Header Ads Widget

Responsive Advertisement

AFYA YAKO |KAMA ULIKUWA UNAMPANGO WA KUNYWA POMBE WEEKEND HII NI VYEMA UKASOMA KWANZA MADHARA HAYA


Pombe ni kinywaji ambacho hutumika kama kiburudisho kwa baadhi ya watu hapa duniani, lakini wengine hutumia kinywaji hicho kwa lengo la kupunguza mawazo, huku wengine wakidai kwamba kinywaji hicho huwasaidia kuondoa aibu.

Mbali na kuwa pombe imeonekana kuwa na wapenzi wengi, lakini utumiaji wa bidhaa hii kupita kiasi umekuwa ukileta madhara mbalimbali kwa watumiaji wa kinywaji hicho kila iitwapo leo.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuwa watu milioni 3.3 hufariki dunia kila mwaka kutokana na matumizi ya pombe kupita kiasi, ambayo wanasema ni sawa na asilimia 5.9 ya vifo vyote.

Aidha, huko nchini Scotland, Shirika la NHS mnamo mwaka 2003 lilitoa makisio ya kwamba, kifo cha kila mtu mmoja kati ya vifo vya watu 20 vilitokana na pombe. Utafiti uliofanyika mwaka 2009 , ambao pia uligundua ya kuwa watu 9,000 walikufa kutokana na magonjwa yaliyohusishwa na matumizi ya pombe.

Hali kadhalika nako nchini Marekani kupitia Kituo cha Udhibiti Uzuiaji wa Magonjwa wao waliripoti kuwa, kutoka mwaka 2001 hadi kufikia mwaka 2005 kulikuwa na takribani vifo watu 79,000 vilivyotokana na matumizi ya pombe kupita kiasi.

Mtaalam wa tiba asili Dk Abdallah Mandai anasema kuwa, kiafya matumizi ya pombe huleta madhara mbalimbali ndani ya mwili wa binadam, kwa mfano ini huathirika vibaya kutokana na matumizi ya pombe kupindukia, lakini pia tumbo nalo huathirika kutokana na kuchubuka kwa ngozi laini ya tumbo la chakula na kusababisha vidonda vya tumbo.

Mbali na madhara hayo, pia ubongo nao huathirika, kutokana na baadhi ya chembe chembe za ubongo yaani ‘brain cells’ kuharibika na kusababisha tatizo la kupoteza kumbukumbu.

Dk Mandai anaeleza kuwa, pia pombe huleta madhara katika moyo na mapafu ya binadamu, lakini pia kwa upande wa wanawake wajawazito pombe huwasababishia kuharibika kwa mimba na hata kupelekea kujifungua mtoto mwenye mtindio wa ubongo.

Aidha, inaelezwa kwamba asilimia 90 ya watu wenye saratani ya tumbo ni watumiaji wa pombe kupita kiasi, huku ikielezwa kuwa pombe husababisha ongezeko la mafuta ndani ya damu na wakati mwingine husababisha unene uliokithiri pia.

Dk Mandai anasema pombe imekuwa na madhara mengi yakiwemo yale ya moja kwa moja na yanayokuja taratibu ambapo mtaalam huyo anaeleza kuwa pombe husababisha mtu kutetemeka, kuzubaa zubaa na hata kupauka kwa mwili ndio maana hata katika vitabu vya baadhi ya dini kama vile dini ya Kiiislamu, pombe imeharamishwa kwa kuzingatia madhara yake kwa binadamu.

Mtaalam huyo anaeleza kwamba, pombe pia huleta madhara kama vile upungufu wa nguvu za kiume, kukosa hamu ya tendo la ndoa (loss of libido), saratani ya figo na kufanya figo kushindwa kufanya kazi yaani (renal failure).

Hali kadhalika pombe pia husababisha matatizo ya ganzi miguuni na mikononi ambayo kitaalam hujulikana kama ‘peripheral neuropathy,’ lakini pia pombe huleta utapiamlo hasa kwa wale wanaokunywa sana huku lishe yao ikuwa duni.

Licha ya madhara hayo pia pombe husababisha saratani ya ini, kusinyaa kwa ini na hata saratani ya tumbo sambamba kabisa na vidonda vya tumbo.

Hata hivyo, Dk Mandai anasema, mbali na madhara ya kiafya, pia pombe huleta mifarakano ndani ya jamii na hata kuvuruga na kuondoa amani ndani ya familia.
Pombe huathiri uchumi wa mtu kwani pombe ikishakuwa sugu ndani ya mwili wa binadamu (chronic), watu wengi huishia kumaliza vipato vyao kwa ajili ya kununua kinywaji hicho.

Dk Mandai anasema pamoja na kuwepo kwa tahadhali katika matangazo ya pombe lakini bado kinywaji hicho kimekuwa na wanywaji wengi, hivyo anasema ni vizuri ukahakikisha unaepuka matumizi ya pombe kupindukia kwa ajili ya kulinda afya yako

Post a Comment

0 Comments