Na Habib Anga (The Bold)
Mwenendo wa utokeaji wa matukio katika maisha ni kana kwamba unafuata mfumo fulani wa mzunguko. Kwamba matukio ambayo yamekwisha kutokea huwa yanajipa muda fulani, labda miaka michache au miongo kadhaa na hata karne kadhaa kabla ya kutokea tena.
Yako mengi ambayo tunaweza kuyajadili kama mfano halisi wa hiki ambacho ninakisema lakini leo hii ningelipenda tutazame sekta na mifumo ya kifedha na utapeli ambao umejaa ndani yake.
Katika miaka ya hivi karibuni mwaka hadi mwaka kumekuwa kukiibuka namna fulani ya upatu ambao umekuwa ukija kwa sura tofauti tofauti lakini ukiwa na matokeo yale yale. Katika miaka ya 2007 mpaka 2009 tulishuhudia kuibuka kwa kampuni ya DECI ambayo iliiteka nchi kwa umaarufu wake lakini pia ilikuja kuiteka nchi kwa vilio ambavyo ilileta. Miaka ya hivi karibuni mchezo ule ule umekuwa unarudi kwa sura nyingine ya kisasa zaidi na za akili zaidi lakini lengo likiwa ni lile lile. Tumeona kuibuka kwa kampuni kama D9 Club, baadhi ya kampuni za biashara za mtandao (japo sio zote) na sasa hivi upatu huu umeingia mpaka kwenye sarafu za kidigitali (cryptocurrency). Nimeshuhudia kuna baadhi ya kampuni ambazo wanawafanyia watu semina ati wawekeze hela kwenye kampuni yao inayojihusisha na biashara ya sarafu za digitali na kila wiki watapokea gawio la kiasi fulani cha fedha. Pia ziko kampuni za bidhaa za vipodozi na afya, hizi ndizo ziko nyingi zaidi ambazo zinatoa ahadi watu wakijiunga nao na kuwafanya kuwa mamilionea ndani ya muda mchache.
Niseme kwamba katika makundi yote hayo ambayo nimeyataja hapo juu ziko kampuni ambazo zinafanya shughuli zake kwa mfumo halali kabisa lakini ziko nyingi zaidi ambazo ndizo haswa nazilenga katika makala hii. Kutaja majina ya kampuni moja moja si sawa sana maana kampuni hizi zinaibuka mpya kila siku na maendeleo ya teknolojia pia yanafanya mifumo hii ya upatu kuboreka na kuwa ya kisasa zaidi na muda mwingine kufanya kuwa ngumu kung’amua haraka haraka kama kampuni husika inajihusisha na upatu ama la. Kuna watu wameenda mbali zaidi na kuanza kuuliza kama pia kampuni za biashara za forex nazo ni upatu.
Lengo la andishi hili fupi ni kujaribu kutazama chimbuko la michezo hii ya upatu, na pindi ambapo tutafahamu kwa usahihi asili ya michezo hii itakuwa rahisi kwetu kuelewa kama mfumo wa kampuni husika ni upatu ama la na hivyo kusaidia kuchukua tahadhari na kujiepusha nazo ili kulinda fedha zetu ambazo tumevuja jasho kuzipata.
Kulipata kuwepo bwana mmoja anayeitwa Charles Ponzi ambaye alikuwa ni mzaliwa wa Lugo huko nchini Italia katika miaka ya 1882. Familia yake ilikuwa ni familia yenye hadhi japo alipofikia umri wa ujana walifilisika na kuwafanya waisi maisha ya kawaida kabisa. Charles Ponzi alibahatika kuchaguliwa kujiunga na chuo kikuu cha Rome La Sapienza ambacho kilikuwa ni chuo cha hadhi kubwa kwa kipindi hicho. Akiwa chuoni hapo kutokana na historia ya maisha ya juu ambayo familia yao walikuwa nayo huko nyuma alijikuta anajenga urafiki na watoto wa matajiri ambao wao miaka mine ya kuwepo hapo chuo waliibatiza jina kuwa ni “four year vacation”. Walitumia muda wao wote kwenye mabaa, mikahawa ya starehe na majumba ya opera. Hii ilimfanya Charles Ponzi kutumia hela hovyo badala ya kusoma na miaka minne baadae alikuwa yuko hoi kiuchumi na madeni makubwa na pasipo shahada ambayo alienda kusomea.
Ikimbukwe kwamba katika kipindi hiki ndipo ambapo kulikkuwa na wimbi kubwa la Waitaliano kuhamia nchini Marekani. Vijana wengi wa Kiitalilano walikuwa wanaenda nchini Marekani wakiwa makapuku na miaka michache baadae wanarejea Italia wakiwa matajiri. Hivyo Charles Ponzi naye aliamua aende Marekani kuusaka utajiri.
Charles Ponzi aliwasili nchini Marekani mwezi November mwaka 1903 akiwa na dola 2 tu mfukoni. Alianza maisha kwa kufanya kazi kwenye migahawa kama muosha vyombo huku akilala chini sakafuni. Ponzi alikuwa ni mtu mcheshi sana na alikuwa anaongea lugha tatu, Kiitaliano, kifaransa, na kiingereza. Hii ilimvutia muitaliano mwenzake aitwaye Luigi Zarossi ambaye alikuwa amefungua benki nchini Canada kuhudumia waitaliano ambao walikuwa wanahamia kwa maelfu kila mwaka. Kwa hiyo Ponzi alijipatia kazi kama ‘teller’ wa benki nchini Canada mji wa Montreal kwenye benki ya Zarossi iliyoitwa Banco Zarossi. Kutokana na ucheshi wake na ukarimu Ponzi alipanda cheo mpaka kufikia ngazi ya meneja wa benki hiyo kwa muda mfupi tu.
Benki hii ilikuwa inalipa interest ya 6% kwa wateja wake. Hii ilikuwa ni mara mbili ya interest ambayo benki nyingine zilikuwa zinalipa wateja wake kwa miaka hiyo. Hii ilisababisha benki hii kukua kwa kasi sana. Ponzi alipoinuka mpaka kuwa na cheo cha meneja wa benki ndipo ambapo alijua siri kubwa ya benki hii ambayo wateja na hata wafanyakazi wa kawaida wa benki hii walikuwa hawaijui. Benki hii ilikuwa inalipa interest kwa wateja wao sio kutokana na faida ambayo walikuwa wanaipata bali walikuwa wanatumia deposits ambazo zilikuwa zinafanywa na wateja wapya. Ndipo hapa ambapo Ponzi alijifunza mfumo huu wa “Kumuibia Peter, Unamlipa Paulo”.
Miaka michache baadae benki hii ilikufa na Zarossi mwenyewe alitoroka na kukimbilia nchini Mexico.
Ponzi alijaribu kutumia kitabu cha hundi cha moja ya wateja wao kujiandikia malipo ya dola 423 lakini polisi walimkamata kabla hajatoroka kurejea Marekani. Alishtakiwa na kukutwa na hatia na kuhukumiwa jela miaka mitatu. Akiwa huko huko gerezani ili kuficha aibu hii na familia yake wasipate wasi wasi aliwaandikia barua kuwadanganya kuwa amepata kazi ya kuwa msaidizi maalumu wa mkuu wa gereza hivyo atachelewa kidogo kurejea Marekani.
Ponzi aliachhiwa mwaka 1911.
Akiwa anarejea MArekani alijaribu kuwakusanya wahamiaji haramu kadhaa ambao walikuwa wanataka kuingia nchini Marekani ambao walimlipa hela na akajaribu kuratibu mpango wa kuwaingiza nchini Marekani kimagendo. Mpamgo huu haukufanikiwa na Ponzi alikamatwa na kutupwa gerezani Atlanta kwa miaka miwili.
Baada ya kuachiwa kutoka gerezani Ponzi alihamia mjini Boston ambako alikutana na bibie Rose Maria Gnecco ambaye alimuoa. Familia Rose Maria walikuwa wanamiliki kampuni ya uuzaji wa matunda yenye mafanikio. Kwa hiyo Ponzi walau alipata auheni ya maisha.
Baade Ponzi alipata wazo la kuanzisha kampuni ya matangazo japo kampuni hii haikupaya mafanikio yoyote yale.
Ndipo hapa ambapo Ponzi alianzisha utaratibu wa kuwaandikia barua watu mbalimbali na hata makampuni nchini Italia akijaribu kuwauzia fursa tofauti tofauti zilizoko nchini Marekni.
Mungu si athumani kampuni moja walijibu barua yake wakitaka wapate nafasi ya kufanya matangazo nchini Marekani. Lakini ndani ya bahasha hii iliyokuja na barua kulikuwa na kitu ambacho Ponzi hakuwahi kukiona kabla maishani mwake, kulikuwa na IRC (International Reply Coupon). IRC inatumika katika namna ambayo mtu unatuma barua kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine na ndani yake unaweka IRC ambayo mpokeaji wa barua yako kwenye nchi ile nyingine anaweza kuitumia kubadilisha na kupewa stamp ya barua ya nchi yake ili aweze kukujibu barua yako na kukutumia. Yaani ni kama vile unakuwa unamlipia gharama za kukujibu barua yako.
Ponzi aliuliza kuhusu IRC na akapewa ufafanuzi namna ambavyo IRCs inavyo fanya kazi. Kichwani mwake taa iliwaka na akang’amua udhaifu katika mfumo wa IRC. Udhaifu huu ambao aliung’amua ulikuwa ni kwamba hizi IRC zinanunuliwa kwa gharama kwa nchi ambayo imetoka na kama ikibadilishwa katika nchi nyingine kunakuwa na utofauti wa bei ambao unaweza kuutumia kujitengenezea faida.
Yaani kwamba, tuseme kwa mfano unamuandikia barua jamaa yako aliyeko Marekani, ndani yake ukaweka IRC ili aweze kukujibu. Hiyo IRC unainunua hapa Tanzania kwa shilingi mia tano mathalani. Jamaa yako kule Marekani akipokea barua ataichukua ile IRC na kwenda ofisi ya posta na kupewa stamp za kawaida za barua ili aweze kuituma ile barua yake ya kukujibu. Sasa basi tumesema kwamba ile IRC huku Tanzania inauzwa shilingi mia tano, na labda kule Marekani stamp ya barua inauzwa dola moja.
Kwa hiyo jamaa yako akienda kuibadili ile IRC uliyomtumia (ambayo umeinunua kwa shilingi mia tao) atapewa stamp ya barua ambayo ina thamani ya dola moja (shilingi 1200) kwa hiyo kama hataitumia ile stamp kukutumia barua na kuamua kuiuza mtakuwa mmepata shilingi 1200 yaani faida ya shilingi mia saba za kitanzania.
Huu ndio udhaifu wa mfumo huu ambao Ponzi aliungundua na kuamua kuutumia ajitengenezee utajiri. Hiki ni kipindi ambacho vita kuu ya kwanza ya dunia ndio ilikuwa imetoka kuisha, uchumi wa Italia ulikuwa umeyumba haswa na kuifanya sarafu yake kushuka thamani kwa kiwango kikubwa sana dhidi ya dola ya Marekani. Ponzi mwenyewe alidai kwamba zile IRC zikinunuliwa Italia na kubadilishwa huku Marekani kwa stamp za barua zitaleta faida ya zaidi ya 400% kwa kila kuponi.
Ponzi aliingia benki kadhaa kuomba mkopo kuanzisha biashara hii lakini mabenki hawakupendezwa na wazo lake hili. Akahamia kwa ndugu na jamaa na marafiki akiwataka wafanye uwekezaji na ndani ya siku 90 atawalipa mara mbili zaidi. Baadae ili kuwavutia zaidi akapunguza siku na kuwaeleza kuwa ndani ya siku 45 tu atawalipa fedha zao walizowekeza mara mbili zaidi. Hiki ni kipindi ambacho mabenki walikuwa wanalipa interest ya 5% kwa hiyo ofa ya Ponzi ilikuwa ni nono kweli kweli.
Ponzi akaanzisha utaratibu wa kufanya kam mikutano midogo hivi (au twaweza sema semina) kukutana na watu ambao alitaka wawekeze kwenye huo mpango wake. Katika mwezi wa kwanza pekee watu 18 waliwekeza jumla ya dola 1800. Mwezi uliofuata aliwalipa watu hawa mara mbili ya mitaji ambayo waliwekeza.
Kitu ambacho wawekezaji hawa hawakufahamu ni kwamba Ponzi alikuwa hanunui kuponi za IRC na kuziuza bali alikuwa anawalipa kwa kutumia fedha za watu wapya ambao walikuwa wanajiunga. Maneno matamu ya kutumia kuponi za IRC kubadilisha kwa stamp za barua ilikuwa ni chambo ya kujaribu kuhalalisha kile ambacho alikuwa anakifanya.
Baada ya mkupuo wa kwanza wa wawekezaji kulipwa mara mbili ya uwekezaji wao, watu wakaanza kumiminika kwa kasi zaidi. Ndani ya miezi miwili tu uwekezaji ulikuwa kutoka dola 1800 mpaka kufikia dola 25,000 (sawa na kama dola 310,000 kwa mwaka huu 2018). Ponzi akafungua ofisi kubwa kwenye jengo la kifahari liitwalo Niles na mradi wake huu akaufungulia kampuni rasmi kabisa ambayo iliitwa Securities Exchange Company. Akaajiri mawakala wa kutafuta ‘wawekezaji’ wapya. Mawakala wake alikuwa anawalipa commission nono kwa kila mteja mpya ambaye walikuwa wanamleta kuwekeza.
Watu walimiminika kutoka kila kona ya Marekani kwenda kuwekeza kwenye mradi wa huu wa Charles Ponzi. Mpaka kufikia mwezi May mwaka huo 1920 Ponzi alikuwa amepokea uwekezaji wenye thamani ya dola 420,000 kutoka kwa wananchi (sawa na dola milioni 5 kwa mwaka huu 2018). Mwezi uliofuta, June uwekezaji huu ulikua na kufikia dola milioni 2.5 (sawa na dola milioni 30 mwaka huu 2018). Mpaka kufikia mwanzoni mwa mwezi July, Ponzi alikwa anapata uwekezaji wa dola milioni moja kwa wiki na mwishi wa mwezi huo huo Ponzi alianza kupokea kiasi cha dola milioni moja kila siku.
Ponzi alionekana kama shujaa ‘aliyeshushwa’ kuwaokoa masikini. Watu waliuza nyumba zao ili wawekeze kwa Charles Ponzi. Mbaya zaidi watu walikuwa wakilipwa faida zao mwisho wa mwezi hawazichukui, bali wanaziwekeza tena ili mwezi unaofuata walipwe faida kubwa zaidi.
Charles Ponzi alizidi kushamiri. Ndani ya muda mchache sana alibadili maisha yake kutoka kuwa muhangaikaji asiye na mbele wala nyuma na sasa alikuwa milionea mwenye kuheshimika nchi nzima ya Marekani. Utajiri wa Ponzi ulifikia mkubwa kiaisi kwamba fedha zake ambazo alikuwa anazitunza katika benki ya Hanover Trust Bank zilikuwa nyingi kukaribia mtaji wa benki na Ponzi alianza kuilazimisha benki wampe wadhifa wa kuwa ‘President’ wa benki hiyo.
Watu waliokuwa wanawekeza kwenye mradi huu wa Charles Ponzi sio hoe hae tu, bali hata watu wenye heshima zao. Ilifika kipindi karibia 75% ya maafisa wa polisi wa Boston walikuwa wanawekeza mishahara yao kwenye kampuni ya Charles Ponzi. Hata watu maarufu nao waliwekeza kwenye mradi huu na Ponzi aliwatumia sana kwenye matangazo yake.
Waswahili wana msemo wanasema, masikini akipata… makalio hulia mbwata. Ndicho ambacho kilijidhihirisha kwa Charles Ponzi. Ponzi alibadili mfumo wake wa maisha na kuishi maisha ya anasa kubwa ili kuwadhihirishia watu kuwa mradi wake ‘unalipa’ na hivyo wawekeze. Alinunua kasri la mamilioni ya dola kwenye maeneo ya kitajiri ya Massachusetts. Akanunua gari la gharama zaidi kipindi hicho lililoitwa Locomobile. Alinunua kampuni ya kutengeneza macaroni. Akanunua kampuni ya kutengeneza mvinyo nchini Italia. Na pia akafanya shughuli za kibinadamu kama vile kujitolea kiasi cha dola milioni 1.5 kufadhili kituo cha watoto yatima nchini kwake Italia.
Ponzi alikuwa ni shujaa wa kila mtu, mkombozi wa kiuchumi, mfano wa kuigwa, mjasiriamali nguli na mtoa misaada… lakini ukweli wa mambo alikuwa anaujua yeye pekee moyoni mwake.
Japokuwa katika mahojiano yake ya redio na magazeti alikuwa anaeleza kwamba kampuni yake inawekeza kwenye kuponi za IRC na kuwezesha kutengeneza faida kubwa hivyo, lakini uhalisia ni kwamba alikuwa anatumia fedha za watu wapya wanaojiunga kuwalipa wale wa zamani. Alikuwa anatumia falsafa rahisi tu, “Muibie Peter, mlipe Paulo”.
Kuendesha mradi mkubwa hivi kwa kutumia kuponi za IRC ilikuwa haiwezekaniniki… kwa mfano wale watu wa kwanza kabisa ambao waliwekeza jumla ya dola 1800 ili kuwalipa ingehitajika kusafirisha kuponi 53,000 kutoka Itali na kuziuza. Mradi ulipokuwa na kufikia wawekezaji 15,000 ilihitaji kujaza kuponi kwenye meli kubwa kama Titanic na kuzisafirisha mpaka Marekani na kuziuza. Kwa maneno mengine mradi wa Ponzi kuuza kuponi kinadharia ulikuwa unaonekana uko sahihi lakini kiutekelezaji lilikuwa ni suala ambalo haliwezekani abadani.
Lakini mafanikio haya ya haraka mno na ahadi ambazo kampuni ya Charles Ponzi ilikuwa inatoa kwa wawekezaji wake ilifanya baadhi ya watu waanze kupata wasiwasi. Kuna muandishi wa makala za uchambuzi wa uchumi aliandika andishi katika gazeti la Boston kueleza kuwa mradi wa Charles Ponzi ulikuwa ni utapeli. Lakini Ponzi alimshitaki kwa kumuharibia jina lake na akashinda kesi na gazeti la Boston wakatakiwa kumlipa fidia ya dola 500,000.
Hii ilifanya watu wengine waliokuwa na wasiwasi kukaa kimya wasihoji hadaharani mfumo wa uendeshaji wa mradi wa Ponzi.
Badala yake magazeti yalianza kumuandika Ponzi kwa uzuri zaidi. Gazeti la Boston Post liliandika makala ukurasa wa mbele likieleza namna ambavyo mradi wa Charles Ponzi unawalipa wawekezaji 50% ndani ya siku 45 tu. Mbaya zaidi chini ya makala hii liliwekwa tangazo la benki likionyesha kuwa wanalipa wawekezaji 5% kwa mwaka.
Hii iliwehusha akili za watu. Kesho yake Charles Ponzi alipofika ofisini alikuta kuna maelfu ya watu wanamsubiri nje wakitaka ‘kuwekeza’. Kundi la watu lilikuwa kubwa kweli kweli kana kwamba ni mkutano mkubwa wa kisiasa.
Ponzi alizidi kushamiri. Lakini wenye akili nao wasiwasi haukuondoka walizidi kuhoji japo chini kwa chini.
Minong’ono hii na wasiwasi ilimfikia mpaka Daniel Gallagher ambaye alikuwa ni mwanasheria mkuu wa seriakli eneo la Massachusetts. Akateua wataalamu wa masuala ya fedha ili kuichunguza kampuni ya Charles Ponzi. Wataalamu hawa aligundua kuwa ili Ponzi aweze kutengeneza faida ambayo alikuwa anasema, inapaswa kuwa na kuponi milioni 160 ziwe kwenye mzunguko lakini badala yake kulikuwa na kuponi 27,000 kwenye mzunguko. Na hata ofisi ya Taifa ya posta walipoulizwa walitoa taarifa kuwa hakujawa na ununuaji wowote mkubwa wa stamp za barua wala kubadilishwa na kuponi za IRC.
Wataalamu hawa pia waligundua kuwa hata kama kuponi hizo zingenunuliwa, rasilimali watu ambayo ingehitajika kuziuza ingelikuwa ni ghali sana kiasi kwamba isingemletea Ponzi faida yoyote zaidi ya hasara tu. Na hata kama biashara hiyo ingefanikiwa maana yake ni kwamba angekuwa anajitajirisha kwa kuitia hasara serikali kwa makusudi kabisa.
Habari hii ilivuja kwenye vyombo vya habari na ilisababisha taharuki kubwa kwa wananchi waliowekeza kwenye kampuni ya Charles Ponzi. Kesho yake walijaa ofisini kwake kwa maelfu wakitaka kuwithdraw pesa zao. Moja kati ya turufu ambazo Ponzi alikuwa nazo ni kiwango kikubwa cha kujiamini. Hakubishana nao. Akafunga mahema nje ili wasichomwe na jua na kuwawekea viti. Kisha kila mtu akapewa kahawa na vitafunwa. Akaanza kuwaeleza kuwa hakuna ‘ujanja ujanja’ wowote kwenye kampuni yake lakini kama wanataka kutoa fedha zao hawezi kupinga, atawapa lakini wafahamu kuwa wanapoteza fursa kubwa ya maisha yao. Na kweli akaanza kuwapa watu hela zao. Wale wengine walivyoona hivi wakaghairisha kuchukua fedha zao. Wakamuomba radhi kwa kumtilia shaka na kuondoka.
Lakini uchunguzi wa mwanasheria mkuu wa serikali uliendelea na waligundua madudu makubwa zaidi. Maelfu ya watu walikuwa tayari wamejiunga na mradi huu wa Ponzi na ilifika kipindi watu waliokuwa wanajiunga walikuwa wachache kuzidi wale ambao walikuwa tayari wamejiunga wanasubiria kulipwa faida zao. Maana yake ni kwamba japo huku nje Ponzi alikuwa anaonekana anashamiri lakini kiuhalisia kampuni hiyo ilikuwa inajiendesha kwa hasara kubwa na siku si nyingi angeshindwa kuwalipa wawekezaji wake. Wataalamu hao waligundua pia kuwa kutokana na kampuni ya Ponzi kuwa na akaunti nyingi kubwa mno katika benki mbali mbali kama ikitokea kampuni yake ikicollapse basi na mfumo mzima wa benki eneo la Boston utacollapse.
Nilieleza awali kwamba, Ponzi kutokana na ukubwa wa akaunti yake alikuwa amepata wadhifa mkubwa ndani ya Hanover Trust Bank. Alitumia mwanya huu kuidhinisha mikopo mikubwa kwa kampuni yake.
Mwanasheria mkuu wa serikali aliligundua hili kwenye uchunguzi wake, kwamba kampuni ya Ponzi tayari ilikuwa kwenye mstari mwekundu, hakuwa na uwezo wa kulipa wawekezaji wake, watu wanaojiunga walikuwa ni wachache kuliko wale anaopaswa kuwalipa. Kwa hiyo kampuni ya Charles Ponzi ilikuwa inatumia mikopo hii kulipa watu wa mwanzoni kujiunga.
Lakini pia mwanasheria mkuu akapewa historia ya Ponzi ambayo watu walikuwa hawajui, hata mkewe, hata familia yake… rekodi yake ya kufungwa mara mbili jela kwa makosa ya jinai. Moja lile alilofanya Canada kwa kujaribu kujiandikia hundi na kughushi sahihi. Na pili kuratibu mpango wa kuingiza wahamiaji haramu nchini Marekani
Hakukuwa na haja ya kusubiri tena. Charles Ponzi alikamatwa na kushtakiwa. Kesi yake iliunguruma na kukutwa na hatia na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela. Lakini Ponzi ni mwenye kujua kupenya akili ya mtu, alifanya deal na serikali na upande wa mashitaka na adhabu hiyo kupunguzwa mpaka miaka mitano tu.
Wawekezaji wake uraiani walibakia na vilio. Watu walikuwa wameuza majumba, wengine wametumia akiba zao za maisha, wengine wametumia ada za shule, wengine urithi wao… wote hawa waliwekeza kwa Charles Ponzi ili wapate kutajirika haraka. Lakini ambao walivuna pesa walikuwa watu wachache sana wa mwanzoni, na maelfu waliobaki hawakuambulia hata senti tano kipande. Inakadiriwa kwamba hasara ambayo Charles Ponzi aliisababisha inafikia dola milioni 700 kwa viwango vya leo hii mwaka 2018 (zaidi ya shilingi Trilioni 1.6 za kitanzania).
Baada ya kutoka gerezani Charles Ponzi alirudishwa nchini kwao Italia. Huko baada ya miaka kadhaa ya kuhangaika mtaani hatimaye alifanikiwa kupata ajira katika shilinga la ndege la nchi ya Italia akiwa kama wakala nchini Brazili. Mwishoni mwa uhai wake upande mmoja wa mwili wake ulipooza na uwezo wake wa kuona ulikuwa hafifu katika kiwango cha kama alikuwa kipofu kabisa. Akiwa nchini Brazili katika mahojiano yake ya mwisho na vyombo vya habari mwaka 1948 alipoulizwa anajisikiaje kwa kile amabcho alikifanya… Charles Ponzi aliwajibu kuwa “…hata kama wawekezaji hawakupata kitu, lakini niliwapa kitu ambacho walikipata kwa bei nafuu sana. Ukiacha kunihukumu kwa ufedhuli, lazima utakubaliana nami kuwa nilichokifanya ilikuwa ni ‘show’ maridhawa zaidi kuwahi kutokea tangu mtu yeyote kukanyaga mguu kwenye ardhi ya Marekani. Kama ningeliuza tiketi watu kushuhudia ‘show’ ile nadhani labda tiketi moja ingegharimu dola milioni 15..”
Mradi huu wa Charles Ponzi ndio ambao ulisababisha hata wanataaluma kuanza kutafiti mifumo ya kibiashara yenye kufuata mkondo huu. Na hii ndio asili ya biashara za upatu ulimwenguni mpaka leo hii kubatizwa jina la “Ponzi Schemes”.
Unaweza kujiuliza ni kwa naman gani watu wametapeliwa kirahisi namna ile? Walikuwa ni mazuzu kiasi gani? Hapana, si uzuzu wala umbumbumbu, bali ni mwanya ambao upo katika saikolojia ya binadamu…mwanya ambao akitokea mtu mwenye uwezo wa kuutumia vizuri anaweza kumtapeli hata msomi kabisa wa karne hii. Udhaifu ambao binadamu wote tumeubwa nao… greedy..tamaa!! kutaka kufikia ndoto kwa haraka, kutaka ‘shortcut’.
Udhaifu huu ungali unatugharimu hata leo hii, ni juzi juzi tu hapa mwaka 2008 ambapo Bilionea Bernard Madoff ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa soko la hisala NASDAQ, kampuni yake ya Madoff Investment iligundulika kuendesha ‘Ponzi Scheme’ ambayo ilisababisha hasara ya dola bilioni 18 za wamarekani wenzake (zaidi ya shilingi trilioni 40 za kitanzania). Pia ni juzi juzi tu hapa mwaka 2009 ambapo ‘Ponzi Scheme’ iliyoitwa DECI hapa nchini kwetu imesababisha hasara ya mabilioni ya shilingi za watanzania. Mbaya zaidi hizi Ponzi scheme bado zingalipo hata leo hii mwaka 2018 hapa nchini kwetu zikija na majina tofauti na sura mbali mbali za kupendeza… lakini zote zinafuata falsafa ile ile, falsafa ya Charles Ponzi ambayo imedumu kwa zaidi ya karne… “Muibie Peter, Mlipe Paulo.”
Keep your eyes open. Mchana mwema chiefs,
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena