Header Ads Widget

Responsive Advertisement

Makala | Ziara ya Rais wa China nchini Marekani, muendelezo wa unyonyaji wa pamoja kwa Mataifa madogo?

Obama wakiwa kwenye maongezi wakati wa mapumziko baada ya mkutano
RAIS Xi Jinping wa China anatarajiwa kufanya ziara nchini Marekani mwishoni mwa mwezi huu, ambayo itakuwa ziara yake ya kwanza ya kiofisi kwenye taifa hilo tangu awe Rais.
Ziara hii inavutia ufuatiliaji kwanza ni kutokana na kuwa China na Marekani ni nchi mbili zenye nguvu kubwa zaidi ya kiuchumi duniani. Ziara za viongozi wa nchi hizo katika nchi hizo si jambo jipya, hata Rais Xi na mwenyeji wake Barack Obama hii itakuwa ni mara ya tatu kukutana katika miaka miwili iliyopita. 
Kwa mujibu wa Nadharia ya Mtego wa Thucydides (Thucydides trap), nchi inayoibuka kuleta changamoto kwa ukiritimba wa nchi kubwa iliyopo, kunakuwa na hatari ya kutokea vita. Lakini kutokana na chaguo la vita kuendelea kuwa la hatari na kusababisha hasara, katika zama hizi mtego wa Thucydides unategulika.
China na Marekani zimetegua mtego huu kwa kukubaliana kujenga 'aina mpya ya uhusiano kati ya nchi kubwa', ambao msingi wake ni kuheshimiana na kunufaika kwa pamoja. Ziara ya rais Xi nchini Marekani inatarajiwa kuendeleza mwelekeo huu.
Tukiangalia picha ya jumla ya ziara ya Rais Xi Jinping nchini Marekani na umuhimu wake kwa uchumi wa China, tunaweza kuona kuwa ziara hiyo kwa namna moja inahusu dunia nzima. Kupungua kwa kasi ya ongezeko la uchumi wa China ambayo kwa sasa ni injini muhimu kwa ongezeko la uchumi wa dunia, pamoja na kutetereka kwa soko la fedha la China, kumegusa moja kwa moja uchumi wa dunia. 
Kitakachojadiliwa kati ya China na Marekani kuhusu ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi zao, matokeo yake sio tu yatakuwa mazuri kwa China na Marekani, bila shaka yatakuwa mazuri kwa nchi nyingine zinazohusiana na China.
Nafasi ya nchi nyingine kwenye uhusiano kati ya China na Marekani
Kwa kawaida wapambanapo mafahali wawili ziumiazo ni nyika. Kiuchumi China na Marekani ni mafahali, ambao kama wakipambana nchi nyingine ndogo ndogo kama yetu ndio zinaumia.
Mwaka 2013 marais wa China na Marekani walifanya ziara zinazofuatana nchini Tanzania, baadhi ya watu walitaja ziara hizo kuwa ni ishara ya nchi hizo mbili kugombea fursa barani Afrika. Lakini tukiangalia nyuma zaidi mwaka 2006, tutagundua kuwa mkutano wa viongozi wa China na Africa wa baraza la ushirikiano kati ya China na Africa (FOCAC) ulitoa mwelekeo mpya duniani wa ushirikiano na Afrika.
Barack Obama, Xi Jinping
Obama na Xi walipokutana kwa mara ya kwanza California
Baada ya mkutano huo, mikutano ya aina hiyo kati ya Afrika na India, Japan, Umoja wa Ulaya, na Marekani ilifanyika kwa mfululizo. Tunajua kuwa enzi za mkutano wa Berlin na watawa kama chifu Mangungo umepita, ni juu yetu kuamua tunashirikiana vipi na ujio wa nchi hizo kubwa, kwa hiyo kwa upande fulani tunaweza kusema China imeleta kitu kinachotusaidia. 
Pamoja na kuwa vyombo vya habari vya nchi za Magharibi kuna wakati vinalinganisha uwepo wa China na Marekani, na kama hali ilivyokuwa kwa nchi za Ulaya kabla ya mkutano wa Berlin, Marekani na China zenyewe zimegundua kuwa zina nafasi kubwa ya kushirikiana barani Afrika, kutokana na kuwa maslahi yao barani humo yanafanana kwa kiasi kikubwa.
Kuna maeneo kadhaa yanayoonesha kuwa uwepo wa nchi hizo mbili barani Afrika, umekuwa na manufaa chanya kwenye maeneo mbalimbali ya uchumi, usalama na hata mambo ya kijamii.
Marekani na China na mabadiliko ya hali ya hewa
Hivi karibuni nchi mbalimbali za Afrika Mashariki zimetoa tahadhari ya El-Nino, kuwa mvua zinazotokana na mkondo wa El Nino zinaweza kuleta madhara tena kwenye nchi za Afrika Mashariki. Wataalamu wanasema El Nino inatokana na mabadiliko ya hewa.  Kila suala la mabadiliko ya hali ya hewa linapotajwa, China na Marekani zinatajwa zaidi hasa kwa kuwa ndio watoaji wakubwa wa hewa zinazosababisha kuongezeka kwa joto duniani. 
Mwezi Novemba mwaka jana katika hali ya kushangaa China na Marekani zilitoa taarifa ya pamoja zikiahidi kushirikiana kukabiliana na mabadiliko hayo, na kuweka bayana mpango wa kila upande hadi mwaka 2020 kutekeleza ahadi yao. Ziara hii ya rais Xi Jinping nchini Marekani inakuja miezi karibu mitatu kabla ya mkutano wa mabadiliko ya hali ya hewa wa Paris.
Bila shaka watakachojadili kati ya Rais Xi na Obama, kitakuwa na ushawishi mkubwa fulani katika kufikia mkataba wa dunia nzima wenye nguvu.

Post a Comment

0 Comments