Header Ads Widget

Responsive Advertisement

MAHUSIANO | Njia Bora za Kumiliki Mali Kwa Wanandoa

Image result for african couple

Changamoto kubwa katika ndoa nyingi si kupata mali bali namna ya kuzimiliki. Japokuwa mchakato wa umiliki unaweza kuathiriwa na jinsi mali husika zilivyopatikana. Lakini, mara nyingi migogoro mingi hujitokeza baada mali kupatikana.

Watu wengi hujiuliza ni mfumo upi unaofaa kiuchumi na kisheria katika kumiliki mali kwa wanandoa. Wengi hujiuliza pia kama mali zilizopatikana kwa juhudi za mume pekee kama mke ana haki ya kuzimiliki au zilizotafutwa na mke kama mume naye ana sehemu ya umiliki.

Kuna maswali mengi. Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inasema mali zote zilizopatikana kabla ya kufunga ndoa huendelea kuwa binafsi hadi wanandoa wenyewe watakapokubaliana kuzifanya za wote wawili.

Ikumbukwe, endapo kutakuwa na ongezeko lolote la thamani katika mali hiyo, hilo linaweza kufanya mali hiyo kuhesabika kuwa ni ya wanandoa japokuwa ilianza kumilikiwa na mwanandoa mmojawapo.

Jambo la msingi na la kuzingatia ni kwamba, japokuwa sheria inatoa mwanya wa kumiliki mali binafsi, lakini, ili kulinda maslahi ya wanandoa wote wawili, inaeleza mali zitakazochumwa kuanzia siku waliyoanza kuishi pamoja zitakuwa za wote wawili bila kujali mchango wa kila mmoja.

Kitendo cha kuishi pamoja kama wanandoa ni mchango tosha unaotambulika kisheria katika upatikanaji na umiliki wa mali hizo. Haijalishi zilinunuliwa kwa jina la nani au hati za umiliki wa mali hizo zimeandikwa jina la nani.

Mchango wa upatikanaji wa mali, sheria inasema sio lazima uwe wa fedha bali unaweza kuwa mawazo, ushirikiano, nguvukazi, usimamizi, mazingira mazuri ya ndoa, huduma za kindoa, utekelezaji wa majukumu ya kifamilia au namna yoyote ile inayomfanya mwanandoa huyo kuwa katika hali itakayomwezesha kupata na kumiliki mali husika.

Mchango wa mwanandoa mmojawapo hauna uhusiano wowote na upatikanaji wa watoto. Watoto wawe wamepatikana au hawajapatikana bado mchango wa mwanandoa upo palepale hivyo ni kosa kisheria kumnyanyasa au kumnyima haki zake za kimsingi za kumiliki au kupata sehemu ya mgao wa mali kwa kigezo kwamba hakupata mtoto.

Ni kosa pia kumnyanyasa au kumnyima haki yake kwa kigezo kwamba hajachangia chochote katika ununuzi wa mali yoyote iliyopatikana kipindi cha kuishi pamoja kwa wanandoa wawili.

Ifahamike, kwa kuwa mali ni za wanandoa wawili, mmojawapo hawezi kuuza, kuweka rehani, kummilikisha mtoto au mtu mwingine yeyote pasipo ridhaa ya mwenzake. Chochote kitakachofanyika pasipo ridhaa ya mwenzi wako kuhusiana na mali hizo kitakuwa ni batili kisheria.

Sheria ya ardhi, sheria ya mikopo ya dhamana ya ardhi na nyinginezo inaagiza kuwepo kwa ridhaa ya wanandoa kabla ya mali husika kuwekwa rehani kwa ajili ya kukopa. Ridhaa hii hupaswa kupatikana bila kujali hati ya umiliki wa mali hiyo inasoma jina gani.

Hata hivyo, kuondoa migogoro kwa mke au mume na wanandugu baada ya mmojawapo kufariki, ni vyema umiliki wa kampuni, biashara, magari, nyumba, viwanja, hisa, akaunti za benki na rasilimali nyingine ukawa wa pamoja. Majina ya wanandoa wote wawili yaonekane katika hati za umiliki wa mali hizo kuanzia kwenye ununuzi.

Mnaweza kuamua kufungua kampuni ambayo wote mtakuwa wakurugenzi kisha mali zenu kuzisajili chini ya umiliki wa kampuni hiyo. Hiyo itasaidia kuondoa usumbufu wa mirathi kwa kuwa yule atakayebaki ndiye atakayekuwa mmiliki halali na itakuwa rahisi kwa watoto au vizazi vijavyo kuendelea na umiliki wa mali hizo chini ya taasisi hiyo pasipo usumbufu wowote.

Inafaa mke amshirikishe mume na mume vivyo hivyo kwenye masuala ya mali bila kufanya siri yoyote.


Chanzo || JamiiForum.com

Post a Comment

0 Comments