Dodoma. Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) kimewasimamisha masomo zaidi ya
wanafunzi 7,000 wa kozi maalumu ya ualimu wa sayansi kwa ngazi ya
stashahada na kuwataka waondoke chuoni hapo mara moja.
Jana, lilitolewa tangazo chuoni hapo likiwataka wanafunzi hao kuondoka
kati ya jana hadi leo saa 12 jioni. Tangazo hilo lilieleza kuwa kutokana
na matatizo yaliyopo katika ufundishaji wa stashahada hiyo, Serikali
kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi
imeamua wanafunzi hao kurejea majumbani na wataelezwa mustakabali wao
“mapema iwezekanavyo”.
Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Idrisa Kikula alipotakiwa kufafanua
suala hilo, alisema kwa ufupi kuwa suala hilo lipo lakini akaelekeza
apigiwe simu Ofisa Uhusiano wa chuo hicho, Beatrice Baltazal kwa maelezo
zaidi.
Baltazal alipotafutwa alisema kusimamishwa kwa wanafunzi hao kulitokana na agizo la Serikali na wametakiwa kulitekeleza.
Kuhusu lini na nini hatima ya wanafunzi hao, alisema bado hawajui hadi hapo watakapoelekezwa vinginevyo.
Hata hivyo, kulikuwa na malalamiko kwa wanafunzi hao juu ya namna
walivyopewa taarifa za kusimamishwa masomo yao kwa ghafla na kutakiwa
kuondoka.
Kozi ya stashahada ya ualimu wa sayansi, ilianzishwa maalumu kwa agizo
la Rais Jakaya Kikwete kwa lengo la kuziba pengo la walimu wa sayansi na
ilikuwa inatolewa UDOM pekee.
Waliokuwa na sifa za kujiunga na kupewa mikopo ni wanafunzi waliomaliza
kidato cha nne na kufaulu vizuri masomo ya sayansi. Wanafunzi hao
waliokuwa wamekopeshwa na Serikali wamesimamishwa siku mbili baada ya
wenzao zaidi ya 480 wa Chuo Kikuu cha St. Joseph kusimamishwa baada ya
kubainika hawakuwa na sifa za kudahiliwa.
"Source: Muungwana blog"
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena