Field Marshal John Okello |
Mwalimu alipoelezwa juu ya maasi hayo, alilipuka kwa hasira na ghadhabu kubwa papo hapo; akataka kwenda yeye mwenyewe kukutana na Waasi hao ili wamweleze sababu za kitendo hicho cha aibu. Mama Maria Nyerere, kwa machozi na kwa kupiga magoti, alimsihi mumewe asitoke kwenda kukutana na watu wenye silaha, lakini hakufanikiwa kumgeuza nia.
Ndipo watu wa Usalama walipojenga hoja nzito kumzuia, na hoja hiyo ikamwingia; akakubali kuteremka dari ya chini, kisha yeye, Kawawa na Mama Maria Nyerere, wakatorokea mahali kusikojulikana. Wakati huo, tayari waasi walikuwa kwenye lango kuu la Ikulu wakimtafuta.
Bado ni kitendawili kuhusu mahali Mwalimu na wenzake walikokuwa wamejificha. Wapo wanaodai alijificha Misheni au Kanisani; wapo pia wanaosema alijificha kwenye nyumba ya Balozi mmojawapo Jijini.
Wengine wanasema alijificha kwenye kibanda kidogo sana (Kigamboni?) karibu na Pwani; na baadhi wanadai alikwenda Arusha au Nairobi. Lakini wapo pia wanaosema alijificha kwenye meli. Wala haielezwi kama John Okello aliondokaje Ikulu usiku huo baada ya mazungumzo au kama maasi yalimkuta Ikulu usiku huo.
Kufikia saa 9:00 alfajiri, waasi walikuwa wamekamata kambi ya Colito, kisha wakajigawa vikundi vitatu na kuingia mjini. Kikundi kimoja kilibakia kulinda kambi ya Colito, kikundi cha pili, kikiongozwa na Sajini Francis Higo Ilogi, ndicho kilichokwenda Ikulu kumtafuta Rais; wakati kikundi cha tatu kililinda barabara kuu zote mjini.
Askari waliofanya mapinduzi wakiwa chini ya ukaguzi |
Ni ujasiri gani huo; ni kujiamini vipi kwa Kambona, kwamba bila ulinzi wala woga, tena akiwa amepanda gari la Mkuu wa Polisi tu, aliweza kukubali kuandamana na askari wenye silaha, na hasira kali, kwenda Colito Barracks?
Mwl Nyerere, Oscar Kambona na Viongozi wengine |
Huko Colito Barracks, walimweka Kambona “kiti moto”, wakimtaka aamue papo hapo, pamoja na mambo mengine, kuondolewa mara moja kwa Maafisa wa Kiingereza Jeshini, na nafasi zao zishikwe na Wazalendo. Walitaka pia mishahara iongezwe, kutoka 105/= hadi 260/= kwa mwezi.
Bila kuonyesha kwamba ameyakubali au kuyakataa madai yao, Kambona aliomba wateue wawakilishi wachache ili wafuatane naye hadi Ikulu kwa mashauriano na Mwalimu Nyerere. Ndipo Kiongozi wa waasi, Francis Higo Ilogi, alipokataa na kusema, “Tunataka kila kitu leo hii”, Yowe zikasikika, “Apigwe risasi, apigwe” (Kambona) huyo!”. Pengine kwa kuingiwa na hofu, kwamba lolote lingeweza kumtokea, Kambona akauliza: “Mnataka nani awaongoze?” Lilitajwa jina la Alex Nyirenda; lakini likakataliwa kwamba alikuwa na majivuno. Akatajwa Luteni Elisha Kavana, akapitishwa kwa kauli moja na kuvishwa kofia ya Brigedia Douglas.
Kambona alikataa kutia sahihi makubaliano, kwa madai kwamba mpaka ashauriane kwanza na Rais. Ndipo kikundi chote cha Ilogi kikafuatana naye kwenda Ikulu.
Walipofika huko, askari hao walijipanga barabara yote iingiayo Ikulu, lakini Sgt Ilogi aliwakataza wasiingie ndani, wakamruhusu Kambona pekee. Wakati huo Nyerere alikuwa ametoroka zaidi ya saa mbili zilizopita.
Baada ya mashauriano kwa muda na wasaidizi wa Rais pamoja na mama mzazi wa Mwalimu, Kambona alitoka nje na kuwatangazia waasi hao kuwa Rais ameyakubali madai yao. Lakini askari hao wakapiga kelele “mwongo huyo! Rais hayumo ndani; mpige risasi, mwongo huyo!” Hata hivyo, waliondoka wameridhika, wakarejea kambini siku hiyo. Hima, Kambona aliwaondoa maafisa wa Kiingereza na kuwasafirisha kwao kupitia Nairobi.
Akiwatangazia wananchi kupitia Redio “Tanganyika Broadcasting Corporation” Kambona alisema: “Huyu ni Waziri wenu wa Mambo ya Nje na Ulinzi; Serikali ingalipo… Kumekuwa na kutoelewana baina ya askari Waafrika na maafisa wa Kiingereza katika Jeshi. Baada ya kuingilia kati shauri hili, sasa askari wamerudi kambini”. Hata hivyo, hakusema lolote juu ya Nyerere, wala mahali alikokuwa.
Je, ni kweli mambo yalikuwa yamekwisha? Kwa nini Nyerere hakutokea hadi siku mbili baada ya askari kurejea kambini? Kwa nini askari hao waliasi tena siku nne baadaye na Nyerere kulazimika kuita majeshi ya Uingereza kuja kuzima maasi
Mwalimu alijitokeza ghafla siku mbili baadaye, akashika madaraka tena. Hata hivyo, siku nne baadaye, askari hao waliasi tena. Kwa nini? Sasa tuendelee kufuatilia na tutapata majibu.
Siku ya pili, baada ya kurejea kambini, askari waasi walionekana kufurahi kuona maafisa wa Kiingereza wakiondoka, kama walivyoahidiwa na Kambona. Lakini mtu mmoja kati yao hakuwa na furaha kama wengine: naye alikuwa Sajini Francis Higo Ilogi.
Wakati wa mazishi ya askari wawili siku hiyo, waliouawa mtaani na Mwarabu mmoja wakati wa maasi, Sajini Ilogi aliacha kukwepa kuzumgumza na Oscar Kambona, wala kumtazama usoni. Je, ni kwa sababu Kambona hakuweza kutekeleza yote aliyoahidi? Je, ni kwa sababu yeye hakupandishwa cheo baada ya kuongoza maasi?
Siku hiyo ilipokelewa taarifa kwamba, Kikosi cha Pili cha Jeshi kilichokuwa Tabora nacho kilikuwa kimeasi, baada ya kupata habari kwamba wenzao wa Collito walikuwa wameasi.
Inawezekana, ama walikuwa hawajapata taarifa kwamba wenzao wa kambi ya Colito walikuwa wamerejea kambini; au walifahamu, lakini wakataka nao watekelezewe mambo kadhaa kwenye Kikosi chao.
Wakati Kikosi cha Tabora kikiendelea na maasi, ilipokelewa hapo Tabora, simu ya maandishi (telegraph) kutoka kwa Kambona, kwamba alikuwa amemteua Kapteni Mirisho Sam Hagai Sarakikya, kuwa Mkuu wa Kikosi cha Tabora. Wakati huo Sarakikya na maafisa wengine walikuwa wamekamatwa na kuwekwa mahabusu na askari walioasi hapo Tabora.
Sarakikya akatolewa mahabusu, akaomba simu hiyo isomwe kwa sauti; kisha akatoa amri wasimame “Mguu sawa”, wafungue beneti na kutoa risasi. Nao wakamtii. Usiku huo, Sarakikya alifanya mipango ya kuwasafirisha maafisa wa Kiingereza kutoka Tabora kwenda Dar es Salaam na hatimaye makwao.
Tukio la Januari 21, na lile la Tabora pamoja na hali ya hatari ilivyokuwa huko Kenya, Uganda na Zanzibar, lilifanya Serikali ya Uingereza ichukue tahadhari ya ziada kwa kupeleka askari 2,000 zaidi ukanda wa Afrika Mashariki. Kwa hiyo, manowari iliyoitwa Rhy, ikawa imetia nanga hima Pwani ya Dar es Salaam, na nyingine Centaur; iliyobeba ndege, iliwasili na askari 600.
Siku ya tatu baada ya maasi ya kikosi cha kwanza, Jumatano, Januari 23 asubuhi, ghafla Nyerere akatokea hadharani amepanda gari la wazi akiwa na Mama Nyerere na Waziri wa Mambo ya Ndani, Job Lusinde, akatembelea kila sehemu ya mji iliyoathiriwa na maasi.
Alhamis ya Januari 24, ilikuwa shwari; lakini Ijumaa, Januari 25, mazungumzo kati ya Serikali na waasi yalionekana kuanza kuvunjika, wakaasi tena. Ni nani alikuwa kiongozi wa maasi haya awamu ya pili? Sajini Higo Ilogi tena?
Tofauti na maasi ya Januari 21, ambayo hayakushirikisha wanasiasa, wala kugubikwa na hisia au shabaha ya kisiasa, maasi haya mapya yaliingiliwa na wapiga filimbi wa kisiasa.
Taarifa za kiusalama zilionyesha kwamba, viongozi wa vyama vya wafanyakazi, kupitia Chama Kikuu (Shirikisho) cha Wafanyakazi (TFL), walikuwa wakikutana kwa siri na askari walioasi kwenye kambi ya Colito; na kwamba vyama hivyo vilikuwa vimeandaa mgomo nchi nzima mwishoni mwa wiki kuungana na askari hao.
Maasi haya ya pili yaliweza kuambukiza majeshi ya Kenya na Uganda, nayo yakaasi vivyo hivyo, siku hiyo hiyo, wakati huo huo, na kwa mtindo huo huo. Marais Kenyatta na Obote walizisoma alama za nyakati ukutani; nao wakajiandaa kuita Jeshi la Uingereza kuzima maasi. Nyerere hakutaka; hakuamini kwamba Jeshi lake mwenyewe lingeweza kumhujumu, yeye na Serikali yake.
Alianza kuhisi hatari mbele pale maofisa usalama walipomuonesha orodha ya mawaziri wanaotarajiwa iwapo Serikali yake ingepinduliwa, iliyoandaliwa na waasi
Mmoja wa watu wake wa karibu alikwenda mbali zaidi kumwambia kwamba, alikuwa ameombwa na waasi akubali kuwa Makamu wa Rais baada ya Mapinduzi. Mwalimu akalowa; akayaamini maneno hayo, kwamba Serikali yake ilikuwa hatarini.
Ndipo, yapata saa 11:30 jioni siku hiyo, Mwalimu akamwita Ikulu Naibu Balozi wa Uingereza, Bwana F. Stephen Mills; akamwomba msaada wa Kijeshi wa nchi yake naye Mills, bila kuchelewa, akapeleka taarifa London na kujibiwa kwamba maombi ya Nyerere yalikuwa yamekubaliwa bila masharti yoyote.
Naye Oscar Kambona akaenda mbio kwenye Ubalozi wa Uingereza, kumtafuta Brigedia Douglas ambaye alikuwa amejificha humo kwa wiki nzima, kumwomba msaada wa kuratibu mipango. Usiku wa siku hiyo, Douglas na ofisa mwingine, walinyatia hadi kwenye manowari Centaur iliyokuwa imefichwa Pwani.
Mwl Nyerere na Samora Matchel wa Msumbiji |
Kutoka umbali wa mita 20 hivi, na kwa ujasiri mkubwa, Douglas akatangaza kwa kipaza sauti, kwamba alikuwa ameshika madaraka yake tena; akatoa amri askari wote watoke nje kambini “mikono juu” na kukaa chini barabarani.
Baada ya dakika 10 bila kuona kitu, Brigedia Douglas akaanza kuhesabu, “moja, mbili….. kumi”, askari wa Kiingereza wakafyatua roketi hadi kambini. Waasi wakaanza kujisalimisha.
Dakika 10 zingine zilizofuata askari 150 walijisalimisha, na wengine 150 baada ya saa moja. Kufikia saa 1:30 asubuhi, wote walikuwa wamesalimu amri; maasi yakawa yamezimwa katika zoezi ambalo askari walioasi, watano waliuawa na wengine watano kujeruhiwa. Hakuna askari wa Kiingereza kati ya 60 walioongoza mapambano, aliyedhurika. Na kwa juma lote la maasi, raia wasiopungua 17 waliuawa.
Wakati wanajeshi wa Jeshi la Uingereza wakiwadhibiti askari waasi wa Tanganyika, huko Uganda na Kenya nako, Jeshi lilikuwa linachukua hatua kama hiyo, muda huo huo saa hiyo hiyo na kwa staili hiyo hiyo kwa askari walioasi.
Kwa wenzetu uasi ulifanyika Jinja (Uganda), na katika kikosi cha 11 cha Bark-Lanet (Kenya). Hayo ndo maeneo yaliyojihusisha na maasai kwa Uganda na Kenya.
Haielezwi ni jinsi gani Sajini Higo Ilogi aliweza kuponyoka, akaonekana mjini asubuhi hiyo kwenye jumba la Simu za Nje za Kimataifa (Extelcoms), akituma simu ya mandishi kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) U Thant, kuomba msaada. Simu hiyo ilisomeka hivi: “Majeshi ya Tanganyika yametekwa na askari wasiojulikana saidia haraka kuleta Majeshi ya Umoja wa Mataifa LUTENI KANALI ILOGI, MKUU WA JESHI”. Turejee kwenye swali letu la msingi: Nani alichochea maasi ya jeshi letu mwaka 1964? Oscar Kambona? John Okello?
Kambona alikuwa Waziri mwenye dhamana ya ulinzi wakati huo, ambapo Jeshi lilikuwa chini ya wizara yake. Kwa sababu hii, kushiriki kwake katika kutuliza maasi ya awamu ya kwanza, hakuwezi kuchukuliwa kwamba alikuwa na hisa au kwamba alijua mpango huo wa maasi hayo.
Ni ujasiri wake tu uliomtuma kukabiliana na hali hiyo. Kama kweli angekuwa na nia mbaya kwa Serikali; na kwa kuzingatia pia jinsi alivyodhibiti hali hadi askari wakamkubali, angeshindwaje kupindua nchi ambayo ilikuwa mikononi mwa Jeshi kwa siku mbili mfululizo kama alikuwa na nia hiyo?
Je, ni Field Marshal John Okello? Hapa tena jibu ni HAPANA. Yeye hakuwa na muda huo, kwa sababu kwa kipindi chote tangu Mapinduzi ya Zanzibar, alikuwa katika hati hati za kulinda na kuimarisha utawala wake visiwani kutokana na tishio la kuenguliwa na wahasimu wake ambao alidai hawakushiriki katika Mapinduzi. Okello aliongoza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa miezi miwili mfulilizo kabla ya kuenguliwa na Karume kwa kushirikiana na Mwalimu Nyerere.
Wala haishangazi kwamba, maasi ya askari hawa yaliweza kuambukizwa kwa wenzao wa Kenya na Uganda, ikizingatiwa kuwa majeshi ya nchi hizi tatu yamezaliwa na Jeshi la Wakoloni wa Kiingereza waliotawala nchi hizo. Kwa hiyo, kwa kipindi hicho, na kwa mazingira ya kazi ya wakati huo, malalamiko yao yalifanana kuwafanya wadai haki zao kwa njia na kwa mtindo unaofanana.
Nakubaliana na maoni ya Balozi Abbas Kleist Sykes (akinukuliwa mwaka 2001), kwamba, “Maasi ya Jeshi la Tanganyika Rifles (TR) mwaka 1964, yalitokana kwa sehemu kubwa na kuchelewa kuwaondoa makamanda wa kizungu na kuwapandisha vyeo waafrika”, kama ilivyofanyika kwa Jeshi la Polisi na watumishi wengine serikalini. Na ndivyo ilivyokuwa kwa maasi ya Kenya na Uganda.
Wala haishangazi kwamba, viongozi wa vyama vya wafanyakazi waliungana na waasi awamu hii ya pili kutaka kuiangusha Serikali, kutokana na ukweli kwamba, tangu Mwalimu alipositisha zoezi la “Africanisation” Januari 1963, wao walikwishaapa mapema kutolala usingizi “mpaka kieleweke”. Kutokana na maasi hayo, Mwalimu alikifuta Kikosi chote cha Kwanza (Colito Barracks) na kuwafukuza kazi askari 100 wa kikosi cha pili, Tabora. Alifukuza pia 10% ya askari polisi 5,000 waliokuwapo, kwa kushindwa kutekeleza wajibu wao wa kudhibiti maasi.
Watu zaidi ya 400 walikamatwa na kuhojiwa, wakiwamo viongozi wa vyama vya wafanyakazi; na wengine 500 walitiwa nguvuni chini ya Sheria ya kuzuia hali ya hatari, lakini wengi waliachiwa.
lililokuwa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TFL) lilifutwa, badala yake kikaundwa Chama cha National Union of Tanganyika Workers (NUTA) kama Jumuiya ya Chama tawala – TANU. Mwalimu alimteua Mirisho Sam Hagai Sarakikya kuwa Mkuu mpya wa Jeshi na kumpandisha cheo kuwa Brigedia.
Mwanzoni mwa Aprili 1964, Majeshi ya Uingereza yaliondoka na nafasi yake kuchukuliwa na Kikosi cha Tatu cha Jeshi la Nigeria, chini ya Luteni Kanali James Pam. Sajini Francis Higo Ilogi alipatikana na hatia ya uasi wa Jeshi na kufungwa miaka 15, ambapo washirika wake wakuu 13 wakafungwa kifungo kati ya miaka 5-10.
Waswahili walisema, “Kila ovu lina baraka zake”. Mwalimu aliongeza kima cha chini cha mishahara kwa wanajeshi kutoka shilingi 105 hadi 240/= kwa mwezi. Lakini la muhimu kuliko yote ni kwamba, maasi hayo yalitusaidia kujihoji na kufahamu aina ya Jeshi lililotakiwa kwa nchi kama yetu. Yalituwezesha kujenga Jeshi upya, tukapata “Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania” (JWT), kwa maana halisi ya Jeshi la Wananchi kwa ajili ya Wananchi.
MWISHO...!!!
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena