OPERATION OPERA
"…katika siku hiyo ambayo BWANA aliwatoa Waamori mbele ya wana wa Israeli; akasema mbele ya macho ya Israeli, wewe Jua, simama kimya juu ya Gibeoni;Na wewe Mwezi, simama katika bonde la Aiyaloni."
- JOSHUA 10:12
Ze'ev Raz kiongozi wa marubani wa ndege za kivita pamoja na wenzake anaowaongoza walioko kwenye ndege nyingine za kivita walikuwa wakitamka tena na tena mstari huu biblia kutoka agano la kale katika vinasa sauti vyao vya ndege.
Kwa mara nyingine wakatamka tena na tena…
"…katika siku hiyo ambayo BWANA aliwatoa Waamori mbele ya wana wa Israeli; akasema mbele ya macho ya Israeli, wewe Jua, simama kimya juu ya Gibeoni;Na wewe Mwezi, simama katika bonde la Aiyaloni."
Hii ni moja kati ya aya kadhaa za Taurat ambazo zinatumiwa na jeshi la Israel kutamka ushindi dhidi ya adui.
Ze'ev Raz na wenzake walikuwa wanatamka aya hii kwa furaha na kushangilia kwenye msafara wa ndege nane aina ya F-16 na ndege sita aina ya F-15 zikiwa zinatembea kwa kasi ya juu kabisa kuelekea Etzion Airbase karibu kabisa na mpaka wa Israel na Misri.
Japokuwa Ze'ev na wenzake walikuwa katika kiwango cha juu kabisa cha furaha lakini huko chini watu wachache sana ambao walikuwa japo wanahisi kujua nini kimefanyika walikuwa kwenye mkanganyiko mzito na kutoamini kuziona ndege hizo zikipita angani kurejea Etzion Airbase.
Kutokuamini kwao kulitokana na kutokuwezekana kwa namna yoyote ile kwamba ndege hizi na marubani wake kuwa hai mpaka muda huu. Hii inatokana na ukweli kwamba dakika kadhaa zilizopita msafara huu wa ndege za kivita ulipita katika anga la ghuba ya Aqaba kaskazini magharibi mwa Saudi Arabia. Kwa bahati mbaya, Mfalme Hussein, ambaye alikuwa mfalme wa nchi ya Jordan kipindi hicho alikuwa kwenye mapumziko katika eneo hili la Aqaba kwa kutumia boti yake ya starehe.
Pasipo kujua marubani hawa wa Israel walipopita eneo hili la ghuba ya Aqaba kwa kuwa walikiwa wanarusha ndege chini chini sana ili kukwepa kuonekana na 'radar' walirusha ndege zao kupita juu kabisa ya boti ya Mfalme Hussein wa Jordan. Mfalme Hussein alifanikiwa kuona nembo zilizopo kwenye ubavu wa ndege hizi zote na kutambua kuwa zilikuwa ni ndege za kivita za jeshi la anga la Israel. Na kutoka na muelekeo waliokuwa wanaenda aliamini kabisa kwa asilimia kubwa ndege hizo zilikuwa zinaelekea ncini Iraq ambako kwa kipindi hicho mahusiano ya Israel na Iraq yalikuwa tete kuliko hata hivi sasa.
Mfalme Hussein hakuwa na hakika haswa msafara huo wa ndege za kivita ulikuwa una nia gani haswa kuingia Iraq au 'target' yao hasa ilikuwa ni ipi, lakini alikuwa na hakika kabisa kulikuwa na harufu ya damu inanukia. Damu ya watu wa Iraq muda mchache ujao itamwagika na ulimwengu utatikisika.
Mfalme Hussein aliamuru jeshi lake kuwapa taarifa jeshi la Iraq juu ya uwepo wa ndege za kivita za Israel zinazoruka chini chini kuepuka rada kwa lengo la kuingia kwenye anga la Iraq kinyemela.
Kutokana na taarifa hii ambayo jeshi la Jordan kwa amri ya mfalme lilitoa kwa jeshi la Iraq kulikuwa na uhakika kabisa kwamba ndege hizi za kivita za Israel zitadunguliwa pindi tu hata pua zake zikigusa anga la Iraq.
Ndio maana ilikuwa inashangaza haswa kuona muda mchache baadae msafara huu wa F-15 na F-16 za Israel ukirejea wakiwa salama salimini na wakionekana kuwa wametekeleza walichoenda kukifanya.
Wakati Mfalme Hussein akiwa bado ameduwaa kwa kuona ndege hizo zikirejea, wakati ambapo jeshi la Iraq nalo liko kwenye kigagaziko wasielewe nini kimetokea, na wakati ambapo Iran na hata Marekani wasiamini kitu ambacho kimefanywa na Israel bila hata kuwashirikisha, kule juu angani Ze'ev Raza na wenzake waliendelea kufurahi kwa kunukuu tena na tena aya hii kutoka agano la kale kitabu cha joshua;
"…katika siku hiyo ambayo BWANA aliwatoa Waamori mbele ya wana wa Israeli; akasema mbele ya macho ya Israeli,Wewe Jua, simama kimya juu ya Gibeoni;Na wewe Mwezi, simama katika bonde la Aiyaloni."
Ni dhahiri kwamba kuna jambo la kipekee lilikuwa limetokea katika ulimwengu wa medani za kijeshi… jambo la weledi wa juu zaidi. Oparesheni ambayo itaenda kwenye vitabu vya historia kama moja ya oparesheni ya kijeshi iliyofanikiwa zaidi na ya weledi wa juu zaidi.
Lakini kabla ya yote, tujiulize swali ambalo Mfalme Hussein alijiuliza akiwa kwenye boti yake ya mapumziko na kuona msafara wa F-15 na F-16 za Israel zikipita… what happened??
MWAKA MMOJA ULIOPITA - 1980
Kabla sijaeleza tukio muhimu lililotokea mwaka 1980 ambalo lilitangulia tukio kuu la 1981 nieleze kwa kifupi sana historia fupi…
Nchi ya Iraq katika miaka ya 1960 ilianzisha programu za nyuklia ambao walitanabaisha kuwa ni kwa matumizi ya kisayasi na nishati.
Ilipofika katikati ya miaka ya 1970 Iraq ilianza kupanua miradi hii kwa kuanza kununua vinu vya urutubishaji. Mwanzoni harakati hizi japokuwa zilikuwa zinafuatiliwa kwa karibu na mataifa ya magharibi lakini hawakuzitilia maanani sana kwa kuwa hawakuona uwezo wa kiutendaji na kisayansi kwa Iraq kutumia miradi hii kuunda silaha za atomiki. Lakini baadae mwishoni mwa miaka ya 1970 Iraq ilifanya kitendo ambacho kilisababisha mataifa ya magharibi na hata maadui zake kwenye nchi za kiarabu waanze kuwaangalia kwa macho yote mawili.
Serikali ya Iraq ilipeleka ombi kwa nchi ya Ufaransa wauziwe kinu cha kurutubisha plotonium ambacho kinafanana kabisa na kile ambacho kinatumiwa na nchi ya Ufaransa kutengeneza silaha. Pamoja na kinu hiki Iraq pia walikuwa wanataka wauziwe na kinu cha 'uchakataji rejea' (reprocessing plant) kwa ajili ya kuvuna tena plotonium inayotoka kwenye kinu kikuu cha kwanza.
Vinu hivi vya nchi ya ufaransa ambavyo vilikuwa vikitumiwa kutengeneza silaha za nyuklia vilijulikana kama Osiris… jina la Mungu wa wafu wa Kimisri.
Ombi hili la kununua vinu vya urutubishaji lilikataliwa moja kwa moja na nchi ya Ufaransa kwa kuhofia mahusiano yake na maswahiba wake wa magharibi kuzorota.
Lakini kama misemo yote ya kulaani pesa isemavyo, "pesa mwanaharamu" au "pesa shetani" na kadhalika ndicho ambacho kiliwakengeusha Ufaransa.
'Dau' ambalo lilikuwa linawekwa mezani na Iraq lilikuwa ni nono kiasi kwamba ilikiwa ni sawa na wendawazimu kulikataa. Iraq walikuwa wako tayari kulipa kiasi cha dola milioni 300 kwa ajili ya biashara hii na ufaransa (kumbuka hii ni miaka ya 1970).
Nchi ya ufaransa ilikataa ombi la kuwauzia Iraq vinu vya kurutubisha plotonium na badala yake wakatoa pendekezo la kujenga vinu vya "tafiti" nchini Iraq pamoja na maabara zake. Kwa mujibu wa makubaliano yao vinu hivi ambavyo vitajengwa nchini Iraq vitafanana kabisa na vinu vya Osiris vya nchini Ufaransa lakini havitawekewa ufanisi wa kuweza kuunda silaha.
Japokuwa makubaliano yao ambayo yalitangazwa kwenye vyombo vya habari walijitahidi kuyapamba kuonekana wazi kabisa kwamba mpango huu ulikuwa ni wa kisayansi tu na utafiti na wala haukuwa na nia yoyote ya kuunda silaha lakini mataifa ya magharibi pamoja na maadui wa Iraq kipindi hicho wakiongozwa na Iran walisikia harufu mbaya kwenye mpango huu wa Ufaransa na Iraq. Walihisi harufu ya damu. Walihisi kifo kinabisha hodi milangoni mwao.
Wakaelekeza macho na masikio yao kwenye mradi huu wa Ufaransa na Iraq.
Mkataba ukasainiwa. Na ujenzi wa mradi ukaanza.
Kwa hiyo, mkataba huu ulikuwa na makubaliano ya ujenzi wa kinu kikubwa (Osiris-class reactor), kinu kidogo cha uchakataji rejea (Isis-type reactor), kutoa mafunzo kwa wanasayansi wa Iraq pamoja na Ufarasana kuipatia Iraq kilo 72 za Uranium amabyo imerutubishwa kwa 93%.
Iraq ikatenga eneo maalum karibu na mji mkuu wa Baghdad ambalo kituo hiki cha "utafiti" cha ukubwa wa Megawati 40 kilijengwa na kupewa jina la AL TUWAITHA NUCLEAR RESEARCH FACILITY ambapo kinu kikubwa walikipa jina la OSIRAK (walitohoa na kuunganisha majina Osiris na Iraq) lakini serikali ya Iraq wenyewe walipendelea kukiita kinu kikubwa Tammuz 1 na kinu kidogo Tammuz 2. (Tammuz ni mwezi katika kalenda ya kibabeloni, mwezi ambao ndio chama tawala cha Ba'ath kiliingia madarakani nchini Iraq).
Ndani ya muda mchache sana harakati za "tafiti za nyuklia" nchini Iraq zilishika kasi ya ajabu kiasi kwa ikageuka kama ni agenda kuu ya muelekeo mpya wa nchi yao.
Hili lilikuwa ni jambo jema sana kwao kwa madhumuni yoyote yale ambayo walikuwa nayo eidha walikuwa wanayasema (tafiti) au walikuwa hawayasemi (silaha). Lakini maadui wa Iraq mioyo yao ilikuwa ikienda mbio zaidi kwa sababu walijua pasina shaka, kulikuwa na harufu ya damu milangoni mwao.
Mwezi July, 1980 Iraq walipokea mzigo wa kwanza wa kilo 12.5 ya HEU (Highly Enriched Uranium) maalumu kwa ajili ya kuanza kazi katika vinu vyake vya nyuklia na hapa ndipo moto… moto wa kifuu hasa ulianza kuwaka kati ya Iraq na mahasimu wake.
Ufaransa walidai kwamba wanahakikisha kwa muda wowote ule hakutakuwa na kiwango cha HEU kufikia kilo 25 ndani ya Iraq (kiwango cha chini labda kama unataka kuunda silaha).
Lakini vyombo mbali mbali vya Intelijensia vilidai kuwa kulikuwa na kiwango kingine zaidi cha HEU ambacho kilikuwa kinaingizwa kinyemela katika maabara za siri karibu na vilipo vinu vya Tammuz 1 na Tammuz 2.
Kadiri ambavyo joto la mahasimu lilikuwa linapanda ndivyo ambavyo Iraq ilizidi kuchanja mbuga na "tafiti" zake.
Ndipo hapa ambapo maswahiba wawili kipindi hicho, Israel na Iran (yes Israel na Iran walikuwa maswahiba wakubwa kipindi hicho kutokana na wote kuwa na adui mkuu mmoja, Iraq) walikaa chini na kuja na mpango maalumu ambao Iran walikabidhiwa jukumu la kuutekeleza. Mpango huu wa kijasusi uliitwa Operation Scorch Sword.
Naomba tukumbuke kwamba makala hii inaeleza kuhusu oparesheni OPERA. Nikirudi nitaeleza ni namna gani oparesheni ya kijasusi ya Scorch Sword ilihusika kufanikisha Oparesheni Opera.. na je Operesheni Scorch Sword ilihusu nini hasa.
SEHEMU YA PILI
Katika sehemu hii naomba nieleze kwa ufupia sana juu ya Operation Scorch Sword. Tusichanganye kwamba makala hii inahusu Operation Opera ambayo ilitekelezwa na jeshi la Israel na hii Operation Scorch Sword ilitekelezwa na jeshi la Iran.
Sasa basi, katika miaka ya 1970s kulikuwa na uhasma mkubwa sana kati ya Iraq na majirani zake hasa hasa nchi ya Israel na Iran.
Mbaya zaidi mwaka 1979 yalifanyika mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Wananchi wa Iran wakiongozwa na Ayatollah Khomeini walimpindua mfalme Mohammed Reza Shah Pahlavi na kuanzisha jamuhuri ya Kiislamu.
Hili lilikuwa ni tishio lingine kwa Iraq wakihisi kwamba kutokana na mapinduzi ya Iran yaliongozwa na Washia, walihisi kitendo hicho kinaweza kuigwa na Washia wa Iraq kuipundua serikali yao ambayo ilikuwa imetawaliwa na Wasuni wa chama cha sias cha Ba'ath.
Lakini pia kulikuwa na mgogoro wa muda mrefu wa mpaka ambao ulikuwa unafurukuta kwa miaka yote. Iraq walikuwa wanataka kulimega jimbo la Khuzestan lenye utajiri mkubwa wa mafuta pamoja na ukanda wa mashariki wa Shatt al-Arab.
Sababu hizi ndizo zilipelekea Iraq na Iran kuingia kwenye vita kuanzia siku ya tarehe 22 september 1980. Vita hii ilidumu kwa muda wa miaka nane na kumalizika mwaka 1988.
Katika sehemu ya kwanza nilieleza juu ya mpango wa nyuklia wa Iraq kuanzia miaka ya 1970s. Kwa hiyo vita kati ya Iraq na Iran ilipolipuka hofu kuu ya kwanza ya Iran ilikuwa ni juu ya mpango huu wa Nyuklia wa Iraq. Walihofia Iraq wanaweza kuunda bomu la nyuklia na kulitumia dhidi yao.
Kwa hiyo wakati vita ikiendelea walidhamiria kuweka mkakati wa dharura kuhakikisha kwamba wanasambaritisha vinu hivi vya nyuklia vya Iraq.
Kabla ya mapinduzi ya Iran, nchi hiyo ilikuwa inashika nafasi ya tano kwa kuwa na jeshi imara zaidi duniani. Lakini baada ya mapinduzi walikuwa wamempoteza moja ya maswahiba wake muhimu zaidi, Marekani ambaye alikuwa anaunga mkono utawala wa Mfalme Mohammed Reza Pahlavi kibaraka wao waliyemuweka madarakani ambaye alikuwa amepinduliwa.
Marekani ndiye alikuwa 'supplier' mkuu wa vifaa vya kijeshi na vipuri kwa Iran. Lakini baada ya mapinduzi ya mwaka 1979 Marekani aliwawekea vikwazo vya kiuchumi na Kijeshi nchi ya Iran.
Kwa hiyo Iran wakati inaingia vitani walikuwa hawana nyenzo za kutosha za kijeshi kuikabili Iraq.
Na vita ilivyoanza tu mbele yao walikuwa na changamoto ambayo walipaswa kuishughulikia mara moja, Osirak… lakini hawakuwa na vifaa vyenye ufanisi wa kutosha.
Hii iliwalazimu Israel kuingiza kwa siri kubwa vipuri vya ndege za kijeshi kwenda Iran ili kufanikisha Oparesheni hii.
Mabaki ya Osirak Nuclear Reactor
Lakini changamoto ya pili ambayo walikuwa nayo ilikuwa na watu wenye weledi wa kutosha kutekeleza oparesheni hii.
Sehemu kubwa ya maafisa wa Air Force ya Iran walikuwa wameuwawa kwa kupigwa risasi baada ya mapinduzi ya 1979 na serikali mpya.
Kama hii haitoshi, nilieleza kwamba Marekani walikuwa wamewawekea Iran Vikwazo vya kijeshi baada ya mapinduzi ya mwaka 1979. Kwa hiyo jeshi la Iran walikuwa wamepokonywa mpaka uwezo ambao walipewa awali kabla ya mapinduzi kuaccess ya 'spy satellite' za Marekani.
Kwa hiyo jeshi la Iran hawakuwa na layout nzuri ya kinu cha Osirak namna kilivyo ili waweze kufanya tathimini na hatimaye kufanya chaguo zuri zaidi la namna ya kushambulia.
Lakini pia kutokana na nchi hizo mbili kuwa karibu karibu sana… Iran walikuwa na hofu ya kutokea kwa 'radioactive fallout'. Kwamba kama watalipua vinu hivyo vya nyuklia kienyeji bila kuwa na layout nzuri ya namna kilivyo, mlipuko huo wa nyuklia unaweza kusombwa na upepo na presha ya anga na kufika mpaka Iran na hatimaye kuleta madhara nyumbani kwao.
Ndipo hapa ambapo Iran ikafikia uamuzi kwamba shambulio ambalo watalifanya kwenye majengo yale ya kinu cha Osirak, yalenge research labaratories, control rooms na trainings facilities bila kugusa vinu vyenyewe. Kwa hiyi lengo hili lilikuwa linamaanisha kwamba walikuwa wanataka kukwamisha shughuli za urutubishaji nyuklia au kuzichelewesha na kuviruga.
Siku ya tarehe 30 septemba 1980 siku nane baada ya vita ya Iran na Iraq kuanza, marubani wa ndege za kijeshi za Iran aina ya F-4 Phantom walirusha ndege kuelekea kwenye eneo la Kinu cha Osirak kilipo.
Vinu hivi vilikiwa vinalindwa na silaha za kudungua ndege aina ya SA-6 moja, Roland missile batteries tatu na anti-aicrafr artillery arobaini.
Ndege ya kivita aina ya F-4 Phantom
Mzinga wa SA-6
Anti-aicraft Artillery
Nimeeleza kwamba Iran ilikuwa na imewekewa vikwazo vya kijeshi na Marekani. Hii ilisababisha washindwe kuweka hata ECP katika ndege zao za F-4 Phantom. ECP (Electronic Countermeasure Pods) ni vifaa ambavyo vinafungwa kwenye ndege za kivita ili viweze kufanya 'jamming' kwenye radar za silaha za adui na kushindwa kung'amua position halisi ya ndege ilipo.
Kwamba ECP inafanya adui akiangalia kwenye radar yake aone 'multiple targets' au labda target inaenda kwa kasi kubwa kuzidi uhalisia. Kwa namna hii inampunguzia adui ufanisi wa kuishambulia ndege inayokuja kwenye anga.
Sasa kwa kuwa F-4 Phantom za Iran hazikuwa na ECP hii iliwabidi marubani kurusha ndege chini chini sana ili kulwepa radar za jeshi la Iraq. Lakini ukirusha ndege chini chini kiasi hiki inaongeza uwezekano wa ndege kudunguliwa na anti-aircraft missiles. Hivyo basi iliwalazimu marubani wa Iran kupeleka ndege kwa kasi kubwa ili wasidunguliwe.
Matokeo yake ni kwamba yale mabomu ambayo waliyadondosha hayakuweza kuleta madhara makubwa kuharibu kinu cha Osirak.
Kwa kifupi, Operation Scorch Sword ilikuwa haijafaulu… mission failed.
Ndipo hapa ambapo Israel waliamua 'kuvua gloves' na kuingia mzigoni wenyewe ili ku-neutralize hatari hii iliyoko mbele yao..Osirak! Uwezekano wa nchi ya Iraq kuwa na silaha za nyuklia.
Na ndipo hapa ambapo Operation Opera ilizaliwa au kama baadhi ya makomando wanavyoiita ndani ya Israel, Operation Babylon.
Baada ya Oparesheni Scorch Sword ya Iran ambayo pia Israel walisaidia sana Iran kijeshi kutofanikiwa, Israel iliweka nia ya kufanya Oparesheni nyingine wao wenyewe.
Ilikuwa tayari imepita miezi tisa tangu kufanyika kwa Opearation Scorch Sword. Na katika muda huu Iraq ilikuwa kwenye vita kali ya kijeshi na majirani zao wa Iran. Kwa hiyo mpango wa nyuklia ulikuwa unaendeahwa kwa haraka na kasi kubwa huku kukiwa na uvumi kwamba Iraq walikuwa wamedhamilia kutengeneza bomu ambalo watalitumua kuwamaliza adui zao wa Iran.
Hii ilikuwa ni habari mbaya pia kwa Israel kwa kuwa kutokana na uadui wao mkali na Iraq kwa miaka mingi walihisi kabisa kwamba silaha hizo za nyuklia zinaweza pia kutumika dhidi yao.
Tayari ilikuwa imepita takribani miezi tisa tangu kufeli kwa Oparesheni Scorch Sword ya jeshi la Iran na kwa mujibu wa taarifa za intelijensia za Israel zilikuwa zinasema kwamba Iraq walikuwa wamebakiza takribani mwezi mmoja tu kufikia lengo la kuunda silaha ya nyuklia.
Ndipo hapa ambapo jeshi la Israel walikuja na Operation Opera na kuipendekeza kwa Waziri Mkuu wa Israel na bila kuchelewa Waziri Mkuu alitoa ruhusa kwa Oparesheni hiyo kufanyika.
Siku ya jumapili, June 7 mwaka 1981… ndege nane za kivita aina ya F-16A zikibeba mabomu mazito aina ya Mark-84 ziliondoka kutoka uwanja wa ndege wa kijeshi wa Etzion Airbase. Chaguo hili la mabomu aina ya Mark-84 lilikuwa ni mujarabu kabisa kutokana na mfumo wa mabomu haya. Haya ni aina ya mabomu ambayo yako kwenye kundi tunaita 'delay-action bomb'. Yenyewe yanalipuka muda kadhaa baada ya kudondoshwa. Yaweza kuwa baada ya sekunde kadhaa au hata baada ya wiki kadhaa kutegea na jinsi limetegeshwa.
Lengo kuu la kuunda mabomu ya namna hii ni kuhakikisha kwamba linafanya uharibifu mkubwa sehemu lengwa. Kwa mfano likidondoshwa juu ya paa la ghorofa, litadondoka na kupenya floor kadhaa ndipo kisa lilipuke. Uzito wake pia unasaidia sana kuhakikisha uharibifu wa kupenya mpaka floor ya mwisho unakuwa wa ufanisi. Kwa mfano mabomu haya ambayo yalibebwa siku hii na ndege hizi za F-16 yalikuwa na uzito kuzidi kilo 1,000 kwa kila bomu.
Lakini pia msafara huu wa F-16 ulisindikizwa na ndege sita aina ya F16A kwa ajili ya kutoa 'support' ya ushambuliaji adui mtambuka kama ikihitajika kufanta hivyo.
Msafara huu wa ndege hizi ziliongozwa na ndege ambayo iliendesha na rubani nguli wa kivita, Ze'ev Raz.
Ndege ya Jeshi la Israel aina ya F-16A Netz 243
Ndege ziliondoka Etzion Airbase majira ya tisa na dakika 55 alhasiri.
Kutoka Etzion Airbase kuelekea Iraq lazima upite juu ya anga la nchi ya Jordan na nchi ya Saudi Arabia.
Ndege zilipopita juu ya anga la Jordan, marubani wa Israel waliongea na waongoza ndege wa Jordan kwa kutumia kiarabu cha lafudhi ya Saudi Arabia. Walijitambulisha kama msafara wa ndege za kijeshi za Saudi Arabia ambao wanafanya 'patrol' na kwa bahati mbaya wamejikuta wekosea njia ya anga na kuingia anga la nchi ya Jordan. Waliomba radhi na kuruhusiwa kupita kwenda Saudi Arabia.
Walipoingia kwenye anga la Saudi Arabia, walibadili 'signal' na 'formations' za mawimbi ya radio na kuanza kutumia radio signals na formations za nchi ya Jordan. Wakajitambulisha kama msafara wa ndege za nchi ya Jordan na wakaruhusiwa kupita.
Ni muda huu sasa baada ya kupita Saudi Arabia na kuingia ghuba ya Aqaba ndipo walipopita juu ya boti ya starehe ya Mfalme Hussein, Mfalme wa Jordan, ambaye alikuwa mapumziko eneo hilo. Kutokana na ndege kuruka chini chini sana kukwepa radar, mfalme Hussein aliweza kuona bendera ya Israel ubavuni mwa ndege na kisha akatoa taarifa kwa serikali yake ya Jordan ili wawasiliane na serikali ya Iraq kwa kuwa alikuwa na hakika kutokana na mwelekeo wa ndege hizo lazima zilikuwa zinakwenda kufanya shambulizi nchini Iraq.
Msafara huu wa ndege ulipoingia kwenye anga la nchi ya Iraq zilijigawa ambapo ndege zile nane aina ya F-16 ziliendelea kwa pamoja huku ndege mbili za F-15 zikijitenga na zile nyingine sita na kuja kukaa karibu na msafara huu wa F-16 kwa ajili ya kutoa 'escort'. Ndege nyingine zile nne aina ya F-15 zilizosalia zilijigawa angani na kutawanyika ili kufanya diversion kama ikitokea wameonwa na rada za jeshi la Iraq lakini pia kwa ajili ya kujiandaa kutoa msaada kwa msafara wa squadron ya F-16 kama ikihitajika.
Msafara uliruka mpaka kufikia mita 30 tu kutoka ardhini ulipofika kwenye jangwa la Iraq ili kukwepa rada.
Ile taarifa ambayo Mfalme Hussein aliitoa kwa serikali yake ili ipelekwe Iraq, ilipelekwa. Bahati mbaya sana huu ulikuwa muda wa 'lunch' na wanajeshi wanaolinda kinu cha Osirak walikuwa wameenda kupata mlo wa mchna. Kwa hiyo hata taarifa ilipofika kwamba wajiandae katika mizinga yao ya kutungua ndege hawakuweza kufanya hivyo kwa wakati.
Msafara ulipokaribia Majengo ya vinu vya nyuklia vya Osirak, ndege zilipanda juu kwa pamoja kwa kasi kubwa mpaka kufikia umbali wa mita 2,100 kutoka ardhini.
Baada ya hapo ndege zilianza kushuka kwa mlalo wa nyuzi 35 na kasi ya kilomita 1,100 kwa saa.
Zilipofika umbali wa wa mita 1,100 kutoka ardhini… ndege zote nane ziliachia bomu moja moja. Sekunde tano baadae zikaachia bomu nyingine moja moja. Kwa hiyo ndani ya sekunde tano tu, mabomu 16 mazito aina ya Mark-84 yaliachiwa kwenye kinu cha Osirak.
Ndege zilirudi juu kwa kasi ya ajabu mpaka umbali mkubwa sana wa kutosha kutoka ardhini na kuanza safari ya kurejea Israel.
Tukio lote hili lolidumu kwa muda wa dakika mbili tu lakini liliacha kinu cha Osirak majivu matupu.
Kiongozi wa marubani wa ndege za F-16 kwa furaha kubwa alitamka maneno ya taurati katika kinasa sauti chake…
"…katika siku hiyo ambayo BWANA aliwatoa Waamori mbele ya wana wa Israeli; akasema mbele ya macho ya Israeli, wewe Jua, simama kimya juu ya Gibeoni;Na wewe Mwezi, simama katika bonde la Aiyaloni."
Oparesheni ilikuwa imefanikiwa kwa asilimia 100. Na hivi ndivyo ambavyo ndoto za Iraq kuwa dola ya nyuklia zilivyokomeshwa.
Imeandaliwa na Habib Anga (The Bold) | RoryaFinestMedia
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena