Zaire isijulishwe kabisa juu ya kikosi hiki kwa sasa huenda mpaka hapo baadaye itakapokuwa lazima (Zaire haikuwa mojawapo katika nchi nane za kamati ya usalama) na mwisho lazima kikosi hiki kiundwe haraka iwezekanavyo na kiwe kimefika Zaire wakati bado kuna moto wa kifo cha ndugu Mongo,' alimalizia.
Wakurugenzi wengine wote wa usalama kutoka katika nchini nyingine walikubaliana na maoni hayo yote ya mwenzao. Lililokuwa limebaki sasa juu ya kikao kuzungumzia uundwaji wa kikosi chenyewe. "Ndugu wanakamati, inaonekana tumepiga hatua za haraka sana katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili," alisema Mwenyekiti. "Lilopo sasa ni kuzingatia maoni yaliyotolewa na kuyashughulikia kikamilifu kufuatana na vile mkutano utakavyokubaliana na maoni hayo. Kwa sababu tumekubaliana kuwa lazima kikosi kiwe tayari wakati bado kuna moto wa kifo cha ndugu Mongo huko Zaire, hii ina maana hatuna nafasi ya kuchagua watu ili tukawafundishe waje waunde kikosi hiki, bali inatubidi tupate watu ambao tayari yamekwisha pata ujuzi wa juu katika upelelezi, kutoka katika nchi mojawapo za Kiafrika na kuunda kikosi hiki kutokana nao. Suala sasa ni kwamba je, tunao watu kama hawa Afrika. Ikiwa suala hili litajibiwa sina shaka tatizo letu litakuwa limekwisha," alimaliza Mwenyekiti huku akiwaangalia wanakamati mmoja baada ya mwingine.
Mkutano kwa mara nyingine uliingiwa na minong'ono kati ya kila Waziri na Mkurugenzi wake wa Upelelezi mingong'ono hii iliendelea karibu nusu saa, ubishi ukizuka hapa na pale kati ya Waziri na Mkurugenzi wake. Kisha mjumbe wa Tanzania aliinua kichwa na kutoa kohozi la kujitayarisha kusema. Wengine waliposikia ishara hii walinyamaza na kumwangalia wakingojea kusikia atasema nini, naye alianza, "Ndugu wajumbe, sina budi kutoa shukrani zangu kwenu nyinyi kwa kuwa tayari kunisikiliza. Vilevile ningependa kutoa furaha yangu jinsi mkutano huu unavyoendeshwa na jinsi ambavyo wajumbe waliowahi kusema, wameweza kusema kwa moyo wa Afrika moja na wala si kwa nchi binafsi kwa sababu hii hata mimi nasikia mori na ninathubutu kuwaeleza kuwa serikali ya Tanzania inaye mtu ambaye akipata msaada wa mtu mmoja au wawili pamoja na baraka za Afrika Huru anaweza kuitekeleza kazi hii kwa kiasi kikubwa sana. Mtu huyu amewahi kufanya shughuli za namna hii kubwa kubwa, na kama ndugu wajumbe mnakumbuka juu ya karatasi za wapigania uhuru zilizoibiwa jijini Dar es Salaam na kuweza kukamatwa mjini Nairobi mtu aliyewezesha jambo hili lifanikiwe ndiye ninayemwelezea. Ujuzi wake ni wa hali ya juu sana na ni imani yangu kuwa anaeleweka vizuri kwa wakurugenzi wa upelelezi, hasa kwa jina.
"Ndiyo tunamfahamu sana, hata sisi tulikuwa tunamzungumzia huyo huyo," alidakia Mkurugenzi wa Upelelezi wa Kenya.
"Sina shaka ni Willy Gamba," alitamka Mkurugenzi wa Upelelezi wa Ghana.
"Ndiye hasa nilikuwa namzungumzia," alijibu mjumbe wa Tanzania.
Mkutano ulinza kumzungumzia huyu mtu aitwaye Willy Gamba, sifa zake zote zilielezwa mbele ya mkutano na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Tanzania na mkutano kwa ujumla ulikubaliana kuwa mtu huyu angefaa apewe jukumu hili.
"Nafikiri ndugu wanakamati tumefikia uamzi juu ya suala hili kwa sasa mimi naonelea jambo hili tunawaachia Wakurugenzi wa Upelelezi wakae na walishughulikie. Huyu mtu Willy Gamba tumeamua ndiye ataongoza "Kikosi Cha Kisasi" na mambo mengine yote yatatengenezwa na hawa wakurugenzi ambao ni wataalam, itabidi tuonane tena kesho saa kumi na mbili jioni hapa hapa. Hii itawapa nafasi nyinyi wataalam kutayarisha mambo yote na kuhakikisha kuwa tuonanapo kesho Willy Gamba nae awe amefika hapa. Kwa sasa hivi tufunge mkutano, nyinyi mtapanga muda wenu wa kukutana, nafasi zenu za kulala zimetayarishwa, kila mtu aondokapo hapa apite mapokezi kuna dereva na ofisa usalama kwa kila mwanakamati. Ni matumaini yangu kuwa tuonanapo kesho jioni mambo yatakuwa yameshughulikiwa kikamilifu. Itakuwa tu kupokea taarifa kamili na mambo ya kuanza. Asante sana."
Mwenyekiti alifunga mkutano na kuangalia saa yake ambayo ilionyesha ni saa mbili unusu za usiku wa siku hii ya Jumamosi.
ITAENDELEA 0784296253
Credits : Iddy Eba
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena