Wanawake wengi hukabiliwa na mabadiliko mbalimbali ya kimwili na kisaikolojia pale wanaposhika ujauzito.
Mabadiliko hayo hutokana na homoni za uzazi kuzalishwa kwa wingi zaidi. Miongoni mwa mabadiliko hayo katika kipindi hiki cha ujauzito ni pamoja na mama kuhisi kuchoka zaidi ya ilivyokawaida.
Katika kipindi cha mwanzo cha ujauzito, mwanamke anaweza kujikuta akihisi hali ya uchovu mara kwa mara. Na hii inaweza kuwa uchovu wa kawaida au kuchoka sana zaidi ya kawaida ukilinganisha na kipindi ambacho hakuwa na ujauzito.
Mama mjamzito pia huweza kutapika hasa nyakati za asubuhi, hii si hali ya ajabu kwa wanawake wengi wakati wa kipindi cha mwanzo wa ujauzito, lakini wengi pia hujikuta wakiondokana na hali hiyo kadri mimba inavyozidi kukua.
Hata hivyo mama mjamzito wakati wa ujauzito huweza kutapika na anashauriwa kumuona daktari endapo ataona anatapika sana karibu siku nzima.
Hali nyingine ambayo huweza kujitokeza kwa mama mjamzito katika kipindi cha mwanzo ni kupata haja ndogo mara kwa mara. Hii ni kutokana na tumbo la uzazi kuanza kukua na kukandamiza kibofu cha mkojo na hivyo kuchangia kuhisi haja hiyo mara nyingi zaidi.
Matiti kuvimba na kuuma, hii hali pia huweza kujitokeza na huchangiwa na mabadiliko ya kihomoni kwa sababu wakati huo pole pole matiti huanza kukua na kujiandaa kutengeneza maziwa kwaajili ya mtoto hivyo mabadiliko hayo huchangia kuleta hali ya matiti kuvimba na kuuma.
Kukosa hedhi hii ni moja ya ishara kuu ya ujauzito na kwa kawaida haitegemewi mwanamke mjamzito kuendelea kupata siku zake za hedhi isipokuwa kutokwa na damu kidogo (matone kidogo kwenye nguo za ndani kwa siku moja au mbili). Mwanamke anapopata hedhi ya kawaida au kutokwa damu nyingi wakati wa ujauzito huashiria hatari ya ujauzito kutoka, hivyo ni muhimu kwenda hospitali mapema pale hali hiyo inapojitokeza.
Kukosa hamu ya baadhi ya vyakula, kipindi hiki mama huweza kuacha kupenda baadhi ya vyakula au vinywaji hata kama hapo awali kabla ya ujauzito alikuwa anavitumia na wengine hujikuta wakichukizwa na baadhi ya harufu pia.
Pia kuna baadhi ya kinamama wanapokuwa katika hali hii ya ujauzito huweza kuwa wepesi wa kununa na kukasirika na hali hii husababisha hata wengine kujikuta wakiwachukia wenzi wao pia. Hivyo inashauriwa kuwachukulia katika hali hiyo endapo ikiwa hivyo.
Mabadiliko yote hayo hutofautiana kati ya mwanamke mmoja na mwingine, kutoka siku hadi siku na unapopata mabadiliko yanayokupa hofu ni vizuri ukaonana na daktari wako haraka.
Mbali na hayo pi wakati wa ujauzito mama huhitaji kupata lishe bora wakati wote wa kipindi hicho na hata baada ya kujifungua.
Miongoni mwa vinywaji ambavyo huweza kuleta manufaa kwa afya ya mama wakati wa ujauzito ni pamoja na juisi ya karoti.
Juisi hii humsaidia mama mjamzito kwenye upande wa mmeng'enyo wa chakula na hivyo kumuepusha mama dhidi ya ukosefu wa choo kama ilivyo kwa wajawazito wengi hujikuta wakipatwa na tatizo la ukosefu wa choo mara kwa mara.
Pia kinywaji hicho husaidia kuboresha ngozi ya mama mjamzito kwani baadhi ya kinamama wakati wa ujauzito huharibika ngozi zao.
Kinywaji kingine muhimu wakati wa ujauzito ni pamoja na juisi ya boga, ambayo husaidia kumuepusha mama dhidi ya kisukari cha mimba pamoja na ukosefu wa choo na kupunguza uwezekano wa shinikizo la juu la damu.
Pamoja na hayo, wakati wa ujauzito mama huhitajika kuzingatia ulaji wa matunda na mboga za majani. Ikiwezekana nusu ya mlo wake uwe ni matunda na mboga za majani.
Miongoni mwa matunda muhimu kwa kipindi hiki ni pamoja na tikitimaji, ambalo huweza kufanya kazi nyingi kwa mjamzito kwa wakati mmoja.
Matumizi ya tikitimaji husaidia kuzuia tatizo la mwili kuvimba, baadhi ya wanawake wanapokuwa katika hali ya ujauzito hupatwa na matatizo ya miguu kuvimba au mikono, hivyo matumizi ya tikitimaji huweza kutatua tatizo hilo kutokana na tunda hilo kuwa na madini ambayo huweza kuzuia mishipa ya damu isizibe.
Tikitimaji pia husaidia kupambana na homa za asubuhi ‘Morning sickness’, inaelezwa kuwa tunda hili ni nzuri kwa wanawake wajawazito kwani husaidia kuzuia kichefuchefu hususani asubuhi.
Tunda hili pia hupunguza hatari ya mama kukumbwa na upungufu wa maji mwilini kutokana na kusheheni kiwango kikubwa cha maji, hivyo hufaa kwa wanawake hususani wanapokuwa katika hali ya ujauzito.
Pia mjamzito anashauriwa kutumia zaidi nafaka zisizokobolewa kama unga wa dona au mtama, mchele usiokobolewa, mikate ya brown.
Chagua vyanzo vyako vya protini zaidi katika samaki, kuku, mayai, jamii ya maharage, soya na karanga.
Mbali na vyakula hivyom mjamzito kipindi chote huhitajika kunywa maji ya kutosha angalau lita 2.5 kwa siku, huku akizingatia ufanyaji wa mazoezi mepesi ikiwa ni pamoja na kutembea angalau kwa dakika 30 kwa siku.
Sambamba na hayo, mamamjamzito anapaswa kuepuka matumizi ya pombe na dawa za kulevya kwani matumizi ya vitu hivyo huhatarisha afya ya mtoto na huweza kuchangia mtoto kuzaliwa akiwa na ulemavu, hivyo wataalam wa afya hupendekeza mama mjamzito asinywe pombe hata kwa kiwango kidogo.
Pia mama mjamzito hupaswa kuepuka kutumia dawa ovyo pasipo maelekezo maalum ya wataalam wa afya (daktari).
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena