Nyanya |
Kitunguu Saumu |
Brokolini |
Beri |
Hali i mbaya zaidi katika nchi zilizoendelea ambako tunataarifiwa ya kwamba kuna idadi kubwa sana ya watu wanaopoteza maisha yao kila siku kutokana na magonjwa ya kansa ambayo kimsingi yanasababishwa na na ulaji wa vyakula tunavyokula kila siku. Mfano nchini Marekani pekee karibu theluthi moja ya wagonjwa wa kansa inasababishwa na vyakula wanavyokula kila siku, na hii ni kwa mujibu wa Taasisi ya Saratani ya nchini Marekani.
Pamoja na kuwepo habari hiyo mbaya na ya kusikitisha ya kupoteza mamia ya ndugu zetu kila siku, kuna habari njema pia kuwa unaweza kabisa kujikinga na ugonjwa huu hatari kwa kula vyakula vinavyostahili na kuepuka vinavyochangia saratani.
Kwa leo hebu tuangalie orodha ya baadhi ya vyakula ambavyo vinaaminika kuwa na uwezo mkubwa wa kupambana na seli zinazosababisha saratani mwilini. Mwenyekiti wa Taasisi ya Kuzuia na Kutibu Saratani, DK. Richard Béliveau wa Chuo Kikuu cha Québec, Montreal Canada, anasema kuwa tafiti zote zinaonesha kuwa kinga ya saratani iko kwenye ulaji wa vyakula vitokanavyo na mimea (Plant-based foods).
Unachotakiwa kufanya ili kuupa mwili wako kinga dhidi ya saratani, kula matunda na mboga za majani za aina mbalimbali kila siku, hasa hizi zifuatazo:
BROKOLI (BROCCOLI)Hii ni ana fulani ya mboga ya majani, iko kama maua ya maboga au uyoga, inapatikana katika masoko mengi makubwa nchini. Aina hii ya mboga inaelezwa kuwa na kiasi kingi cha kirutubisho aina ya ‘sulforaphane’ ambacho uwezo wake wa kutoa kinga ni mkubwa. Inatoa kinga dhidi ya saratani ya matiti, ini, mapafu, kibofu, ngozi, tumbo na kizazi.
BERI (BERRIES)Haya ni matunda maarufu ambayo hujulikana pia kama matunda ya kuongeza damu au ‘matunda damu’ kutokana na kuwa na rangi nyekundu na mengine meusi na kijani. Ulaji wa matunda haya hutoa kinga dhidi ya saratani ya utumbo, koo, mdomo na ngozi.
NYANYA (TOMATOES)Wengi tunaidharau nyanya na kuipuuzia kwa kutoila katika milo yetu ya kila siku, wakati nyanya ziko nyingi kiasi zingine zinaoza mitaani. Nyanya inaelezwa kuwa na kirutubisho aina ya ‘Lycopene’ ambacho kina uwezo mkubwa wa kuzuia saratani ya kizazi ambayo nchini Marekani inaua zaidi ya watu 8,000 kila mwaka, kwa Tanzania hali ni mbaya zaidi. Nyanya huzuia pia saratani ya mapafu, tumbo na kibofu.
KITUNGUU SAUMU (GARLIC)Faida za kitunguu saumu zipo nyingi, lakini miongoni mwa hizo faida ni kutoa kinga dhidi ya ugonjwa wa saratani. Kwa kuweka mazoea ya kula mara kwa mara, kwa kuchanganya katika mlo wako au saladi yako utakuwa umejijengea kinga mwilini. Hutoa kinga dhidi ya saratani ya utumbo, matita, koo na tumbo kwa ujumla.
MAHARAGE (BEANS)Wengi wetu hatupendi kula maharage tukiamini ni mboga ya kimaskini! Ukweli ni kwamba maharage ni mboga muhimu na ina faida nyingi mwilini, ikiwemo kutoa kinga dhidi ya saratani ya utumbo na matiti. Utafiti kuhusu faida za maharage uliofanywa na Chuo Kikuu cha Michigan nchini Marekani umethibitisha faida hizo.
Kwa ujumla, magonjwa ya saratani yanaweza kuepukwa iwapo mtu atazingatia ulaji wa mboga na matunda asilia kila siku na kujiepusha na ulaji wa vyakula vya ‘kutengeneza’. Wiki ijayo nitakuletea orodha ya vyakula vinavyosababisha saratani ambavyo unatakiwa kuviepuka kama ukoma!
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena