Dar es Salaam. Baadhi ya wanawake
wa Kitanzania waliofungwa katika magereza ya China na Hong Kong,
walishika ujauzito kama moja ya mbinu ya kupitisha dawa za kulevya bila
kugundulika kwenye viwanja vya ndege na mipaka mingine ya kimataifa.
Mwananchi limebaini.
Watanzania
wanne walio katika magereza ya China na Hong Kong walijifungua watoto
kwa nyakati tofauti wakiwa wanatumikia vifungo na wamekiri kuwa walibeba
ujauzito kama mbinu ya kupitisha dawa hizo bila kukaguliwa.
Watoto
wanaozaliwa magereza baada ya kufikisha mwaka mmoja hupelekwa katika
vituo vya watoto yatima na kusomeshwa na Serikali ya China hadi pale
wazazi wao watakapomaliza adhabu.
Imebainika kuwa watoto
wawili wapo katika vituo hivyo, mmoja tayari yupo Tanzania baada ya bibi
yake kumrejesha na mwingine bado yupo gerezani na mama yake. Wanawake
hao ambao wote wana umri wa kati ya miaka 20 na 30 walieleza masikitiko
yao jinsi ambavyo wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya
wanavyowarubuni ili kubeba dawa hizo kwa ahadi za kuwapa fedha nyingi.
“Tunapata
mimba makusudi kwa sababu tulijua kuwa katika viwanja vya ndege vingi
wajawazito hawakaguliwi hasa wakiwa na mimba kwa hiyo tungebeba unga na
kuupeleka China, halafu baadaye tungerudi nchini na kutoa mimba au
tukiamua tunajifungua,” alisema mmoja wa wafungwa hao.
Hata
hivyo, mbinu hiyo ilifanikiwa katika Uwanja wa Ndege Kimataifa wa Julius
Nyerere (JNIA), lakini haikufua dafu katika viwanja vya ndege vya
China, Hong Kong, Macau na Guang Zhou.
Mkurugenzi wa Makosa
ya Jinai (DCI), Kamishna Diwani Athuman alisema hana taarifa za
Watanzania hao lakini ofisi yake inafanya taratibu za kuwasiliana na
China ili kujua hali za wanawake hao.
Mkurugenzi wa JNIA,
Moses Malaki alisema kwa kawaida kila mtu hukaguliwa kwa uangalifu bila
kujali mjamzito au la. Akielezea namna wanavyopimwa, Malaki alisema
kwanza kila msafiri hupimwa kwa mashine ya kawaida ambayo hubaini uwepo
wa kifaa chochote kisichotakiwa mwilini kwa mfano chuma kama hereni,
bangili, mikanda lakini si ndani ya tumbo.
“Iwapo mashine ya
awali itatoa mlio hata baada ya msafiri kutoa vitu vya chuma, basi
atatakiwa kwenda katika chumba maalumu cha ukaguzi wa mikono,” alisema.
Kamanda
wa kitengo cha Polisi cha Dawa za Kulevya, (SACP), Godfrey Nzowa
alisema wapo wanawake kadhaa raia wa Zambia, Zimbabwe, Nigeria, Afrika
Kusini na Malawi ambao wamefungwa katika magereza ya Tanzania kwa
kusafirisha dawa za kulevya wakitumia mbinu hiyo ya ubebaji wa mimba.
Alisema
mbinu hizo zinatumiwa na wanawake kwa sababu wajawazito hawakaguliwi
kwa mashine za x-ray na kwamba wengi walikamatwa kutokana na taarifa za
kikachero.
“Hata magereza ya hapa tunao na wamejifungua
watoto wakiwa gerezani, lakini wajue kabisa kuwa watakwepa mashine
lakini taarifa zinatusaidia na ndiyo maana nasema taarifa ni nguvu,”
alisema.
Pamoja na kukamatwa kwa raia wa kigeni wanaotumia
mbinu hiyo, Kamishna Nzowa hakuwa na taarifa za Watanzania waliokamatwa
nje ya nchi kwa kutumia mbinu hiyo.
Septemba mwaka jana,
raia wa Canada, Tabitha Ritchie alikamatwa kwenye Uwanja wa Ndege wa
Columbia kwa kubeba dawa za kulevya kwenye mimba ya bandia, mbinu ambayo
ilibainika baada ya kuhojiwa na maofisa wa uhamiaji kuhusu umri wa
mimba yake na walipomgusa tumboni walibaini kuwa tumbo lilikuwa baridi
na gumu.
Askari mmoja wa Kitengo cha Dawa za Kulevya wa
JNIA, (jina linahifadhiwa), alieleza wazi kuwa hakuna mashine ya kujua
mtu aliyemeza dawa hizo zaidi ya kuhisi tu kwa mbinu za kiaskari.
Alisema
mara nyingi watu waliomeza dawa hizo hukamatwa kwa kuhisiwa na baada ya
kupekuliwa huamriwa kuruka kichura au kujisaidia ili kujua iwapo wana
‘mzigo’ tumboni.
Hata hivyo, askari huyo alisema kwa kawaida
wajawazito hawawezi kurushwa kichura au kulazimishwa wajisaidie
kutokana na hali zao.
Miongoni mwa wanawake waliobeba mimba
kwa ajili ya kubeba dawa za kulevya na wasichana maarufu nchini, mmoja
wao mtoto wake sasa analelewa katika kituo cha watoto yatima China.
Baada
ya kupata taarifa hizo, Mwananchi ilizitafuta familia za wafungwa hao
ambazo hazikuwa na taarifa kuwa na ndugu zao walikuwa na ujauzito
walipokuwa wakisafiri.
Baadhi ya waliohojiwa walisema walipata taarifa za ndugu zao kuwa na watoto wachanga lakini hawakuwa na habari za ujauzito.
“Hata
hivyo, ninamshukuru Mungu kwa kuwa amepata mtoto na anaendelea vizuri,
kutokana na uwezo wetu kuwa mdogo siwezi kwenda kumchukua mjukuu wangu
huko Hong Kong, mwache akae kituoni hadi mama yake atakapoachiwa,”
alisema mama wa mmoja wa wafungwa hao.MWANANCHI
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena