1.1. Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania ni taasisi ya Serikali yenye dhamana ya kusimamia shughuli za
Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta hapa nchini. Kuwepo kwa Sheria
ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya 2010 na Kanuni za EPOCA
(CEIR) za mwaka 2011 zimewezesha kutekelezwa kwa mfumo wa rajisi ya
namba za utambulisho wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi.
1.2. Mfumo huu wa
kielektroniki ulizinduliwa rasmi tarehe 17 Desemba 2015 na unahifadhi
kumbukumbu za namba tambulishi za vifaa vya mawasiliano vya mkononi (IMEI) kwa lengo la kufuatilia namba
tambulishi za vifaa vinavyoibiwa, kuharibika, kupotea au ambavyo havikidhi
viwango (bandia) vya matumizi katika soko la mawasiliano. Namba tambulishi za vifaa
vyote vya mawasiliano vya mkononi ambavyo vimeibiwa, vimeharibika, kupotea au
visivyokidhi viwango vya matumizi katika soko la mawasiliano havitaruhusiwa
kuunganishwa kwenye mitandao ya watoa huduma ifikapo kesho tarehe 16 Juni 2016.
1.3. Kipindi
cha mpito cha kuelimisha umma pamoja na zoezi la wateja kuhakiki simu walizo
nazo au wakati wanataka kununua simu mpya lilianza mwezi Desemba 2015 wakati
mfumo ulipozinduliwa na litamalizika kesho tarehe 16 Juni 2016. Hata
hivyo, elimu kwa umma kuhusu simu bandia imekuwa ikitolewa nchini tangu mwezi
Novemba 2011 baada ya Kanuni za CEIR kutoka, kufuatia kupitishwa na Bunge
Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta tarehe 20 Juni 2010 ikielekeza
kuwekwa kwa mfumo wa namba za utambulisho wa vifaa vya Mawasiliano vya
kiganjani.
2.0 KAZI ZILIZOFANYIKA TANGU KUZINDULIWA KWA
MFUMO
2.1 Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania imeendelea kusimamia kwa karibu makampuni ya simu hapa nchini katika
uendeshaji wa kila siku wa mfumo wa rajisi ya namba za utambulisho wa vifaa vya
mawasiliano vya mkononi. Hii imesaidia pamoja na mambo mengine kupata taarifa za namba tambulishi (IMEI) na
kuzifanyia uchambuzi wa kina ili kupata mwelekeo halisi kabla ya kipindi cha mpito
kuisha hapo tarehe 16 Juni, 2016.
2.2 Mamlaka ya Mawasiliano iliendelea pia na
kampeni za kutoa elimu kwa umma kuhusu jinsi ya kuhakiki namba tambulishi
(IMEI) za vifaa vya mkononi (mobile devices). Katika kampeni hizo wananchi walipata
uelewa wa kutambua uhalisia wa simu zao ikiwa ni pamoja na mambo muhimu ya
kuzingatia wakati wa kununua simu mpya. Makampuni yote ya simu hapa nchini kwa
nyakati tofauti wameshiriki pia katika kuelimisha umma, ikiwa ni pamoja na
kuwapelekea ujumbe mahususi moja kwa moja kwa watumiaji wote wa simu za mkononi.
Hali kadhalika Shirika la Viwango Tanzania na Tume ya Ushindani nchini,
wameshiriki moja kwa moja katika kutoa elimu kwa umma sambamba na Mamlaka ya
Mawasiliano.
2.3 Kipindi cha kuanzia Desemba 2015 mpaka mwezi
Mei 2016 Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ilitoa elimu kwa umma katika mikoa ya
Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Mbeya, Rukwa, Ruvuma, Iringa, Dodoma,
Singida, Tabora, Mwanza, Shinyanga, Geita, Simiyu, Mara na Kagera. Pia elimu
kwa umma ilitolewa Zanzibar. Mamlaka imefanya pia elimu kwa umma katika miji
ya, Morogoro, Pwani, Lindi na Mtwara wiki iliyopita pamoja na wiki hii. Aidha
kesho ambayo ndio siku ya ukomo wa matumizi ya simu bandia nchini, kutakua na
mkutano wa wafanya biashara wa simu wa mkoa wa Dar es Salaam. Mkutano huo
utawahusisha pia mafundi wa simu, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa. Pamoja
na mikutano ya hadhara na mikutano ya barabarani (road shows), elimu imetolewa
kwa wauzaji wa simu, Mafundi wa Simu na Maafisa Biashara pamoja na Kamati za
Ulinzi na Usalama za maeneo husika.
3.0
UCHAMBUZI WA NAMBA TAMBULISHI (IMEI)
Wakati mfumo wa rajisi ya namba za utambulisho wa
vifaa vya mawasiliano vya mkononi unazinduliwa mwezi Desemba 2015, idadi ya
namba tambulishi ambazo zilikuwa hazina viwango (bandia) zilikuwa sawa na 4% na
zile ambazo zilikuwa zimenakiliwa (duplicates) zilikuwa ni sawa na 30%. Hii
ikiwa na maana 66% ni sio simu bandia. Uchambuzi huu haukuhusisha taarifa za
makampuni ya Viettel na Smile.
Kielelezo
1: Uchambuzi wa takwimu za namba tambulishi (IMEI) za Disemba, 2015
Uchambuzi wa
mwezi Februari 2016 ulionyesha idadi ya namba tambulishi ambazo zilikuwa hazina
viwango zilikuwa sawa na 3%, vilevile idadi ya namba tambulishi ambazo
zimenakiliwa zilikuwa sawa na 18%. Simu halisi zilikuwa sawa na 79%.
Kielelezo 2. Uchambuzi
wa takwimu za namba tambulishi (IMEI) February 2016
Uchambuzi wa
mwezi Machi 2016 ulionyesha idadi ya namba tambulishi ambazo zilikuwa hazina
viwango zilikuwa sawa na 4%, na idadi ya namba tambulishi ambazo zimenakiliwa
zilikuwa sawa na 13%. 83% zikiwa simu halisi. Uchambuzi huu unahusisha taarifa
za makampuni yote ya simu nchini.
Kielelezo
3: Uchambuzi wa takwimu za namba tambulishi (IMEI) za Machi, 2016
Uchambuzi wa
mwezi Aprili 2016 unaonyesha hakuna mabadiliko yoyote ya idadi ya namba
tambulishi ambazo zilikuwa hazina viwango (invalid) hivyo kubakia 4%, na idadi
ya namba tambulishi ambazo zimenakiliwa ziliongezeka kutoka 13% na kufikia 14%.
Vilevile idadi ya namba tambulishi za simu halisia ilipungua kutoka 83% mpaka
82% kama ilivyoonyeshwa katika kielelezo kifuatacho.
Kielelezo
4: Uchambuzi wa takwimu za namba tambulishi (IMEI) za Aprili, 2016
Matokeo ya
uchambuzi wa mwezi Aprili, 2016 umeonyesha namba tambulishi ambazo zilikua
zimenakiliwa kuongezeka na kuleta taswira kuwa kuna uwezekano mkubwa kwa wauzaji
wa simu wasio waaminifu kupunguza bei za simu zao zenye namba tambulishi
zilizonakiliwa na kuwafanya watumiaji wa simu katika maeneo husika ambayo elimu
kwa umma ilikua bado haijawafikia kushawishika kununua simu hizo. Matokeo haya yalitoa msukumo kwa Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania pamoja na wadau wote kuongeza nguvu zaidi kuelimisha
wananchi katika maeneo yaliyobakia kuhusu umuhimu wa kuhakiki simu zao ikiwa ni
pamoja na kuelewa zaidi utaratibu wa kufuata wakati mtu atakapo hitaji kununua
simu mpya.
Kielelezo
5: Uchambuzi wa takwimu za namba tambulishi (IMEI) za Mei, 2016
Uchambuzi wa
mwezi Mei, 2016 ulionyesha idadi ya namba tambulishi ambazo zilikuwa hazina
viwango zilikuwa sawa na 3%, na idadi ya namba tambulishi ambazo zimenakiliwa
zilikuwa sawa na 2% ambapo 95% zikiwa simu halisi. Uchambuzi huu unahusisha
taarifa za makampuni yote ya simu nchini.
Matokeo haya mazuri
yanaonyesha matokeo ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania, Makampuni ya simu hapa nchini pamoja na wadau wengine
katika kuelimisha umma juu
ya kuhakiki uhalisia wa simu walizo nazo ikiwa ni pamoja na mambo muhimu ya
kuzingatia wakati wa kununua simu mpya.
Kielelezo 6: Uchambuzi wa takwimu za namba
tambulishi (IMEI) za Juni, 2016
Uchambuzi uliofanywa
tarehe 14 Juni 2016 unaonyesha mabadiliko chanya ya idadi ya namba tambulishi
ambazo zilikuwa hazina viwango (invalid) kupungua kutoka 3% hadi kufikia 2.96%,
na idadi ya namba tambulishi ambazo zimenakiliwa zikipungua kutoka 2% hadi kufikia
0.09%. Vilevile idadi ya namba tambulishi za simu halisia zimeongezeka kutoka 85%
mpaka 96.95% kama ilivyoonyeshwa katika kielelezo 6 hapo juu.
Matokea haya yanaonyesha
mwitikio mzuri wa wananchi juu ya uelewa wao katika suala zima la uzimaji wa
simu ambazo hazikidhi viwango. Matokeo hayo yanatoa picha nzuri hasa
tunapoelekea kuhitimisha zoezi la uzimaji wa simu bandia kesho tarehe 16 Juni
2016.
4.0 CHANGAMOTO
Pamoja na
jitihada mbalimbali zilizofanywa na Mamlaka pamoja na wadau wengine bado kuna
changamoto ambazo zinahitajika kutatuliwa. Changamoto hizo ni pamoja na:
(i) Uaminifu mdogo kwa baadhi waauzaji wa simu kwa kutoa
punguzo kwa wananchi ili kuwashawishi kuzinunua simu bandia kwa bei nafuu;
(ii) Gharama zinazohitajika katika kuwafikia wananchi na
kuelimisha ili waweze kuelewa zaidi juu ya mpango mzima wa kuhakiki simu zao;
na
(iii) Uelewa mdogo wa baadhi ya wananchi katika kuitikia wito
wa kuhakiki simu zao katika kipindi cha mpito.
5.0 HITIMISHO
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
inaendelea kumbusha watanzania wote kuwa ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha
kuwa simu yake ni halisi na sio bandia kwani kuanzia kesho, hakuna simu bandia
itakayoweza kufanya kazi nchini. Vilevile Mamlaka inawakumbusha wauzaji wa
vifaa vya mawasiliano vya mkononi kutambua kuwa ni kosa kubadilisha namba
tambulishi za vifaa vya simu za mkononi (mobile devices) kwani adhabu yake ni
kifungo kisichozidi miaka kumi (10) au faini isiyopungua TZS millioni 30 au
vyote kwa pamoja.
Mamlaka inatoa wito kwa
wale wote wote wanaofanya biashara za kuingingiza simu hapa nchini kutoka nje wahakikishe
kuwa simu wanazoleta zinakidhi viwango, zimehakikiwa kwa mujibu wa Shirika la
Viwango Tanzania. Aidha Mamlaka inawakumbusha kwa mara nyingine kuwa wanapaswa
kuwa na leseni ya Mamlaka ya Mawasiliano kwa mujibu wa Sheria. Hii pia ni kwa
mafundi wote wa simu nchini, wanatakiwa kuanza mchakato wa kupata leseni ya
kutengeneza simu, ikiwa ni pamoja na kuweka utaratibu wa kuwaorodhesha
wanaoleta simu zao kutengenezwa ili kuepuka kuwa sehemu ya mtandao wa wizi wa
simu.
Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania inayapongeza makampuni ya simu kwa ushirikiano mzuri wanaondelea
kuuonesha katika kutekeleza agizo hili la Serikali kupitia Mamlaka. Hali
kadhalika, jitihada zao za kushiriki elimu kwa umma kwa wateja wao pamoja na
kuwapatia simu wateja waliokuwa wanatumia simu bandia, kumepelekea agizo hili
kufanikiwa kwa kiwango cha hali ya juu. Mafanikio ya jambo hili, kwa kiasi
kikubwa yametokana na ushirikiano wa wadau mbalimbali wa Mawasiliano, wakiwemo
jeshi la Polisi, Tume ya Ushindani pamoja na Shirika la Viwango Tanzania.
Mhandisi James
Kilaba
KAIMU MKURUGENZI
MKUU
15 Juni,
2016
Maelezo ya
ziada kwa Wahariri
FAIDA ZA MFUMO WA RAJISI YA NAMBA
TAMBULISHI
Mfumo huu wa rajisi una faida zifuatazo:
- Kuthibiti wizi wa simu. Iwapo mtu atapoteza au ameibiwa simu ya kiganjani na akatoa taarifa kwa mtoa huduma, simu hiyo itafungiwa isiweze kutumika kwenye mtandao mwingine wowote wa simu za kiganjani. Mteja anaponunua simu ni lazima adai risiti halali na halisi na pia garantiii ya miezi 12. Mteja anatakiwa aihifadhi risiti hiyo angalau kwa miezi mitatu. Baada ya hapo, iwapo simu imekuwa inatumika, taarifa za matumizi zinaweza kutumika kama uthibitisho mbadala wa milki ya simu husika.
- Kuhimiza utii wa sheria: Kifungu cha 128 cha EPOCA kinamtaka mtumiaji wa simu kutoa taarifa ya kupotea au kuibiwa kwa simu au laini ya simu. Kifungu cha 134 kinayataka makampuni ya simu kutokutoa huduma kwa simu ambayo imefungiwa kama ilivyoelezwa hapo juu. Mara tu mteja anapopoteza simu yake ya kiganjani anatakiwa kutoa taarifa kwa kituo cha Polisi cha karibu ambapo atapewa namba ya kumbukumbu ya taarifa ya tukio, maarufu kama RB. Anatakiwa aende kwa mtoa huduma kutoa taarifa ya tukio akiwa na hiyo RB na uthibitisho wa umilki wa simu iliyopotea (risiti aliyopewa wakati wa kununua iwapo itakuwepo).
Mtoa huduma kwanza atahakiki umilki wa simu iliyopotea
au kuibiwa na atampatia mteja namba ya kumbukumbu kwamba simu hiyo imefungiwa
isutumike kwenye mitandao ya simu na hatimaye ataifungia simu hiyo ndani ya saa
24.
- Kujenga misingi ya matumizi ya simu halisi, zisizo bandia. Mtumiaji ataweza kutambua iwapo simu aliyo nayo inakidhi viwango, ni halisi na sio bandia.
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena